Kuna wakati unakosa kabisa hamasa ya kuchukua hatua ili kufika kule unakotaka kufika. Wengi husubiri mpaka wapate hamasa ndiyo wachukue hatua. Lakini kuhubiri siyo njia sahihi ya kupata hamasa. Badala yake unapaswa kufanya kitu, na hicho huzalisha hamasa ya kukuwezesha kufanya zaidi.
Kuna wakati unajikuta njia panda na hujui ni kitu gani sahihi hufanyi. Hali hii inakufanya ukwame na usichukue hatua yoyote. Lakini kukwama huko hakuna msaada wowote kwako, maana kutokuchukua hatua yoyote, hakutasaidia hali uliyonayo. Unachopaswa kufanya pale unapojikuta njia panda ni kufanya chochote, kufanya chochote kunakuweka kwenye mwendo, wa kukuwezesha kufanya zaidi.
Kuna wakati mtu unajiona bado hujawa tayari, bado unahitaji maandalizi ndiyo uanze kufanya. Lakini kama maandalizi hayo yanakupelekea kusubiri, hayatakuwa bora kwako. Badala yake unapaswa kufanya kitu na hicho kitakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Rafiki, kufanya kitu ni dawa ya mambo mengi, kwa sababu ufanyaji una nguvu kubwa kuliko kitu kingine chochote.
Ni bora kufanya kitu kwa kukosea kuliko kutokufanya kabisa, kwa sababu kufanya kwa kukosea unajifunza, lakini kutokufanya kabisa hakuna unachojifunza.
Jiwekee utaratibu wa kukusukuma kufanya kitu unapojikuta kwenye hali za kukwama na kusubiri, hilo litakuwezesha kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,