Watu wanapenda sana kuhusisha mafanikio na bahati.
Kwamba wale waliofanikiwa wana bahati fulani ambayo wale ambao hawajafanikiwa hawana.
Nimekuwa nakuambia mara kwa mara kwamba bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa.
Wakati unaona kwa nje mtu kakutana na fursa nzuri na kuitumia kufanikiwa, ambacho huoni ni maandalizi ambayo mtu huyo alifanya huko nyuma ambayo yalimweka kwenye nafasi nzuri ya kunufaika na fursa iliyojitokeza.
Hivyo kama unataka uwe na bahati kwenye maisha yako, mara zote kuwa na maandalizi kwa fursa zile unazozilenga.
Lakini ipo njia nyingine moja ya wewe kujiongezea bahati.
Njia hiyo ni kuwa na mtazamo chanya, mtazamo wa uwezekano, mtazamo wa kufanya makubwa.
Unapokuwa na mtazamo chanya, unaona uwezekano mkubwa pale wengine wanapoona kutokuwezekana, unaona mwanga pale wengine wanaona giza, na unapata matumaini wakati wengine wamekata tamaa. Mtazamo chanya utakuwezesha kujisukuma zaidi wakati wengine wameshaacha na hapo ni rahisi kwako kukutana na fursa nzuri, ambayo wengine wataita ni bahati.
Lakini pia mtazamo chanya unawavuta watu sahihi kwako. Kwa sababu watu wanakufanyia kile ambacho unajifanyia mwenyewe, wanakupa kile ambacho utakivumilia. Unapokuwa na mtazamo chanya muda wote, unawavutia wale wenye mtazamo chanya na wanakufanyia mambo ambayo ni chanya. Hili linakuletea fursa nyingi ambazo zitaonekana ni bahati kubwa kwako.
Jijengee mtazamo chanya utakaouishi kila siku bila ya kutetereka na utaweza kuvuta fursa bora sana kuja kwako kitu ambacho wengine wataona ni bahati.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,