“The task of a philosopher: we should bring our will into harmony with whatever happens, so that nothing happens against our will and nothing that we wish for fails to happen.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.14.7

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari TUMIA VIZURI KILA KINACHOKUJA KWAKO…
Kila kitu kinachokuja kwenye maisha yako,
Kila matokeo ambayo unayapata, iwe unayapenda au huyapendi,
Una nafasi ya kuweza kuyatumia vizuri na yakafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Kama kuna mahali unawahi na ukakwama kwenye foleni, badala ya kujilaumu na kulalamikia foleni ambayo huwezi kuibadili, unaweza kutumia muda huo kupumzika na kutuliza akili yako.
Kama upo njiani na mtu akakaribia kusababisha ajali ambayo ingeondoa uhai wako, badala ya kukasirika na kuona watu hawana maana, unaweza kushukuru kwa kuepushwa na ajali hiyo, kukumbuka utamu wa maisha na pia kuwa makini zaidi wakati mwingine.

Kuna mtu amekuahidi kitu halafu hakutimizi, unaweza kumlaumu utakavyo, lakini hilo halitasaidia. Badala yake unaweza kujifunza kutoweka mategemeo yako yote kwenye ahadi za wengine.

Hakuna chochote kinachotokea kwenye maisha yako ambacho huwezi kukitumia vizuri na kikakusukuma mbele zaidi.
Umekuwa unachukulia vitu kirahisi sana na ndiyo maana vingi vinakukwamisha.
Anza leo kutumia kila hali vizuri, jilazimishe kuona uzuri kwenye kila jambo linalotokea kwenye maisha yako, hata kama unaliona ni baya kiasi gani.
Dhumuhi la maisha ni kugeuza kila unachokutana nacho kuwa cha manufaa kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia kila kinachotokea kwenye maisha yako kwa manufaa yako.
#KilaKituKinatokeaKwaKusudi #MaishaHayanaBahatiMbaya #GeuzaKilaKinachotokeaKuwaChanyaKwako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1