Watu wengi wanaoanza kitu na kushindwa mwanzoni huona kama ni kitu kibaya kwao, huona kama ni kiashiria kwamba kitu hicho siyo sahihi kwao.
Lakini huo siyo ukweli, kushindwa mapema kwenye kile unachofanya siyo kiashiria kwamba huwezi au siyo sahihi kwako, bali ni zawadi kubwa kwako.
Makosa yoyote unayoyafanya mwanzoni mwa kitu, madhara yake ni madogo kuliko yale utakayokuja kufanya baadaye.
Kwa mfano kama umeanza biashara ukiwa na mtaji wa milioni tano, ukafanya kosa ambalo linakupa hasara ya milioni moja, ni kiasi kikubwa cha fedha na kinachoumiza. Lakini fikiria kama ungeshakuwa umekuza sana biashara hiyo, mtaji ukafika milioni 50 na hasara kosa ulilofanya likaleta hasara ya milioni kumi! Huoni kwamba kosa hilo hilo limekuwa na madhara makubwa zaidi baadaye?
Hii ndiyo sababu ni muhimu sana ushindwe mapema na ushindwe haraka, kwa sababu utajifunza mengi unaposhindwa mapema ambayo yatakuzuia usirudie makosa hayo baadaye na kushindwa zaidi.
Kadiri unavyofanikiwa zaidi, ndivyo kosa dogo unalifanya linakugharimu kiasi kikubwa. Kadiri kipato chako kinavyokua, ndivyo kosa dogo unalofanya linaleta hasara kubwa.
Hivyo lengo lako wewe ni kujifunza mapema, kupitia makosa unayofanya na kushindwa, lakini pia kupitia makosa ya wengine.
Kila kosa unalofanya kwenye safari yako ya mafanikio, kila unachoshindwa, chukulia hilo kama darasa. Hasara unayopata chukulia kama ada unayolipa ili kujifunza na kujizuia usikutane na magumu zaidi baadaye.
Shindwa mapema na shindwa haraka ili ujijengee kinga na kupunguza hasara za baadaye.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,