“Let us also produce some bold act of our own—and join the ranks of the most emulated.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 98.13b
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIISHIE TU KUHAMASIKA, HAMASISHA PIA.
Kila mmoja wetu ana watu ambao wanamhamasisha, watu ambao wamefika pale ambapo mtu amefika.
Tunapoyaangalia maisha yao tunapata hamasa kubwa.
Tunaposoma vitabu vyao, moto wa hamasa kubwa unawaka ndani yetu, na kuona tunaweza kufika kule walikofika wao pia.
Lakini wengi huishia kwenye hamasa tu, na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida. Wakitaka hamasa tena wanarudi kuwaangalia watu hao na kusoma vitabu vyao, lakini hakuna hatua wanayopiga.
Wanaishia kuwa walevi wa hamasa, kila wakati kutaka kupata tena na tena lakini hakuna hatua yoyote wanayopiga.
Rafiki, kama unataka kupiga hatua kwenye maisha yako basi usiishie tu kuhamasika, bali pia unapaswa kuhamasisha wengine.
Kwa kujifunza kupitia anayekuhamasisha, hakikisha na wewe kuna watu unawahamasisha.
Na utawagamasisha siyo kwa maneno au hamasa yako, bali kwa hatua unazochukua.
Angalia yule anayekuhamasisha, je nini kinakuhamasisha kwake, maneno yake au matendo yake? Jibu lipo wazi, matendo yake ndiyo yanakuhamasisha.
Hivyo ili kuwahamasisha wengine, weka kwenye matendo yale unayopata kupitia anayekuhamasisha.
Kila unapomwangalia yule anayekuhamasisha, ondoka na kitu cha kwenda kufanyia kazi kwenye maisha yako, na hapo utatengeneza hamasa kwa wengine pia.
Na unapojikuta njia panda hujui ufanye nini, basi jiulize yule anayekuhamasisha angefanya nini kwenye hali kama hiyo.
Hapo utaweza kutumia hamasa yako kwa usahihi na kupiga hatua zaidi, huku pia ukiwahamasisha wengine.
Ukawe na siku bora ya leo, siku ya kuwa hamasa kwa wengine kupitia hatua unazochukua baada ya kuwa umehamasika.
#UsiweMleviWaHamasa, #GeuzaHamasaKuwaVitendo, #KuwaMfanoBoraKwaWengine
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha