Huwezi kufanikiwa kama huna misingi na maadili unayoyasimamia kwenye maisha yako, kazi zako na hata biashara ambazo unafanya.
Lakini pia unapokuwa na misingi hii, mambo hayatakuwa rahisi.
Dunia inapojua kwamba kuna misingi unaiishi na kuisimamia, huwa inakupa majaribu kwenye misingi hiyo.
Inakuletea njia na fursa za kunufaika zaidi, kama tu utakwenda kinyume na misingi hiyo.
Na huu ndiyo wakati sahihi wa wewe kusimamia misingi na maadili yako.
Wakati ambapo unajaribiwa, wakati ambapo maisha yanakuwa magumu kwa kusimamia misingi na yanaweza kuwa rahisi kama utavunja misingi yako, ndiyo wakati ambao unapaswa kuisimamia zaidi misingi hiyo.
Wakati wa majaribu ndiyo wakati wa kupikwa kwa ajili ya mafanikio makubwa, kama utaweza kuyavuka majaribu hayo bila ya kuvunja misingi yako, utakuwa umeiva na tayari kwa kupokea mafanikio makubwa kwako.
Lakini kama utaivunja misingi hiyo ili kurahisisha mambo, hutaweza kufanikiwa, kwa sababu kila wakati utaendelea kushawishiwa kuivunja misingi hiyo. Na ukishavunja misingi yako mara moja basi jua utaivunja tena na tena na tena.
Kila wakati fanya kile kilicho sahihi kulingana na misingi yako. Hata kama mambo ni magumu kiasi gani, kwa kujua umefanya kilicho sahihi, kunakupa amani ya kuendelea kupambana. Lakini kama utavunja misingi yako, hata kama mambo yatakuwa rahisi, wewe mwenyewe utajiona kama msaliti na hutajiamini kama mwanzo.
Wakati wa majaribu ndiyo wakati sahihi kwako kusimamia misingi na maadili uliyojijengea, na ndiyo kitu pekee kitakachokuwezesha kuvuka majaribu na kufikia mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,