Mwangalie mtu yeyote anayelalamika kwamba maisha ni magumu na mambo hayaendi, na wote utakuta wana sababu moja nyuma ya ugumu huo wa maisha. Iwe ni wewe binafsi au watu wanaokuzunguka, ukiangalia lazima utaona sababu moja kubwa inayopelekea maisha kuwa magumu.
Sababu hiyo ni mazoea na ukawaida. Kufanya vitu kwa mazoea na kufanya kwa kiwango cha kawaida ndiyo chanzo kikuu cha maisha kuwa magumu na mambo kutokwenda.
Wote tunajua ya kwamba dunia inabadilika, hakuna kitu kinabaki kama kilivyokuwa hapo awali. Lakini sisi wenyewe hatutaki kubadilika, tunataka kuwa vile ambavyo tumezoa kuwa, tukifanya tulichozoea kufanya halafu tutegemee kupata matokeo mazuri.
Hapa ndipo ugumu wa maisha unapoanzia, unapotaka kila kitu kiwe kama ulivyozoea, unapokataa kubadilika na kufanya vitu kwa ubora zaidi. Utaweka juhudi sana lakini matokeo yanakuwa madogo, kwa sababu ulichozoea kimeshabadilika lakini wewe hutaki kubadilika.
Kama unataka kuachana na maisha magumu, anza kubadilika wewe mwenyewe, angalia mabadiliko ambayo yameshatokea kwenye kazi yako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla na kisha badilika ili kuendana na mabadiliko hayo.
Utakuwa mbele zaidi kama utayaona mabadiliko yanayokuja na kubadilika kabla mabadiliko hayajakulazimisha ubadilike.
Using’ang’ane na ulichozoea, angalia mabadiliko yanayoendelea na wewe badilika kadiri unavyopaswa kubadilika.
Pia ondoa ukawaida kwenye maisha yako, kazi zako na biashara zako. Chochote unachofanya, kifanye kwa upekee, kifanye kwa viwango vya juu sana. Usifanye chochote kwa kawaida, maana kawaida ni sawa na hovyo. Hakuna anayehamasika na kitu cha kawaida, kila mtu anahamasika na kitu cha kipekee, kitu cha tofauti.
Ondokana na mazoea na ukawaida na utasahau hadithi za maisha magumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,