Rafiki yangu mpendwa,

Imekuwa ni mazoea kwa wengi kusingizia siku kwamba ndiyo zinatengeneza hali ambazo wanazo.

Labda ni jumatatu ambayo mtu anajisikia vibaya kwenye kazi zake na hapo kusingizia kwamba jumatatu siyo nzuri, na kuipa majina kama ‘blue monday’ na mengineyo.

Au ni ijumaa ambayo mtu anajisikia vizuri sana kwa mapumziko ya wiki anayoelekea na kuipa majina kama ‘furahi day’ na mengine kama hayo.

Rafiki, siku haitengenezi hali yoyote unayojisikia kuwa nayo, bali hali uliyonayo wewe ndiyo inatengeneza siku yako.

Kila siku inaanza na kuisha vile vile, jua linachomoza mashariki na kuzama magharibi, dunia inajizungusha kwenye mhimili wake na wakati huo huo inalizunguka jua. Dunia inaendelea na mambo yake na haijali leo ni jumatatu au ijumaa.

Hali uliyonayo ndiyo inayotengeneza siku yako. Kama unaianza siku yako ukiwa kwenye hali nzuri, hali ya furaha basi siku hiyo itakuwa nzuri sana kwako, utatekeleza majukumu yako vizuri na kuweza kupiga hatua. Tena utajiona ni mtu mwenye bahati.

Lakini kama utaianza siku yao ukiwa na hali mbaya, ukiwa hujisikii vizuri, una msongo na hasira, siku hiyo lazima itakuwa mbaya. Itakuwa siku ambayo kila kitu kinakwenda vibaya, hutaweza kukamilisha majukumu yako na utajiona mwenye kisirani kwa sababu kila unachojaribu kinashindikana.

Unachopaswa kujua na kukumbuka mara zote ni kwamba siku haitengenezi hali yako, bali hali yako ndiyo inatengeneza siku yako. Hivyo hakikisha unaianza kila siku ukiwa na hali nzuri, ianze siku kwa kupitia malengo yako, kupata mafunzo yanayokupa hamasa na hakikisha unaanza siku hiyo mapema.

Mtu mmoja amewahi kusema hizi ndizo siku za wiki ambazo zina bahati kubwa, alhamisi, jumanne, jumamosi, jumatano, jumapili, ijumaa na jumatatu. Ukizianza siku hizo ukiwa na hali nzuri basi utaweza kutimiza makubwa sana mpaka utajishangaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha