Moja ya vitu vinavyotukatisha tamaa kwenye maisha ni pale tunapoona kwamba maisha yetu ni magumu kuliko ya wengine. Hapa ndiyo tunaona labda sisi hatuna bahati na hivyo kukata tamaa.
Lakini ukiangalia kwa undani, hakuna mtu yeyote ambaye maisha yake ni rahisi kuliko yako. Kila mtu kuna mambo anapambana nayo kwenye maisha yake.
Kila unachopitia wewe, jua kuna wengine wanakipitia pia, tena kwa viwango vikubwa kuliko unavyopitia wewe.
Kwa hofu ulizonazo wewe, jua kila mtu ana hofu zake pia. Wewe unaweza kuwa na hofu unapata wapi fedha, mwingine akawa na hofu anatunzaje fedha alizonazo. Hakuna ambaye hana hofu kabisa.
Kwa magumu unayopitia wewe kwenye maisha yako, kazi na hata biashara, kila mtu kuna magumu yake anayopitia pia. Kila mtu kuna vita yake anapigana. Hakuna ambaye mambo ni rahisi kwake kama unavyofikiri.
Hivyo pale mambo yanapokuwa magumu kwako, badala ya kuangalia wengine na kufikiri mambo ni rahisi kwako, weka nguvu zako kwenye hatua sahihi kwako kuchukua kwa mambo yalivyo sasa. Hii ndiyo njia pekee itakayokuwezesha kupiga hatua zaidi.
Na wale unaowaona kama mambo siyo magumu kwao, wale unaowaona wanacheka na kufurahi, wale unaowaona wanaweka picha za mambo mazuri mitandaoni, usiwaonee wivu na kuona mambo yao ndiyo mazuri. Ukipewa maisha yao unaweza kuyatamani maisha yako mara mia.
Shukuru kwa maisha uliyonayo na kila siku kazana kuchukua hatua kuwa bora zaidi. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuwa na maisha bora. Hakuna wakati changamoto zote zitaisha, hakuna wakati utapata kila unachotaka, lakini kama bado upo hai, una nafasi ya kuwa bora zaidi kila siku mpya unayoipata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,