Kama umekuwa unaona matangazo ya biashara ya kampuni mbalimbali, utakubaliana na mimi kwamba hakuna tangazo unaliona mara moja. Chukulia mfano wa kampuni za simu, kama unaishi maisha kawaida ya kutoka nyumbani kwako kwenda kwenye shughuli zako, utakutana na matangazo ya kampuni ya simu siyo chini ya mara kumi. Ukifungulia tv au redio utakutana na tangazo, ukisoma gazeti unakutana na tangazo, ukiwa njiani unakutana na mabango. Na kama hiyo haitoshi, kampuni husika ya simu watakutumia ujumbe na hata kukupigia simu kukuambia na kukukumbusha kuhusu huduma zao.

Unaweza kujiuliza kwa nini makampuni hayo yanahangaika hivyo kutangaza, si tayari yanajulikana, kwa nini yatumie gharama kubwa kuendelea kujitangaza? Na jibu ni moja, bila ya kurudia rudia kutangaza, watu huwa wanasahau haraka sana. Watu hawafikirii kitu kimoja, watu wamevurugwa na maisha yao, hivyo ukitegemea kuwaambia kitu mara moja na wakikumbuke kila wakati ni kujidanganya.

Sasa unapaswa kulitumia hili kwenye kazi zako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla.

Kama unafanya biashara, kwanza tengeneza hadithi ya biashara hiyo kisha waeleze watu kwa kurudia rudia, hadithi hii inakuwa sehemu ya kuitangaza biashara yako, inayowafanya watu wakumbuke na kurudi kwenye biashara yako. Kila biashara inaweza kuwa na hadithi fulani, ijue na kutengeneza yako na anza kuitumia kila wakati. Na pia kama unatangaza kupitia biashara yako basi hakikisha mpango wowote wa matangazo unaotumia unajirudia kwa muda mrefu na siyo mara moja. Mbobezi mmoja kwenye eneo la utangazaji amewahi kusema inamchukua mtu kukutana na tangazo lako mara saba ndiyo aamue kununua unachouza. Kwa zama hizi za kelele, ni zaidi ya hapo.

Kama kuna kitu unataka kubadili kwenye maisha yako, na unataka watu wajue na kukuunga mkono, inabidi useme kitu hicho na urudie rudie kusema mara nyingi. Kadiri watu wanavyosikia kitu mara nyingi kutoka kwako ndivyo wanavyoua kwamba uko makini na kitu hicho.

Kitu chochote muhimu kwako, ambacho unataka watu waelewe na kuchukua hatua, rudia kusema mara nyingi. Kadiri unavyorudia kusema ndivyo watu wanakuamini na kuona kweli unamaanisha.

Usitegemee kusema kitu mara moja au mara chache halafu watu wakakubaliana na wewe. Kuna wachache watakubaliana na wewe haraka, lakini wengi itawachukua muda. Kuwa mvumilivu na kuwa na utayari wa kurudia chochote mara nyingi uwezavyo na itakupa matokeo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha