Muda unazidi kuwa changamoto kwa wengi, mambo ya kufanya ni mengi na muda wa kufanya mambo hayo ni mchache.
Hili limekuwa likileta msongo kwa wengi, ambao wanakazana kufanya kila wanachotaka kufanya, lakini wanashindwa kutokana na muda kutokutosha.
Wengi wanabaki kulaumu muda na kujiambia kama wangepata muda wa kutosha basi wangeweza kukamilisha mambo mengi zaidi kwenye maisha yao.
Lakini unapokuja kuangalia kwa umakini, unagundua tatizo kubwa halipo kwenye muda, bali tatizo lipo kwenye yale tunayofanya kwa muda tunaokuwa nao.
Ukishagundua kwamba una mambo mengi ya kufanya kuliko muda ulionao, unachopaswa kufanya siyo kukazana kufanya kila kitu, bali kuweka vipaumbele, kipi cha kufanya na kipi cha kuacha.
Unapaswa kujiuliza ni yapi matumizi sahihi ya muda mchache ulionao, na hapo kulinganisha yote unayotaka kufanya ili kupata yale muhimu zaidi kufanya.
Ukichagua kuipitia siku yako yoyote ile, na ukaorodhesha kila ulichofanya kwenye siku hiyo, kisha kuanza kupitia kimoja kimoja na kupima umuhimu wake, utagundua kuna vitu vingi ambavyo umekuwa unafanya kwa kuzoea, lakini havina manufaa yoyote kwako.
Hivi ndiyo vitu ambavyo vinaiba muda ambao ungeweza kuutumia kufanya mambo muhimu.
Hivyo kabla hujaendelea kujipa sababu kwamba huna muda wa kufanya yake muhimu, chagua siku moja na andika kila unachofanya kwenye siku hiyo, tangu unapoamka mpaka unaporudi kulala. Njia hii itakuonesha mambo mengi yanayopoteza muda wako wa thamani.
Unao muda wa kutosha kufanya kila unachotaka kufanya, muhimu ni kuwa na vipaumbele sahihi kwenye kufanya mambo yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,