Kila mtu anataka kupata fedha zaidi, lakini ni wachache sana ambao wanapata fedha wanazotaka kwenye maisha yao.
Hii ni kwa sababu wengi hawajui msingi sahihi wa fedha. Wengi wamekuwa wanakimbizana na fedha na hivyo hawazikamati, kwa sababu fedha zina kasi kuliko wao.
Wachache wanazipata fedha wala hawazikimbizi, badala yake wanazivutia. Fedha zinakuja kwao kwa sababu kuna sumaku ya fedha ambayo wanayo.
Tunaweza kuchukulia kupata fedha kama kipepeo. Kipepeo kizuri kila mtu anakitamani, lakini ukisema ukikimbize ili kukipata, hutakikamata, maana kitaruka juu na juu na kitakuchosha. Lakini kipepeo hicho kinapoona ua zuri, kinajipeleka chenyewe na kutua pale. Kinaenda chenyewe kwenye ua zuri bila ya kulazimishwa au kufukuzwa.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa kwenye fedha, badala ya kuzikimbiza basi unazivutia.
Na njia pekee ya kuvutia fedha kwako ni kujijengea tabia bora kifedha.
Fedha ni zao la tabia zifuatazo;
- Uaminifu, kadiri unavyokuwa mwaminifu, ndiyo wengi wanayokuamini na kukupa fedha zaidi.
- Mbobezi, kadiri unavyobobea kwenye kile unachofanya, ndivyo wengi zaidi wanataka kukupa fedha ili wanufaike na ubobezi wako.
- Ubunifu, kadiri unavyokuwa na ubunifu, ndivyo unavyokuja na vitu vipya na bora na vinavyokuwezesha kupata fedha zaidi.
- Wema, watu ambao ni wema wanawavutia wengi upande wao na kuweza kutengeneza kipato zaidi.
- Afya, watu wenye afya bora wanaweza kujituma zaidi na hivyo kutengeneza kipato zaidi.
- Mawasiliano, wale wanaoweza kuwasiliana vizuri ndiyo ambao wanaeleweka na wengi na kuweza kushawishi wengi na hivyo kupata fedha zaidi.
- Mahusiano, wale wanaoweza kutengeneza mahusiano bora na wengine ndiyo wanaokuwa na mtandao mkubwa na hivyo kupata kipato zaidi.
- Nidhamu, wale wenye nidhamu ya kujisimamia wenyewe, kujituma, kutekeleza walichoahidi na kufanya walichopanga bila ya kuahirisha ndiyo wanaopata fedha zaidi.
- Kuziona fursa, wale ambao wana jicho la kuziona fursa, ambao mara zote wanajua kinachoendelea ndiyo wanaonufaika na fursa mpya zinazojitokeza na kupata fedha zaidi.
- Kuchukua hatua, wale ambao wanachukua hatua mara moja kwenye yale muhimu, bila ya kuchelewa au kuahirisha ndiyo wanaotengeneza kipato kikubwa.
Tabia hizo kumi ni rahisi kuzitaja na kuzielewa, lakini ngumu kujijengea, na ndiyo maana wengi hawatengenezi kipato cha kutosha.
Wajibu wako ni kujijengea tabia hizi, acha kabisa kukimbizana na fedha na kazana kujijengea tabia hizo kumi, utashangaa jinsi ambavyo fedha zitakuwa zinakuja zenyewe kwako, bila hata ya kuzikimbiza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,