Mahusiano ndiyo jina la mchezo, mahusiano ni kiungo muhimu sana kwenye mafanikio yako. Kuanzia kwenye familia, kazi na hata biashara. Mafanikio yako yanategemea sana ubora wa mahusiano yako.
Nimekuwa nakuambia kwamba kujenga mahusiano kunahitaji vitu viwili vikubwa, muda na kujali. Lazima uweke muda kwenye mahusiano kama unataka yakue. Na muhimu zaidi, lazima ujali sana kuhusu wale ambao upo nao kwenye mahusiano, iwe ni mahusiano ya kifamilia, kikazi au kibiashara. Kadiri mtu mwingine anavyoona anajaliwa, ndivyo anavyojali pia kuhusu wewe.
Lakini ipo tabia moja kubwa ambayo imekuwa inaharibu sana mahusiano ya wengi. Wengi wamekuwa wanaishi tabia hii kwa mazoea, lakini wasijue kama ina madhara kwenye mahusiano yao.
Tabia hiyo ni kila wakati kuwa mtu mwenye uhitaji wa kitu fulani kutoka kwa wale ambao uko nao kwenye mahusiano. Kila wakati kuna kitu unataka wakupe au wakusaidie, na unaona ni jukumu lao kufanya hivyo. Unakuwa mtu wa kunung’unika na kulalamika pale ambapo hupati kile ambacho ulitaka kupata kutoka kwa wengine.
Tabia hii inaua sana mahusiano ya wengi, kwa sababu wale ambao wanakuwa wanahitajika kutoa zaidi kwa wengine wanachoka na kuwaona wale wenye uhitaji kama mzigo kwao.
Hebu wewe mwenyewe fikiria, kuna mtu ambaye kila wakati kuna kitu anahitaji kutoka kwako, na asipokipata anaonekana kutoridhika na kuona kama humjali. Mwenyewe utajikuta unamkwepa ili kuondokana na majuto anayotaka kukutengenezea.
Hatua za kuchukua ili tabia hii isiwe kikwazo kwako, tengeneza mahusiano bora ambayo utawapa watu wengine uhuru. Wajue mahitaji yako ni yapi na wao wenyewe wasukumwe kuyatimiza, lakini pia na wewe ujue kipi unatoa kwa ajili ya wengine na ukitoe. Kwa namna hii mahusiano yanakuwa sawa, kila mtu kuna kitu anatoa kwa mwingine na kipo anachopokea pia.
Mahusiano yanakuwa na uhuru mkubwa na hakuna mtu mmoja anayekuwa tegemezi zaidi na kuonekana kama mzigo.
Kwenye kila aina ya mahusiano, kila mtu kuna kitu anaweza kutoa na anachoweza kupokea. Badala ya kuangalia zaidi unachopokea, hebu kazana kuangalia unachotoa na utaweza kuwa na mahusiano bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,