Umeme ni mtiririko wa elektroni ambazo zinatoka eneo moja kwenda eneo jingine. Elektroni hizo zitakaa kwenye mtiririko wake bila ya kuzalisha chochote mpaka pale zitakapokutana na ukinzani. Taa ni ukinzani kwenye umeme, inazuia mtiririko wa elektroni na hivyo kuzalisha mwanga na joto.

Ili ndege iweze kuruka hewani, inahitaji sana ukinzani wa hewa angani. Japokuwa ukinzani huu ndiyo unafanya ndege itumie nishati kubwa kuruka hewani, lakini kama usingekuwepo kabisa ndege isingeweza kuruka hewani. Hivyo ukinzani wa hewa angani ndiyo unafanya kuwepo na mwendo wa ndege na viumbe wengine warukao.

Dunia ina nguvu ya ukinzani, unapotembea juu ya dunia, nguvu ya ukinzani ya dunia inazalisha msuguano kati yako na dunia. Hii ndiyo inasababisha viatu tunavyovaa viharibike na hata kuisha. Unaweza kusema maisha yangekuwa rahisi sana kama kusingekuwa na ukinzani kabisa, lakini nikutahadharishe, tusingeweza kutembea, tungekuwa tunateleza tu kila mahali.

Kadhalika kwenye uendeshaji wa mashine, magari na kila kitu, kuwasha gari unatumia nguvu ya ukinzani, unaposhika breki ili gari isimame unatumia nguvu ya ukinzani.

Sasa turudi kwenye maisha yetu ya kawaida, ukinzani ndiyo unaotuwezesha kukua zaidi. Tangu unazaliwa mpaka ulipofika sasa, umekuwa unakutana na kila aina ya ukinzani na ndiyo umekuwezesha kukua mpaka kufika hapo ulipo sasa.

Hali hii itaendelea kwenye maisha yako, kwenye kazi zako na hata biashara zako, kila hatua unayopiga unakutana na ukinzani. Unapokutana na ukinzani usiumie na kuona huwezi tena kupiga hatua, badala yake furahia na pokea hiyo kama nafasi ya wewe kukua zaidi.

Bila ya ukinzani hakuna mwendo, bila ya mwendo hakuna ukuaji. Karibisha kila ukinzani kama nafasi ya wewe kupiga hatua na kukua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha