Siri ya kwanza ya mafanikio ni wewe kuwapenda wale waliofanikiwa. Huwezi kuwa tajiri kama unawachukia matajiri, kwa sababu akili yako itakuepusha na kila fursa ya kukufikisha kwenye utajiri, kwa sababu imani yako ni kwamba utajiri ni mbaya.
Hivyo tunapaswa kuwapenda sana watu waliofanikiwa, na kusikiliza ushauri wao, kwa sababu wana uzoefu mkubwa kwenye kile wanachofanya ndiyo maana wakafanikiwa. Hilo ni kweli kabisa, kwamba wana uzoefu mkubwa.
Lakini kuna kitu kimoja ambacho wengi wamekuwa hawakielewi kuhusu watu waliofanikiwa, watu hawa wana unafiki mkubwa. Wana unafiki mkubwa siyo kwa sababu hawataki na wewe ufanikiwe, bali wanatumia unafiki huo kuepusha usumbufu usio na umuhimu kwao.
Mfano watu wengi waliofanikiwa, kwenye hadithi zao za mafanikio wanakueleza yale mambo ambayo unataka kuyasikia, na siyo uhalisia wa maisha yao.
Hujawahi kujiuliza kwa nini hadithi zote za mafanikio zinafanana, kwamba mtu alianzia juu, akaweka juhudi sana kwenye kazi na hatimaye akafanikiwa?
Hizo ni hadithi, lakini uhalisia wa dunia hauendi hivyo. Vitu ambavyo watu hawa hawatakuambia ni gharama kubwa waliyolipa kwenye maisha yao katika kuyapata mafanikio yao.
Wakikuambia kwamba ndoa zao zimevunjika, watoto wao hawawapendi, hawana marafiki wengi, wamekuwa wanalala muda mchache kuliko uhitaji wa kawaida na mengine kama hayo, mara moja utaanza kuhukumu maisha yao.
Utaanza kusema hayo mafanikio yana maana gani, bora nikae na familia yangu lakini siyo kufanikiwa na kupoteza familia. Au bora nikae na afya yangu lakini siyo kufanikiwa na kuipoteza.
Kuondokana na hukumu hizi ambazo watu wasiofanikiwa wanapenda kuzitoa kwa wale waliofanikiwa, basi waliofanikiwa wamejifunza kuweka unafiki kidogo kwenye hadithi zao, kwa njia njema kabisa ya kuondoa usumbufu kwao na kuwafanya watu wa kawaida na wao ipo siku watafanikiwa.
Kama utachukua muda wa kuyafuatilia kwa karibu maisha ya walioanikiwa, utaona jinsi ambavyo wamelipa gharama kubwa sana kufika pale walipofika. Utaona jinsi ambavyo maeneo fulani ya maisha yao yameharibiwa na mafanikio yao.
Kwa kifupi hakuna mtu aliyepata mafanikio makubwa ambaye ni wa kawaida, anayeishi maisha yanayokubalika na kila mtu, hayupo, hatakuja kuwepo. Na kama unajiambia utakuwa na mafanikio makubwa huku kila mtu anakubaliana na wewe, unajidanganya.
Zipo gharama nyingi na kubwa za kulipa ili kupata mafanikio, ili kufika pale ambapo umepanga kufika kweli. Na ukitaka kuzijua usisikilize kile ambacho watu waliofanikiwa wanakuambia, badala yake angalia nini walifanya kwenye maisha yao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kweli kabisa cocha kila mafanikio yana gharama zake.
LikeLike
Hakika kama unataka kukubalika na kila mtu mafanikio kwako yatabaki ndoto tu
LikeLike
Kabisa.
LikeLike