Mpendwa rafiki yangu,
Huwezi kufanya mambo makubwa sana kama hujajielewa wewe mwenyewe kiundani, watu wengi bado hawajajitambua kuwa wao ni kina nani na wamekuja kufanya nini hapa duniani.
Hakuna kazi ngumu hapa kama kuishi maisha bila kujua kile unachotaka kwenye maisha yako. Ndiyo maana kila mmoja wetu anaalikwa kufanya juhudi za kujitambua maana kujitambua ni zawadi kwako binafsi na dunia kwa ujumla.
Unapojitambua kwenye maisha yako unatakiwa kufanya vitu vya kipekee sana, kama hujitambua utawezaje kufanya vitu vya kipekee? Wewe ni mtu wa muhimu sana hapa duniani hujazaliwa kwa bahati mbaya hivyo jua kusudi lako na ishi kusudi lako.
Kila binadamu anaishi katika pande tatu za maisha , na pande hizo ni kama zifuatazo;
Upande wa kwanza ni maisha ya wazi ( public life). Haya ni maisha ya wazi dhidi ya jamii inayomzunguka mtu. Kuna maisha ambayo unaishi sasa ni ya wazi ambayo kila mtu anayaona. Kama unaigiza au unafanya kweli ni wewe mwenyewe ndiyo unajua kwa sababu kama ni maisha yako halisi basi jamii inayokuzunguka inajua.
Je hayo ndiyo maisha yako halisi ya wazi unayoishi? Jitafakari na chukua hatua kwenye kile ambacho unaona ni sahihi.
Upande wa pili ni maisha binafsi( private). Kila mmoja wetu ana maisha yake ya ndani binafsi, tukiachana na maisha yetu ya wazi lakini sehemu kubwa ya maisha yetu imelala hapa. Kila mmoja wetu kuna mambo yake binafsi anayofanya na anayopenda. Hivyo basi, mafanikio makubwa ya mtu yanakuja pale anapojielewa kwanza yeye binafsi. Anapojielewa yeye binafsi basi ataweza kufanya makubwa ambayo yatampeleka kwenye mafanikio makubwa.
Kama huna maisha binafsi, basi utakua unaishi maisha ambayo si yako, lakini hata iweje kila mtu ana maisha yake binafsi iwe unajitambua au hujitambui. Unapokuwa umekaa mwenyewe ndiyo utaweza kujijua vizuri.
Upande wa tatu ni maisha ya siri, yaani secret life; kila mmoja wetu ana maisha yake ya siri, ni rahisi kuona maisha ya wazi lakini siyo rahisi kuona maisha ya sirini mwa mtu. Siyo kila kitu kila binadamu anapaswa kuweka wazi mambo yake.
Kwa mfano, vitu kama afya, kipato na familia ni mambo ambayo yanatakiwa kuwa siri ya mtu. Siyo kila mtu anapaswa kujua undani wako ila wewe mwenyewe. siyo kila mtu anaweka wazi mambo yake.
Mambo mengine yanatakiwa yawe siri, dunia ikishakujua wewe una nini lazima itaanza kukusumbua kwa kile ulicho nacho, ukisema una fedha nyingi, itaanza kujipanga kuchukua hela zako.
Hatua ya kuchukua leo; ishi maisha yako katika pande hizi tatu, upande wa wazi yaani maisha ya wazi, maisha binafsi na maisha ya siri. Tambua hizo pande tatu na ziishi kwenye maisha yako kila siku.
Hivyo basi, hakuna mtu anayekujua wewe zaidi yaw ewe mwenyewe. wewe ndiyo injinia wa wewe mwenyewe, unajua unataka nini na mtu wa kukutafutia kile unachotaka ni wewe mwenyewe. Amua sasa kuwa vile unavyotaka kuwa kwani kila kitu kipo ndani ya uwezo wako, na ukiamua wewe hakuna atakayeweza kukusimamisha.
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com
Asante sana