“You say, good fortune used to meet you at every corner. But the fortunate person is the one who gives themselves a good fortune. And good fortunes are a well-tuned soul, good impulses and good actions.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.36
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Leo tumeipata fursa bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Njia pekee ya kunufaika na siku hii ni kuiishi kwa ukamilifu wake, kuishi kwa vipaumbele na kutopoteza muda kwa yale yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JINSI YA KUTENGENEZA BAHATI NZURI…
Huwa tunawaangalia wale waliopiga hatua kwenye maisha yao na kujiambia watu hao wana bahati nzuri.
Tunachoona ni kama vile watu hao walikuwa wamekaa na bahati ikawaangukia.
Kitu ambacho siyo sahihi, hakuna mtu ambaye bahati inamwangukia tu.
Bali wale wote ambao tunaona wamepiga hatua, wale ambao tunaona wana bahati, wametengeneza bahati hizo wao wenyewe.
Hivyo na wewe pia unaweza kujitengenezea bahati nzuri kwako.
Ili kujitengenezea bahati nzuri, anza kuwa mtu bora, kimwili, kiakili na kiroho. Huwezi kitengeneza bahati kama wewe mwenyewe haupo bora katika maeneo hayo matatu ya maisha yako.
Baada ya kuwa bora, hatua nyingine muhimu ni kuchukua hatua sahihi mara zote. Bahati inakuja kwa wale ambao wanachukua hatua, wale ambao wanafanya kitu na siyo waliokaa tu au wanaosema.
Hivyo chukua hatua, na utakutana ma bahati kupitia hatua unazochukua.
Kumbuka usemi kwamba bahati ni pale fursa inapokutana na maandalizi. Kumbe fursa huwa zinakuwa wazi kwa wote, ila wale tu wenye maandalizi ndiyo huweza kutumia fursa hizo. Hivyo kama unataka kuwa na bahati, basi hakikisha una maandalizi sahihi kwa fursa unazozilenga.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujitengenezea bahati nzuri, kwa kuwa mtu bora na kuchukua hatua sahihi, kwa kuwa na maandalizi sahihi kwa fursa unazozilenga.
BahatiInatengenezwa, #KuwaMtuBora, #KuwaNaMaandaliziSahihiKwaFursaUnazolenga
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha