Kuuza ndiyo kitu ambacho kila mmoja wetu anafanya hapa duniani.

Kila mtu kuna kitu anauza, iwe anajua au hajui, lakini wote tunauza. Kama una biashara unauza bidhaa na huduma kwa wateja wako. Kama umeajiriwa unauza muda na utaalamu wako kwa mwajiri. Na kama ni kiongozi unauza sera na maono yako kwa wafuasi wako.

Hii ina maana kwamba kama tunataka kufanikiwa, kitu cha kwanza tunachopaswa kujifunza na kubobea ni mauzo. Kadiri unavyokuwa mzuri kwenye kuuza ndivyo unavyoweza kufanikiwa zaidi.

Lakini watu wengi wamekuwa wanaogopa sana kuuza. Wengi wamekuwa wanaona aibu kujinadi kwa kile wanachofanya, hasa kwa wale wanaoweza kunufaika na kitu hicho.

Ninachokuambia wewe rafiki yangu ni usiogope kuuza, usione aibu kujinadi kwa kile unachofanya kwa wale wanaoweza kunufaika nacho.

Hebu fikiria labda una shida fulani, na hujui utaitatuaje, ukaja kugundua kuna mtu anayeweza kutatua shida hiyo ila amejificha, si utaona ni mbinafsi kabisa?

Basi hicho ndiyo unachofanya pale unapoogopa kuuza. Kama una bidhaa au huduma au uzoefu ambao unamwezesha mtu mwingine kutoka pale alipokwama sasa, lakini humsaidii akaijua, ni ubinafsi.

Ili kuuza zaidi, kwanza jichukulie kama mtu ambaye una kitu chenye manufaa kwa wengine. Kisha chagua watu ambao utawafanya wao kuwa kazi yako. Yaani chagua watu ambao umeamua kuwatumikia, kwa kuwapa bidhaa, huduma au uzoefu wako na waweze kupiga hatua zaidi.

Unapojipa jukumu hili kubwa la maisha ya wengine kukutegemea wewe, aibu ya kuuza inaondoka kabisa na unakuwa ni wajibu wako kuhakikisha kila anayehusika na unachofanya basi anakijua na kuja kunufaika nacho.

Tengeneza maelezo mazuri ya kile unachofanya na namna kinavyomsaidia mtu kupiga hatua, kisha weka juhudi kuhakikisha watu wengi wanaoweza kunufaika na unachofanya wanajua kuhusu uwepo wako na kile unachofanya.

Usiogope kuuza, kuuza ndiyo maisha na mafanikio yako yanategemea sana mauzo yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha