Chanzo kikuu cha hofu kwenye maisha yetu ni kukosa imani kwenye dunia na kwetu wenyewe.
Kuna kitu tunakuwa tunataka, lakini tunapoangalia nafasi ya kuweza kukipata, na hatari iliyopo kwenye kukikosa tunapata hofu kubwa.
Tunajiuliza vipi kama tukijaribu na tukashindwa, au vipi kama mambo yakienda tofauti na jinsi tulivyopanga?
Huwa tunataka kila kitu kiende kama ambavyo tumepanga sisi wenyewe, na chochote kikienda tofauti hofu kubwa inawaka ndani yetu na tunashindwa kuendelea.
Njia bora ya kupoteza kabisa hofu zako na kukupa nguvu ya kuendelea kuchukua hatua ni kuiamini dunia.
Amini kwamba dunia iko upande wako, amini kwamba chochote kinachotokea ni kwa manufaa bora zaidi kwako.
Usiipangie dunia iendeje, badala yake amini kwamba dunia itaenda kama inavyoenda, na kwa vyovyote vile, utakuwa na nafasi bora zaidi kwako kupata unachotaka.
Unapoweka malengo na mipango yako, usitake dunia ikupe kile unachotaka kwa namna unavyotaka, bali itake dunia ikupe kile unachotaka au chochote bora kuliko unachotaka. Kwa njia hii unakuwa huru, na hutaogopa pale mambo yanapokwenda tofauti, kwa sababu utajua dunia imechagua kukupa kilicho bora zaidi.
Hofu ni kitu kisichooneka, kisichosikika wala kushikika, ni hali unayoitengeneza ndani yako pale unapoona mambo yanakwenda tofauti na ulivyotegemea. Unapoiamini dunia na kuona ina nia njema na wewe, kwamba kila kinachotokea ni kwa manufaa bora zaidi kwako, hofu zinapoteza zenyewe.
Iamini dunia na hofu zitapotea zenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,