Chuki ni moja ya hisia zenye nguvu kubwa sana kwetu wanadamu. Hisia za chuki huwa zina nguvu kubwa kwa anayekuwa nazo, lakini pia zinampa nguvu yule ambaye hisia hizo zimeelekezwa kwake.
Watu waliogundua nguvu hii ya chuki, wameweza kuitumia vizuri kuwa maarufu na kuwatumia wengine kupiga hatua zaidi.
Angalia wasanii maarufu sana ambao hawana kitu chochote cha msingi wamefanya kwenye maisha yao, umaarufu wao unatokana na kuibua hisia za chuki baina ya wafuasi wa wasanii hao. Wanafanya kitu ambacho kitafanya baadhi ya watu wawachukie (wanaita ‘kiki’) na kadiri watu wanavyowachukia ndivyo wanavyowazungumzia na kuwafuatilia zaidi na hapo umaarufu wao kukua.
Kadhalika kwa wanasiasa, umaarufu wao unategemea sana jinsi ambavyo wanaweza kuibua hisia kazi za chuki kwa sehemu fulani ya watu, watu hao wanapowapinga na kuwazungumzia na hata kuwafuatilia kuona ni mambo yapi mengine mabaya wanafanya, umaarufu wao unakua.
Vitu viwili muhimu sana vya kuondoka navyo hapa;
Moja; usitafute umaarufu kwa kuibua hisia za chuki kwa watu, umaarufu wa aina hii huwa hauna msingi wowote. Wewe ishi maisha yako, fanya kilicho sahihi, jitume zaidi mara zote na kama umaarufu unakuja, utakuja wenyewe, lakini siyo kwa kuutafuta.
Mbili; usikubali kuingia kwenye mtego wa wanaotafuta umaarufu kwa kuibua hisia za chuki ndani yako. Na siyo lazima wawe watu maarufu, hata watu wa kawaida kwenye maisha yako, wakitaka uwafuatilie sana wanaibua hisia za chuki ndani yako. Dawa sahihi ya kuepuka kuingia kwenye mtego huu wa kuibua hisia unaotegwa na wengine ni kuwapuuza. Pale mtu anapofanya jambo la hovyo au la kijinga kabisa, unajifanya kama hata hujaona au kusikia, wewe unaendelea na maisha yako kama vile hakuna kilichotokea. Hapo mtu huyo atakosa nguvu kabisa na hataweza kukuweka kwenye udhibiti wako.
Kama wananchi wote wangeweza kuwa na hili, wakakazana na maisha yao na kazi zao, tusingekuwa na watu wenye umaarufu usio na tija. Lakini kwa kuwa watu wengi hawana umakini na maisha yao, ni rahisi kuingia kwenye mitego ya wale wanaotafuta umaarufu kwa kuibua hisia za chuki.
Usiwe mmoja kati ya hao wengi ambao hawana umakini na maisha yako. Kuwa tofauti, puuza chochote kisicho na msingi au manufaa kwako. Usiwe na chuki na mtu yeyote yule, peleka nguvu zako kwenye kuyaboresha maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,