Watu wengi wamekuwa wanasema wanapenda kufanya tahajudi, lakini wanaona hawana muda wa kukaa na kutulia kufanya tahajudi.

Mtu mmoja amewahi kusema kama huwezi kutenga dakika kumi za kufanya tahajudi, basi unapaswa kujilazimisha kutenga dakika 20. Kwa sababu kama huwezi kupata dakika kumi basi maana yake maisha yako yamevurugwa sana kiasi kwamba unapaswa kuchukua hatua kubwa zaidi.

Lakini hata tukikubaliana na wewe kwamba unapenda tahajudi lakini unachokosa ni muda au mazingira tulivu ya kufanya hivyo, bado una uwezo wa kunufaika na tahajudi.

Unaweza kunufaika na tahajudi kwa kuchagua kufanya kila kitu kwa tahajudi. Kila kitu unachofanya kwenye siku yako, kichukilie kama nafasi ya wewe kufanya tahajudi.

Kila unachofanya, weka mawazo yako yote pale, weka umakini wako wote, usikubali mawazo yako yazurure sehemu nyingine yoyote. Weka umakini na fuatilia sana hatua ya kila kitu unachofanya. Hapo siyo tu utapata utulivu, lakini utafurahia sana kile unachofanya.

Mfano unaweza kuchukulia zoezi la kula kama tahajudi, unapochota chakula unaona kabisa ni kiwango gani umechota, unapoweka mdomoni unasikia harufu na ladha yake, unapotafuna unazidi kupata ladha yake na unapomeza unasikia chakula hicho kikielekea tumboni. Hufikirii kitu kingine bali chakula unachokula, mawazo yako yote yanakuwa kwenye zoezi hilo la kula.

Kwa tahajudi ya aina hii unapata utulivu mkubwa, unaondokana na hofu na kuweza kufurahia kile ambacho unafanya.

Chanzo kikuu cha hofu na msongo kwenye maisha ni kuruhusu mawazo yako yatoke kwenye kile unachofanya. Yaani unafanya kitu kimoja lakini mawazo yako yapo kwenye kitu kingine tofauti kabisa. Kwa kuweka tahajudi kwenye kila unachofanya, utaweza kuondokana na hofu na msongo wa mawazo.

Weka umakini wako kwenye kile unachofanya, usisumbuke na yaliyopita maana huwezi kuyabadili na wala usisumbuke na yajayo maana hakuna unachoweza kufanya kuyaathiri. Kuwa pale ulipo sasa, kwa kufanya kile unachofanya sasa na kutokusumbuka na kilicho nje ya hapo ulipo sasa. Hivi ndivyo unavyoweza kufanya kila kitu kuwa tahajudi na hata kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha