Tumekuwa tunatumia maneno kwa mazoea na huwa hatuchukui hata sekunde chache kupima nguvu ya maneno hayo.

Kinachotokea ni kwamba baadhi ya maneno ambayo tumekuwa tunayatumia yamekuwa kikwazo kwetu kupiga hatua. Kwa kutumia baadhi ya maneno, tumekuwa tunajiwekea ukomo wenyewe.

Na baadhi ya maneno yanatupa hamasa ya kupiga hatua zaidi, yanatuonesha inawezekana na kutuwezesha kujaribu mambo ambayo hatujawahi kujaribu huko nyuma.

Rafiki, maneno yana nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu, hakuna neno tunalotumia ambalo haliachi alama fulani kwenye maisha yetu.

Hivyo maneno na kauli zetu ni eneo tunalopaswa kuwa na umakini nalo sana, tunapaswa kukagua kila neno kabla hatujalitumia, ili kuhakikisha tunatumia maneno sahihi na yenye manufaa kwetu.

Yapo maneno chanya, ambayo yanatuonesha uwezekano wa kitu na kutupa hamasa ya kujaribu na kupiga hatua. Maneno kama INAWEZEKANA, NAWEZA, NZURI, RAHISI, NAPENDA, MAFANIKIO, UPENDO ni maneno chanya na yenye nguvu ya kukusukuma kuchukua hatua zaidi.

Yapo maneno hasi, ambayo yanatuwekea ukomo kwa kuondoa kabisa uwezekano na kuzima hamasa iliyopo ndani yetu. Maneno kama HAIWEZEKANI, SIWEZI, MBAYA, NGUMU, SIPENDI, KUSHINDWA, HOFU ni maneno hasi na yenye nguvu ya kukuzuia usipige hatua zaidi.

Jukumu lako ni kuchunguza maneno unayotumia kila siku kwenye mazungumzo yako, na kuona mara ngapi unatumia maneno hasi na yaondoe kabisa kwenye mazungumzo yako. Neno lolote hasi na linalokupa ukomo hupaswi kulitumia kama kweli unataka kufanikiwa. Hata kama kila mtu analitumia na inakushawishi kuona ndiyo ukweli, wewe usilitumie.

Mfano kauli ya HALI NI NGUMU ni kauli maarufu sana kutumiwa na watu wengi, wengi wanalalamika hali ngumu na ukiangalia kweli kuna kila aina ya ushahidi wa kuonesha hali ni ngumu. Lakini wewe hupaswi kutumia kauli au neno hilo la ugumu, badala yake tumia kauli ya HALI NI NZURI, na hii itakuwezesha kuangalia upande mzuri wa hali hiyo.

Kufanya hivi siyo kwamba unajidanganya, badala yake unajilazimisha kuangalia upande mzuri wa kitu, ambao upo, hata kama mambo yanaonekana ni magumu au mabaya kiasi gani.

Chagua sasa maneno ambayo ni marufuku kuyatumia kwenye maisha yako, hata kama kila mtu anayatumia na yanaonekana ni sahihi. Kama neno linakupa ukomo au kukukatisha tamaa lifute mara moja kwenye maisha yako na usikae karibu na watu wanaitumia maneno ya aina hiyo.

Maisha ni yako, chagua kutumia maneno ambayo yanakuinua na kukupa hamasa au chagua maneno yanayokudidimiza na kukukatisha tamaa. Uchaguzi ni wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha