Rafiki yangu mpendwa,

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi inayoitwa Social Security Administration, ya nchini Marekani, zinaonesha kwamba ukiwachukua watu 100 wanaoanza kazi au biashara na kisha kuwafuatilia kwa miaka 40 mpaka pale wanapostaafu, hiki ndiyo utakachokiona; mmoja pekee ndiyo atakuwa na utajiri mkubwa, wanne watakuwa na uhuru wa kifedha, 5 bado watakuwa wanafanya kazi kwa sababu wakiacha hawana fedha, 36 watakuwa wamekufa, 54 watakuwa masikini na tegemezi kwa watu wao wa karibu kuweza kuendesha maisha yao.

Kwa kifupi ni kwamba katika watu wote ambao wanafanya kazi au biashara, ni asilimia 5 pekee ndiyo wanaokuwa na mafanikio na utajiri wa kuwawezesha kuwa na maisha yenye uhuru kwao. Asilimia 95 wanakuwa na maisha magumu sana, wanakuwa kwenye umasikini na kukosa kabisa uhuru wa maisha yao.

rich vs poor 2

Sasa swali moja muhimu ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza ni hili, unawezaje kuondoka au kuepuka kuwa kwenye kundi la asilimia 95 na kwenda kwenye kundi la asilimia 5? Kwa maneno mengine unawezaje kutoka kwenye umasikini na maisha magumu na kwenda kwenye utajiri na uhuru wa kifedha?

Na hapa ndipo mwandishi na mhamasishaji Hal Elrod anapotushirikisha hatua tatu ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzitumia kutoka kwenye umasikini mkubwa na kwenda kwenye utajiri. Kupitia kitabu chake kinachoitwa The Miracle Morning: The Not-So-Obvious Secret Guaranteed to Transform Your Life: Before 8AM Hal, pamoja na mambo mengine, ametufundisha hatua tatu ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzichukua na akafanikiwa sana.

Karibu tujifunze hatua hizi tatu na jinsi ya kuzifanyia kazi kwenye maisha yetu ili tusijiweke wala kuendelea kukaa kwenye umasikini na maisha magumu.

HATUA YA KWANZA; TAMBUA ASILIMIA 95 HAWATAFANIKIWA.

Hatua ya kwanza ya kutoka kwenye umasikini na kuelekea kwenye utajiri ni kutambua kwamba asilimia95 ya watu hawatafanikiwa. Kwa maneno mengine ni kwamba utajiri siyo kwa kila mtu. Hata watu wote wangepewa fedha sawa au fursa sawa, bado mgawanyo utabaki vile vile, asilimia 5 watafanikiwa sana na asilimia 95 watakuwa na maisha magumu.

Na hili liko wazi ukiangalia kwenye jamii zetu. Mambo kama haya yapo wazi kabisa;

Ukianzia kwenye upande wa afya ya mwili, watu wengi wanakabiliwa na magonjwa sugu kama presha na kisukari, wengi hawapo kwenye afya nzuri inayowawezesha kujituma zaidi kwenye kazi zao.

Ukienda upande wa afya ya akili na roho, wengi wana msongo wa mawazo na sonona, hawawezi kuyakabili maisha yao bila ya kutumia dawa au vilevi vya kuwasahaulisha matatizo yao kwa muda.

Upande wa mahusiano nao una changamoto kubwa kwa wengi, ndoa nyingi zinavunjika na familia kusambaratika.

Kwenye fedha ndiyo mambo ni magumu zaidi. Wengi wapo kwenye madeni, kipato hakitoshelezi matumizi na hivyo wanaendelea kukopa, kitu ambacho kinawaumiza zaidi na kuwaweka kwenye umasikini mkubwa.

Ni muhimu sana utambue hali halisi na jinsi ambavyo wengi wanakwamba kwenye hali hiyo, ili wewe ukatae hali hiyo na kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

HATUA YA PILI; TAMBUA CHANZO CHA WENGI KUBAKI KWENYE UMASIKINI.

Baada ya kukubali kwamba wengi hawatafanikiwa, hata kama kila kitu kitatolewa sawa kwa wote, hatua ya pili ni kutambua chanzo cha wengi kubaki kwenye umasikini.

Siyo bahati nzuri kwamba asilimia 5 pekee ndiyo wanaofanikiwa sana na siyo bahati mbaya kwamba asilimia 95 wanabaki kwenye umasikini mkubwa.

Kila kinachotokea kwenye maisha ya mtu kinasababishwa, na ili kubadili matokeo, unapaswa kubadili kwanza kisababishi.

Ili kuondoka kwenye kundi kubwa la wasiofanikiwa na kwenda kwenye kundi dogo la wanaofanikiwa, jua sababu hizi zinazowaweka watu kwenye umasikini na ondokana nazo mara moja.

  1. Kuangalia nyuma badala ya mbele. Wale wanaoshindwa wanatumia muda wao mwingi kuangalia mambo ya nyuma kuliko pale walipo sasa na kule anakokwenda. Wamekuwa wanatumia matukio ya nyuma kama sababu ya wao kushindwa kupiga hatua zaidi. Wataeleza jinsi ambavyo walidhulumiwa, kuteswa au kunyanyaswa huko nyuma. Wataeleza jinsi ambavyo wamejaribu mambo mengi lakini wameshindwa. Kwa kuangalia zaidi nyuma kuliko mbele kunawafanya kuangalia kushindwa zaidi kuliko kufanikiwa.

HATUA YA KUCHUKUA; Acha kuangalia yale yaliyotokea nyuma na kuyatumia kama kisingizio au kikwazo kwako kupiga hatua. Chagua leo kuchukua hatua za tofauti ili kuitengeneza kesho iliyo bora kuliko leo.

  1. Kukosa kusudi la maisha. Watu wengi wanaendesha maisha yao bila ya kusudi, hawajui nini wanachotaka kwenye maisha yao na wala hawajisukumi kufanya chochote kikubwa. Kwa kukosa kusudi wanajikuta wanakimbizana na kila kitu, mwisho wa siku wanachoka na hakuna hatua wanayokuwa wamepiga.

HATUA YA KUCHUKUA; Lijue kusudi la maisha yako na ishi kusudi hilo kila siku. Kadiri kusudi linavyokuwa kubwa ndivyo linavyokusukuma kuchukua hatua zaidi na hivyo kufanikiwa.

  1. Kutenga madhara ya matukio. Watu wengi wanabaki kwenye umasikini kwa sababu hawana nidhamu. Mtu anapanga kufanya kitu fulani, lakini wakati wa kufanya unapofika hafanyi na anajipa sababu. Anachoamini ni kwamba asipofanya kitu mara moja hakuna madhara makubwa, atafanya siku nyingine. Asichojua ni kwamba kila tukio lina madhara kwenye maisha yake. Mfano mtu anapoacha kufanya kile alichopanga, hilo lina madhara makubwa kwake, anajichukulia kama mtu asiye makini na ni rahisi kurudia hilo kwenye maeneo mengine ya maisha yake.

HATUA YA KUCHUKUA; Tambua kila kinachotokea kwenye maisha yako kinaathiri maisha yako yote. Hivyo usijiruhusu kufanya kitu chochote ambacho hakiyaboreshi maisha yako.

  1. Kukosa uwajibikaji. Watu wote waliofanikiwa wanajua uwajibikaji ni muhimu sana kwenye mafanikio yao. Ndiyo maana watu hao wana mamenta, makocha na washauri mbalimbali, hawa wanahakikisha watu hao wanatekeleza kile walichopanga. Lakini wasiofanikiwa hawapendi kabisa uwajibikaji, wao wanataka kuendesha maisha kama wanavyojisikia wenyewe. Bila ya uwajibikaji, hakuna hatua mtu anaweza kupiga.

HATUA YA KUCHUKUA; Jijengee uwajibikaji kwenye maisha yako. Chochote kikubwa unachopanga kufanya, kuwa na mtu ambaye unawajibika kwake, anaweza kuwa menta wako, kocha wako na hata watu wa karibu ambao wanajali kuhusu mafanikio yako. Waombe wakusimamie kweli ili utekeleze kila unachopanga.

  1. Kuzungukwa na watu wa kawaida. Utafiti unaonesha kwamba maisha yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka au unaotumia nao muda wako mwingi. Kinachowafanya watu wengi kubaki kwenye umasikini ni kuzungukwa na watu masikini. Unapozungukwa na watu masikini, fikra zako na hata matendo yako yanakuwa kama yao na hilo linapelekea ubaki kwenye umasikini.

HATU ZA KUCHUKUA; Chagua kwa umakini sana ni watu gani unaotaka kuzungukwa nao. Chagua kuzungukwa na watu ambao wameshafanikiwa au ambao wanapambana ili kufanikiwa. Epuka sana kuzungukwa na watu walioshindwa na kukata tamaa. Na wewe utakuwa kama wao.

  1. Kutokujiendeleza binafsi. Watu wanaoshindwa huwa hawajiendelezi wao binafsi. Wakishahitimu masomo ndiyo basi, hawajisumbui tena kuendelea kujifunza hasa kusoma vitabu. Na hata wakisoma vitabu basi ni vya hadithi, na siyo vya kujifunza. Wale wanaofanikiwa wanaweka uzito mkubwa sana kwenye kujiendeleza wao binafsi. Wananunua na kusoma vitabu vinavyowafanya kuwa bora zaidi. Pia wanahudhuria mafunzo na semina mbalimbali zinazowafanya kuwa bora zaidi.

HATUA ZA KUCHUKUA; Uwekezaji wa kwanza na muhimu kufanya kwenye maisha yako ni kuwekeza ndani yako mwenyewe. Weka vipaumbele kwenye kujifunza mambo mapya na kuyafanyia kazi. Soma vitabu vya maendeleo binafsi, hudhuria mafunzo mbalimbali na kuwa na menta au kocha anayekusimamia kwa karibu.

  1. Kukosa uharaka. Watu wengi hawapigi hatua kwenye maisha yao kwa sababu hawana ile hali ya uharaka wa kuchukua hatua kwenye jambo lolote. Ni watu wa kuahirisha mambo na kusubiri mpaka dakika za mwisho ndiyo wachukue hatua. Kwa kukosa hali hii ya uharaka wengi wamekuwa wanajichelewesha wao wenyewe kufanikiwa.

HATUA ZA KUCHUKUA; Jijengee hali ya uharaka kwenye maisha yako, chochote unachopanga kufanya, anza kufanya sasa. Kinachowezekana kufanyika leo kifanyike sasa na kisisubiri kesho. Ondokana kabisa na tabia ya kuahirisha mambo na utaweza kupiga hatua kubwa.

Rafiki, epuka sababu hizi saba ambazo zimewaweka wengi kwenye umasikini mkubwa. Huwezi kuondoka kwenye umasikini huo kama utaendelea kukumbatia sababu hizo.

SOMA; Hii Ndiyo Kanuni Rahisi Itakayokuwezesha Wewe Kufikia Uhuru Wa Kifedha Kwenye Maisha Yako.

HATUA YA TATU; CHORA MSTARI.

Baada ya kuzijua sababu ambazo zimekuweka kwenye umasikini kwa muda mrefu, sasa kuna hatua ya tatu ya kuchukua, ambayo ni kuchora mstari.

Kuchora mstari maana yake ni kufanya maamuzi kwamba kuanzia sasa mambo yako yote yanabadilika. Unaachana na mambo ya nyuma na kuanza maisha mapya ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Maamuzi hayo unayafanya sasa na hatua unaanza kuzichukua sasa. Siyo baadaye, siyo kesho, siyo wiki ijayo, siyo mwezi ujao na wala siyo mwaka ujao. Ni leo, ni sasa. Kama hutachora mstari sasa hivi na kuanza kuishi maisha mapya, utaendelea kujichelewesha kufanikiwa.

Kataa kuwa wa kawaida, kataa kubaki kwenye umasikini na maisha magumu na chagua kufanikiwa na kufikia utajiri. Chagua kuziishi tabia ambazo zitayafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Usikubali kuendesha maisha yako kwa ukawaida, halafu unapofika ukingoni mwa maisha unagundua hukuishi maisha yako. Chagua leo kuyaishi maisha yako, chagua kuwa bora zaidi ya pale ulipo sasa. Yote yanawezekana na yapo ndani ya uwezo wako.

Kwenye TANO ZA JUMA hili nitakwenda kukushirikisha kwa kina uchambuzi wa kitabu hiki, ambapo Hal anatushirikisha mambo 6 ya kufanya kila siku unapoamka asubuhi ambayo yataleta miujiza mikubwa sana kwenye maisha yako. mambo hayo sita ni rahisi, hayahitaji elimu kubwa wala uwe na fedha nyingi. Lakini ukiweza kuyafanya kila siku, maisha yako hayatabaki hapo yalipo sasa. Usikose makala ya TANO ZA JUMA hili, utajifunza njia bora ya kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge