#TANO ZA JUMA #38 2019; Biashara Ni Faida, Mfumo Wa Kuendesha Biashara Unaoleta Faida, Jinsi Ya Kuiona Faida Halisi Ya Biashara Yako, Njia Bora Ya Kudhibiti Matumizi Yako Na Kuongeza Faida, Punguza Wateja.

Hongera sana rafiki yangu kwa kumaliza juma namba 38 la mwaka 2019 salama.

Nina imani juma hilo limekuwa bora na la kipekee sana kwako na kwamba umeweza kujifunza na kuchukua hatua za tofauti ili kuweza kuelekea kwenye mafanikio makubwa unayofanyia kazi.

Karibu kwenye makala yetu ya TANO ZA JUMA ambapo unapata mkusanyiko wa mambo matano muhimu ya kufanyia kazi ninayokushirikisha kutoka kwenye kitabu cha juma ambacho ninakuwa nimekisoma. Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa Profit First: A Simple System To Transform Any Business From A Cash-Eating Monster To A Money-Making Machine kilichoandikwa na Mike Michalowicz.

Profit-First-Book cover

Mike anatuambia biashara nyingi zimekuwa zinaendeshwa bila ya kutengeneza faida, kitu kinachopelekea biashara hizo zife. Hivyo anatuambia njia pekee ya kuendesha biashara yenye mafanikio, ni kwa kuanza kupata faida kwanza kabla ya mengine yote. Mike anasema, faida kwenye biashara inapaswa kuanza kupatikana siku ya kwanza unapoanza biashara, na siyo kusubiri mpaka siku zijazo.

Nani asiyependa kuwa na biashara inayoingiza faida kubwa? Nani anayependa biashara yake ife kwa kukosekana kwa faida? Naamini wote tunapenda biashara zenye faida, hivyo nikukaribishe tena kwenye TANO ZA JUMA ili uweze kupata maarifa sahihi yatakayokuwezesha kuanza kutengeneza faida kwenye biashara yako mara moja, bila ya kujali hali ambayo biashara yako inapitia sasa.

#1 NENO LA JUMA; BIASHARA NI FAIDA.

Biashara nane kati ya kumi zinazoanzishwa, huwa zinakufa ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa. Namba hii ni kubwa sana na inayoumiza na kusikitisha. Sababu namba moja inayopelekea biashara zote hizo kufa ni hii; biashara nyingi hazijiendeshi kwa faida, hasa kipindi cha mwanzoni.

Kipindi cha mwanzo cha biashara huwa ni kipindi cha uwekezaji, ambapo biashara inachukua fedha na rasilimali kuliko inavyozalisha. Wengi tunapokea hilo kama ndivyo uhalisia ulivyo na hivyo hatutegemei biashara izalishe faida kwenye siku hizo za mwanzo kwenye biashara.

Cha kushangaza, huwa hatuweki muda ni lini tunataka tuanze kupata faida kwenye biashara hiyo. Hivyo biashara inaendelea kujiendesha bila faida mpaka pale inapofika hatua kwamba haiwezi kwenda tena kwa sababu mtaji umepungua sana kutokana na hasara zinazotengenezwa.

Mike Michalowicz kwenye kitabu chake cha PROFIT FIRST anatuambia kila biashara inapaswa kutengeneza faida kuanzia siku ya kwanza ya biashara hiyo. Faida haipaswi kusubiriwa mpaka siku zijazo, bali inapaswa kuanza kukusanywa sasa. Anatuambia bila ya kuwa na kipaumbele cha faida, biashara haina nafasi ya kufanikiwa.

Kwenye kitabu hicho mwandishi ametupa mfumo mzuri wa kuanza kukusanya faida yako kwenye biashara mapema. Kwa mfumo huo, ni rahisi kuiona faida, hata kama ni kidogo. Na mfumo huo unazuia tabia yako kama mfanyabiashara ya kuwa na matumizi ya hovyo na yanayoirudisha biashara nyuma.

Biashara ni faida, kama biashara haitengenezi faida hiyo siyo biashara, ni swala la muda tu, itakuwa imeshakufa. Hivyo kama upo kwenye biashara, au unapanga kuingia kwenye biashara, kipaumbele cha kwanza kwenye biashara yako ni faida, kwa sababu ni kupitia faida pekee ndiyo biashara yako inaweza kusimama.

Kama mpaka sasa kupata faida kwenye biashara yako kumekuwa ni kitu kigumu, soma uchambuzi wa kitabu cha PROFIT FIRST kwenye kipengele namba mbili hapo chini na utaondoka na maarifa sahihi ya kukuwezesha kutengeneza faida kwenye biashara yako.

#2 KITABU CHA JUMA; MFUMO WA KUENDESHA BIASHARA UNAOLETA FAIDA.

Biashara ndogo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi duniani. Hii ni kwa sababu biashara hizo ndogo zinatoa ajira kwa wale wanaozifanya na hata wengine wanaoajiriwa kwenye biashara hizo. Lakini pia biashara hizo zinatoa bidhaa na huduma ambazo watu wanazihitaji kwenye maisha yao ya kila siku.

Lakini uanzishwaji na uendeshwaji wa biashara hizi ndogo umekuwa ni changamoto kubwa kwa wengi. Wengi wanaingia kwenye biashara ndogo wakiwa hawana misingi sahihi ya kufanikiwa. Wanaona ni kitu wanachoweza kufanya na wanaingia na kufanya kwa mazoea. Hili limepelekea biashara nyingi ndogo kutokitengeneza faida na hivyo kupelekea biashara hizo kufa.

Mwandishi Mike Michalowicz kupitia kitabu chake kinachoitwa Profit First: A Simple System To Transform Any Business From A Cash-Eating Monster To A Money-Making Machine, ametushirikisha mfumo bora wa kuendesha faida ambao unakuwezesha kuiona faida halisi ya biashara yako.

Mfumo huu wa FAIDA KWANZA unakwenda kufanya kazi kulingana na asili yetu sisi binadamu badala ya kupingana nayo. Mfumo huu unakwenda kutusaidia kuondokana na udhaifu mkubwa ambao tunao inapokuja kwenye swala la fedha, ambao ni kutumia fedha kwa sababu ipo.

Kwa mfumo wa FAIDA KWANZA, kwenye kila kipato kinachoingia kwenye biashara yako, unaondoa kwanza faida na kuitunza sehemu ambapo huwezi kuitumia, kisha kulazimika kutumia kiasi cha fedha kilichobaki baada ya kuondoa faida. Kwenye uchambuzi huu wa kitabu tutajifunza kwa kina jinsi ya kufanya hivyo.

Kuna sababu mbili ambazo zimekusukuma wewe kuingia kwenye biashara, ya kwanza ni kufanya kile ambacho unapenda kufanya na ya pili ni kutengeneza kipato ambacho kitakupa uhuru. Sasa wengi wamekuwa wanajikuta kwenye mtego wa biashara zao, wanafanya wanachopenda, lakini hawaioni faida. Kwa kuwa wanapenda kile wanachofanya, wanaendelea kukifanya zaidi na zaidi na hivyo kuzidi kukosa uhuru. Mfumo wa FAIDA KWANZA unakusaidia kufanya unachopenda na kupata uhuru pia.

MOJA; BIASHARA INAVYOUGEUKA NA KUWA DUBWANA LINALOKULA FEDHA.

Wajasiriamali ni watu wanaotenda miujiza, huwa wanatengeneza kitu ambacho hakipo kabisa, na kinakuja kwenye uhalisia na kuwa msaada kwa watu. Fikiria mtu anakuja na wazo jipya la biashara, ambalo linakuwa msaada mkubwa kwa wengine, kitu ambacho hakikuwepo kabisa, lakini wao wanakileta kwenye maisha, huo ni muujiza mkubwa.

Lakini sasa kuna wakati muujiza huo unazalisha dubwana ambalo linakuwa hatari kwa maisha ya mjasiriamali mwenyewe. Fikiria mtu anaanzisha biashara yake, ambayo inafanya mauzo makubwa, lakini haitengenezi faida. Hapo mtu atajituma sana, ataweka juhudi sana, lakini bado biashara inashindwa kutengeneza faida. Biashara hiyo badala ya kutengeneza faida, inakuwa inakula fedha na hivyo kuleta hasara, ambayo inapunguza mtaji na kupelekea biashara kufa.

Matatizo ya kifedha kwenye biashara huwa yanasababishwa na vitu viwili;

Kitu cha kwanza ni pale mauzo yanaposhuka, wateja wanapopungua au kupunguza kununua. Hapa biashara inakosa kipato na hivyo kushindwa kujiendesha vizuri.

Kitu cha pili ni mauzo kukua sana na kwa haraka. Unaweza kuona hiki ni kitu kizuri, lakini ukweli ni kwamba hicho huwa ni kitu hatari. Biashara inapofanya mauzo makubwa na kwa haraka, inapeleka mfanyabiashara kujisahau na kuona biashara imefika ngazi ya juu. Hapo matumizi yanakwenda juu, na pale msimu huo wa mauzo ya juu unapopita, biashara inajikuta kwenye matatizo makuba.

Kitu kingine kinachofanya biashara ziwe dubwana linalokula fedha badala ya kuzalisha faida ni ndoto za wafanyabiashara kutaka biashara zao ziwe kubwa zaidi. Watu wengi huingia kwenye biashara wakiwa na maono makubwa. Hivyo hujishawishi kwamba ili wafikie maono hayo, kipindi cha mwanzo hawapaswi kutengeneza faida yoyote kwenye biashara zao. Hili linawafanya wateseke sana na kupelekea biashara kufa.

Suluhisho la kuondokana na matatizo haya ya biashara kuwa dubwana linalokula fedha ni kutumia mfumo wa FAIDA KWANZA. Na hii inaanza kwa kuelewa kwamba faida siyo tukio la kusubiria kwa siku moja, bali faida ni mchakato wa kila siku. Kwa kila mauzo unayofanya kwenye biashara yako, unapaswa kutenga sehemu ya mauzo hayo na kuifanya kuwa faida yako. Utakwenda kujifunza jinsi ya kutumia mfumo huu wa FAIDA KWANZA KWENYE BIASHARA YAKO.

MBILI; MSINGI MKUU WA MFUMO WA FAIDA KWANZA.

Mfumo wa FAIDA kwanza umejengwa kwenye msingi mkuu ambao unagusa tabia zetu sisi wanadamu. Msingi huu umejenga na vitu vinne.

Kitu cha kwanza ni sheria ya Parkinson ambayo inasema huwa tunatumia kitu kadiri kinavyopatikana. Mfano ukiwa na elfu 10 kwa ajili ya kula utakula elfu kumi, na ukiwa na elfu 5 kwa ajili ya kula utakula chakula cha bei hiyo. Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kutumia kitu kadiri kinavyopatikana, kama kinapatikana kwa wingi tunatumia kwa wingi, kama kinapatikana kwa uchache tunatumia kwa uchache.

Kutumia sheria hii kwenye biashara yako, unapaswa kuondoa sehemu ya mapato yako na kuyaficha ili usiweze kuyatumia. Tutajifunza jinsi ya kufanya hivyo.

Kitu cha pili ni vipaumbele. Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kuweka mkazo kwenye kile kinachotangulia kuliko kinachofuata. Kile cha kwanza tunachokisikia, tunakipa uzito na kukifikiria kwa muda mwingi kuliko kinachofuata.

Kwenye biashara, kanuni kuu ambayo imekuwa inatumika kupaya faida ni MAUZO – MATUMIZI = FAIDA. Hivyo huwa tunafikiria mauzo na kisha matumizi, na faida tunaifikiria kwa uchache sana. Ndiyo maana matumizi huwa hayana ukomo. Kwa kutumia msingi huu wa vipaumbele, tunahitaji kuwa na njia ya kuifikiria faida kwanza kabla ya matumizi. Na hapo ndipo tunapohitaji kuibadili kanuni hiyo, na kuwa MAUZO – FAIDA = MATUMIZI. Hivyo unapofanya mauzo, unaondoa kwanza faida na kuiweka pembeni, halafu kiasi kinachobaki ndiyo unakitumia. Hapo pia unakuwa umejiweka ukomo kama tulivyojifunza kwenye sheria ya Parkinson.

Kitu cha tatu ni kuondoa tamaa. Kitu kinapokuwa karibu, huwa tunaingiwa tamaa ya kukitumia. Hivyo tunapaswa kujijengea njia ya kuishinda tamaa yetu isiwe kikwazo kwetu. Na njia rahisi ya kuishinda tamaa ni kukiondoa kitu mbele yako. unapokiweka kitu mbali, ambapo hukioni mara kwa mara, tamaa haiwezi kukusumbua. Lakini kama kila wakati unakiona kitu, tamaa yako haiwezi kushuka.

Kwenye biashara yako, akaunti yako ya faida unapaswa kuifungua kwenye benki tofauti na kuweka masharti kwamba huwezi kutoa fedha kwenye akaunti hiyo. Hii itakusaidia kuishinda tamaa ya kutaka kutoa fedha ya faida na kuiweka kwenye matumizi.

Kitu cha nne ni kutengeneza msimamo na tabia. Kufanya kitu mara ya kwanza huwa ni ngumu, lakini tukishatengeneza tabia, huwa inakuwa rahisi kuendelea kufanya. Hivyo unapaswa kutengeneza msimamo wa jinsi unavyofanya mambo kwenye biashara yako ili iwe kitu cha kawaida kwako.

Kwenye biashara yako na mfumo wa FAIDA KWANZA, unatenga siku ambazo unapitia mapato yako na kugawa fedha hizo kwenye mafungu mbalimbali. Kwa kutengeneza utaratibu huu, inakuwa rahisi kwako kuufuata.

TATU; AKAUNTI TANO ZA BENKI UNAZOPASWA KUWA NAZO KWENYE MFUMO WA FAIDA KWANZA.

Umeshaelewa msingi mkuu wa mfumo wa FAIDA KWANZA, ambapo ni kutenga faida kabla ya matumizi na kuiweka sehemu ambapo huwezi kuitumia. Ili kufanikisha hilo, unapaswa kuwa na aina tano za akaunti unazopaswa kuwa nazo.

Akaunti ya kwanza ni ya mapato, hii ni akaunti ambayo inapokea mapato yote ya biashara. Akaunti yako ya biashara uliyonayo sasa unaweza kuifanya kuwa ndiyo akaunti ya mapato, kwa sababu tayari umekuwa unaitumia hivyo. Akaunti hii kazi yake ni kukusanya mapato, kama ambavyo bwawa linakusanya maji.

Akaunti ya pili ni faida, hapa sasa ndipo unapoweka ile faida inayotoka kwenye biashara yako. Baada ya fedha kuingia kwenye akaunti ya mapato, faida inaondolewa na kuwekwa kwenye akaunti ya faida. Hii ndiyo hatua ya kwanza na muhimu. Utakuwa na viwango vya faida kulingana na biashara unayofanya, lakini pa kuanzia ni kuweka asilimia 1 ya kila mapato yanayoingia kwenye biashara yako, kama bado hujajua kiwango chako cha faida.

Akaunti ya tatu ni faida ya wamiliki. Hii ni akaunti ambayo inahifadhi fedha ambazo ni faida au fidia ya wamiliki wa biashara. Hii ni tofauti kabisa na akaunti ya faida. Hii inaweka ile sehemu ya faida ambayo inaenda kwa wamiliki wa biashara hiyo. Hapa ni sawa na kusema ni gawio kwa wamiliki wa biashara.

Akaunti ya nne ni kodi. Biashara inapaswa kulipa kodi, ambayo inakokotolewa kulingana na mauzo na faida ambayo biashara inapata. Sasa wafanyabiashara wengi wamekuwa wanajisahau, inapofika wakati wa kulipa kodi wanakuwa hawana fedha za kufanya hivyo. Kwenye mfumo wa FAIDA KWANZA unapaswa kuwa na akaunti maalumu ya kuweka fedha kwa ajili ya kodi. Na kwenye kila mauzo, unakata kiwango cha kodi na kuweka kwenye akaunti hiyo.

Akaunti ya tano ni ya gharama za uendeshaji wa biashara. Hii ni akaunti ambayo unahifadhi fedha kwa ajili ya kuendesha biashara, na fedha zinapaswa kutoka kwenye akaunti hiyo tu. Akaunti hii ndiyo inakulazimisha uwe na matumizi mazuri ya fedha zako, kwa sababu zikishaisha hakuna nyingine.

Akaunti mbili za kuondoa tamaa. Kama tulivyojifunza, kikwazo kikubwa kwako ni tamaa pale unapoziona fedha kwenye akaunti yako ya faida huku ukiwa huna fedha za kuendesha biashara, utashawishika kuzichukua. Cha kufanya hapa, unapaswa kufungua akaunti nyingine mbili kwenye benki tofauti na unayotumia sasa. Akaunti hizo ni ya FAIDA na ya KODI. Hizi ni akaunti mbili ambazo hupaswi kuzigusa kwa namna yoyote ile, hata kama biashara ina changamoto kiasi gani. Hivyo unazifungua kwenye benki ya tofauti na kwa masharti kwamba huwezi kutoa fedha hivyo kwenye akaunti hizo. Hivyo ukishagawa mapato yako na kupeleka kwenye akaunti zote tano kwenye benki yako ya kwanza, unahamisha zile zilizopo kwenye akaunti za faida na kodi kwenye benki yako ya kwanza na kupeleka kwenye benki ya pili, ili kuzuia tamaa isikuingie na kuzitumia.

Usitishwe na wingi huu wa akaunti, benki nyingi zipo tayari kukufungulia akaunti hizi za ziada bila ya kuwepo kwa gharama za ziada. Na pia benki nyingi zipo tayari kukusaidia kuhamisha fedha kwenye akaunti zako au unaweza kufanya mwenyewe kupitia mtandao wa intaneti ambapo kwa sasa benki nyingi zina huduma hiyo. Siyo ngumu kufanya, inawezekana kabisa.

NNE; TATHMINI AFYA YA BIASHARA YAKO.

Kabla ya kuingia rasmi kwenye mfumo wa FAIDA KWANZA, unahitaji kufanya tathmini ya afya ya biashara yako. Kujua kwa sasa biashara yako iko kwenye hali gani, ili unapokwenda kuchukua hatua, uweze kuchukua hatua ambazo ni sahihi.

Katika kufanya tathmini ya biashara yako, angalia maeneo matano uliyofungulia akaunti, tathmini kwa hatua hizi tatu.

Hatua ya kwanza ni kuangalia kile kinachofanyika kwa sasa. Angalia ni kiasi gani cha mapato unaingiza, kiasi gani cha faida unaweka, kiasi gani kinakuwa fidia ya wamiliki, kiasi cha kodi na gharama za kuendesha biashara. Hapa unaipata picha ya biashara yako inavyokwenda sasa.

Hatua ya pili ni kuweka viwango (kwa asilimia) unavyotaka kufikisha kwenye kila eneo. Ni kiasi gani cha mapato unahitaji, asilimia ngapi iwe faida, fidia kwa wamiliki na kodi, na kiasi gani kiende kwenye gharama za uendeshaji. Hapa unaangalia kule unakotaka kufika ili biashara yako iweze kujiendesha vizuri na kwa faida.

Hatua ya tatu ni kuangalia tofauti ya uhalisia na mipango yako na kisha kuchukua hatua sahihi. Utagundua vitu viwili hapa, kuna viwango utapaswa kupunguza ambavyo umekuwa unaweka juu sana, mfano gharama za matumizi na fidia ya wamiliki, hapa wengi huweka juu. Kuna viwango ambavyo utapaswa kuviongeza kwa sababu vipo chini. Na mara nyingi hii huwa ni kwenye faida na kodi, ni maeneo ambayo wafanyabiashara wengi huyasahau.

Unapofanya tathmini ya biashara yako utagundua kwamba biashara yako ipo kwenye hali mbaya kuliko ulivyokuwa unafikiri. Inaweza kuwa ndiyo mara yako ya kwanza kujua kwamba biashara yako haitengenezi faida. Hali hii isikuangushe, badala yake inapaswa kukufanya upate sababu ya kuchukua hatua sahihi ili biashara yako iweze kukua.

TANO; PANGA ASILIMIA SAHIHI ZA KUANZIA.

Kwenye kila akaunti ambayo umeiweka kwenye biashara yako, unapaswa kuwa na asilimia sahihi ya kiwango cha fedha unachoweka huko. Unaweza kuanzia kwa viwango vya chini na kwenda ukiongeza kadiri biashara yako inavyofanya vizuri. Kwa sababu mwanzoni biashara yako inakuwa kwenye hali mbaya kiasi kwamba kuchagua kuweka asilimia kubwa ya faida kutafanya biashara ishindwe kujiendesha.

Anza kidogo na kua kadiri biashara inavyoendelea kuimarika. Muhimu ni kuwa na biashara yenye afya na inayojiendesha kwa faida, kitu ambacho kinawezekana ukifanyia kazi mfumo wa FAIDA KWANZA VIZURI.

SITA; KUWEKA MPANGO WA FAIDA KWANZA KWENYE MATENDO.

Mpaka sasa umekuwa unaweka mipango mbalimbali pamoja na kufungua akaunti tano muhimu kwa ajili ya kugawa mapato ya biashara yako. Sasa unahitaji kuweka mipango hiyo kwenye matendo ili biashara yako iweze kunufaika.

Ili kuweza kupata kiasi cha kutosha cha fedha kuweza kugawa kwenye akaunti zako tano, unahitaji kuongeza kipato unachoingiza sasa kwenye biashara yako. Zipo njia mbili za kufanikisha hili, njia ya kwanza ni kuongeza mauzo na njia ua pili ni kupunguza gharama za uendeshaji.

Kuongeza faida ndiyo njia ya uhakika na yenye matokeo mazuri kwa biashara yako, lakini matokeo yake hutaanza kuyaona haraka. Inachukua muda tangu unapoanza kufanyia kazi mpango wa kuongeza mauzo mpaka uanze kuona matokeo yake. Hivyo kuwa na mpango wa kuongeza mauzo, lakini jua matokeo mazuri utayaona baadaye.

Kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara ni njia ambayo matokeo yake unaweza kuyaona mara moja. Ni rahisi kupunguza asilimia 10 mpaka 20 ya gharama zako za biashara mara moja na kuona matokeo yake. Na hapa unapaswa kuangalia chochote kinachotoa fedha kwenye biashara yako na kujiuliza kama ni muhimu sana, kama siyo muhimu unaachana nacho mara moja.

Kupunguza gharama za biashara kwa kuacha vitu visivyo na umuhimu huwa kunaumiza, lakini huna budi kufanya kwa sababu unataka biashara yako ijiendeshe kwa faida.

Hapa kuna njia tatu za kupunguza gharama za biashara yako kwa angalau asilimia kumi;

Njia ya kwanza ni kuondoa gharama zozote zinazojirudia rudia ambazo siyo muhimu. Mfano malipo ya huduma ambazo hamzitumii sana lakini zinalipiwa kila mwezi mnaweza kuyaondoa.

Njia ya pili ni kutengeneza makubaliano mapya kwenye zile gharama ambazo huwezi kuziondoa. Hapa omba kupunguziwa kiasi unacholipa au kiasi cha malipo unachopaswa kufanya kwa kujirudia. Ukiangalia kila gharama unayoingia, kuna namna inavyoweza kupungua kama ukiongea na wahusika.

Njia ya tatu ni kupunguza wafanyakazi wasiokuwa na tija kwenye biashara. Mara nyingi wafanyabiashara hujikuta wameajiri wafanyakazi wengi kuliko uwezo wa biashara zao kulipa. Lakini kuwaondoa wafanyakazi hao inakuwa vigumu, unapaswa kufanya tathmini ya wafanyakazi wote ulionao na kuona ni wapi wanaweza kupunguzwa bila kuathiri uzalishaji na ufanisi wa biashara.

HATUA TANO ZA KUWEKA MPANGO WA FAIDA KWANZA KWENYE MATENDO.

Hatua ya kwanza; mapato yako yote yaingie kwenye akaunti ya mapato.

Hatua ya pili; kila tarehe 10 na 25 ya kila mwezi, hamisha fedha yote iliyopo kwenye akaunti ya mapato kwenye akaunti nyingine kulingana na viwango ulivyojiwekea.

Hatua ya tatu; hamisha fedha iliyopo kwenye akaunti ya FAIDA na KODI kutoka benki yako mama na kwenda kwenye akaunti za benki ya tofauti.

Hatua ya nne; kwenye akaunti yako ya fidia kwa wamiliki wa biashara, ondoa kile kiwango ulichojiweka kama cha mshahara pekee. Kiasi kingine kiache kwenye akaunti hiyo. Yaani usitumie fedha yote kwa sababu ipo, tumia kama ulivyojipangia mshahara.

Hatua ya tano; kiasi unachoweka kwenye akaunti ya gharama za kuendesha biashara ndiyo unapaswa kukitumia kwa gharama hizo. Weka vipaumbele ni gharama zipi utazingatia na zile ambazo siyo muhimu achana nazo. Iwapo fedha ulizonazo kwenye akaunti ya gharama hazitoshi kulipa bili mbalimbali za biashara, basi unapaswa kujua una gharama kubwa kuliko biashara yako inavyoweza kumudu. Hivyo badala ya kupunguza fedha kwenye akaunti nyingine, kazana kupunguza gharama za kuendesha biashara.

SABA; VUNJA MADENI YAKO.

Baada ya kuweka mfumo wa faida kwanza kwenye matendo, sasa unapaswa kurudi kwenye matatizo uliyotengeneza kwenye biashara yako siku za nyuma. Na tatizo kubwa ni madeni ambayo unakuwa umeyatengeneza. Huenda huko nyuma ulikuwa unakopa ili kupata mtaji wa kuendesha biashara yako.

Hatua ya kwanza kuchukua baada ya kuanza kufanyia kazi mpango wa FAIDA KWANZA ni kuacha kukopa, kuanzia sasa usiendelee kutengeneza madeni kwenye biashara yako. Umeshajifunza kutenga faida kwanza na kupunguza gharama za kuendesha biashara, huhitaji tena kukopa ili kulipa bili za biashara au mishahara ya wafanyakazi. Kama utakuja kukopa ni kwa ajili ya ukuaji wa biashara, lakini siyo kwa ajili ya matumizi.

Hatua ya pili ni kuanza kulipa deni lako la nyuma. Na unafanya hivi kwa kutumia fedha ambayo umeitenga kwenye akaunti yako ya faida. Unachofanya ni kuchukua asilimia 99 ya fedha unayoweka kwenye akaunti ya faida na kulipa deni, na asilimia moja ndiyo inabaki kama faida. Asilimia hiyo moja unaweza kuitumia utakavyo. Hivyo hapa unanufaika mara mbili, deni linalipwa na wewe unanufaika. Wengi hufanya makosa ya kulipa deni kwanza na kusahau faida, kitu ambacho kinawafanya waishie njiani.

NANE; TAFUTA FEDHA NDANI YA BIASHARA YAKO.

Ni bora kuchimba kisima kuliko kutengeneza mvua. Wafanyabiashara wengi wanaokuwa wanataka kupata fedha zaidi, huanza kuangalia nje ya biashara kabla hawajaangalia ndani ya biashara hiyo. Ndani ya kila biashara kuna fursa nyingi sana za kutengeneza kipato.

Wafanyabiashara wengi hukimbilia kuangalia namna gani wanaweza kuongea mauzo zaidi kwenye biashara zao, kabla hawajaangalia ni namna gani biashara zao zinapoteza fedha. Hii ni sawa na kutafuta mtu wa kutengeneza mvua, wakati huna sehemu za kukinga maji hayo ya mvua.

Hatua ya kwanza kuchukua ni kutengeneza ufanisi kwenye biashara yako. Angalia ni wapi biashara yako inapoteza fedha sasa, au ingeweza kutengeneza fedha zaidi bila ya kuingia gharama za ziada. Na uzuri ni kwamba, kila biashara kuna mahali inaweza kuboreshwa zaidi.

Kuendesha biashara yako kwa ufanisi kunakuwezesha kutengeneza kiwango kizuri cha faida bila ya kuingia gharama za ziada kwenye kuongeza mauzo yako.

Moja ya njia nzuri ya kuongeza ufanisi ni kuacha kuwahudumia wateja wasumbufu na kuchagua kuwahudumia wateja ambao ni bora. Ukitafuta wateja wengi wa aina hiyo biashara yako itatengeneza faida nzuri bila ya kuingia gharama za ziada.

Njia nyingine ni kupunguza bidhaa au huduma unazotoa. Angalia ni zipi kati ya huduma au bidhaa unazotoa zenye faida nzuri na zinazotoka zaidi, kisha weka nguvu zako zote kwenye bidhaa au huduma hizo chache, utaweza kutengeneza faida zaidi.

Angalia kila eneo la biashara yako na jiulize swali hili, nawezaje kupata matokeo mara mbili kwa kutumia nusu ya muda? Ndiyo, unataka upate mara mbili ya matokeo unayopata sasa, lakini kwa kutumia nusu ya muda unaotumia. Kwa kujiuliza swali hili na kupata majibu utakayoyafanyia kazi, utaweza kuongeza ufanisi kwenye biashara yako na kuongeza faida bila ya gharama za ziada.

TISA; MBINU ZA JUU ZA MFUMO WA FAIDA KWANZA.

Mpaka sasa umeshajifunza na kuuelewa vizuri mfumo wa FAIDA KWANZA. Lakini huenda una maswali au wasiwasi juu ya mambo fulani fulani. Labda kuna malipo ya ziada ambayo unafanya kwenye biashara yako na hivyo akaunti tano hazikutoshi. Unapojikuta kwenye hali kama hii, msingi mkuu ni mmoja, ongeza akaunti.

Kama kuna kitu unataka kufanya na unahitaji kuwa na fedha kwa ajili ya kitu hicho, fungua akaunti ya tofauti na weka fedha hizo huko.

Zifuatazo ni baadhi ya akaunti za ziada unazoweza kufungua kulingana na matakwa ya biashara yako.

 1. Akaunti ya dharura.
 2. Akaunti ya manunuzi ya bidhaa.
 3. Akaunti ya kununua mali ghafi.
 4. Akaunti ya kuhifadhi fedha kwa muda.
 5. Akaunti ya mishahara ya wafanyakazi.
 6. Akaunti ya kununua vifaa au mali zinazotumika kwenye biashara, kama mashine n.k
 7. Akaunti ya matumizi madogo madogo.

Siyo lazima uwe na akaunti zote hizi, zile tano za kwanza ndiyo za msingi, nyingine ongeza kulingana na mahitaji ya biashara yako.

KUMI; MAISHA YA FAIDA KWANZA.

Mfumo wa faida kwanza haukusaidii tu kwenye biashara, bali unaweza kuutumia kwenye maisha yako ya kawaida na ukakupa manufaa makubwa.

Kuendesha maisha yako ni sawa na kuendesha biashara. Unaingiza kipato na unakitumia. Na pia una maono makubwa ya maisha yako kama ilivyo kwenye maono ya biashara.

Hivyo tumia msingi huu wa faida kwanza kwenye maisha yako. Kwa kila kipato chako, tengeneza mafungu mbalimbali ambapo utakigawa kabla hujatumia. Kuwa na fungu la kujilipa wewe mwenyewe kwanza kabla hujatumia. Kuwa na fungu la dharura ambapo itakusaidia pale unapokutana na dharura. Kuwa na fungu la starehe na mapumziko na kuwa na fungu la maendeleo mengine na maendeleo binafsi.

Unapopata kipato chako, kigawe kulingana na asilimia ulizojiwekea kwenye kila fungu. Mfano unayojilipa mwenyewe inaweza kuwa silimia 10 ya kipato, dharura asilimia kumi, starehe asilimia 10 na kuendelea.

LENGO KUU LA FAIDA KWANZA.

Lengo kuu la mfumo wa faida kwanza kwenye biashara na hata kwenye maisha ni kufikia uhuru wa kifedha. Uhuru wa kifedha ni pale unapokuwa na kipato cha kutosha kuyaendesha maisha yako jinsi utakavyo hata kama hufanyi kazi kabisa. Hapa unakuwa na akiba na uwekezaji ambao unakuwezesha kuyaendesha maisha yako vizuri hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.

Lakini ili uweze kufikia lengo hili, lazima uweke kazi sana, lazima uchague miaka michache ya kuishi kwa mateso ili kuweza kujenga misingi sahihi. Huwezi kufikia uhuru wa kifedha kama unaishi kama ambavyo kila mtu anaishi. Lazima uchague maisha ya tofauti na hayo ndiyo yatakuwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

Usimuonee mtu yeyote aibu pale unapochagua kuishi maisha yako, tambua kwamba wengi wanaojali kuhusu wewe hawatakushangaa kwa maisha unayoishi na wale wanaokushangaa hawatafanya hivyo kwa muda mrefu.

Wakati unafanyia kazi mpango wa FAIDA KWANZA, ambapo kipaumbele chako kinakuwa kwenye kuongeza kipato na kupunguza matumizi, zingatia mambo haya matano;

 1. Kabla hujanunua kitu, jiulize kwanza kama huwezi kukipata kwa bure.
 2. Kama huwezi kupata bure na inakubidi ununue, basi usinunue kitu kipya kama unaweza kununua mtumba na kikakamilisha jukumu lako.
 3. Pale unaponunua, omba punguzo la bei, kumbuka kila kitu kinaweza kupunguzwa.
 4. Usilipe gharama kamili mara moja, omba kulipa kidogo kidogo kwa awamu.
 5. Kabla hujafanya manunuzi makubwa, andika kwanza vitu kumi mbadala wa manunuzi hayo na fikiria kila kimoja kwa kina. Kwa njia hii utaacha kununua vitu kwa hisia.

Maisha ya FAIDA KWANZA ni maisha ua ubahili, hasa mwanzoni, ila ni ubahili ambao unalipa.

Ukishafikia lengo lako la FAIDA KWANZA ambalo ni UHURU WA KIFEDHA, usisahau kusherekea lakini pia usijisahau na kurudi kwenye tabia za nyuma.

Mwisho kabisa, wafundishe watoto wako mfumo huu wa faida kwanza. Kwa kila fedha unayowapa au wanayoipata kwa njia nyingine, wafundishe kugawa kwenye mafungu. Kadiri wanavyojifunza hili wakiwa wadogo, ndivyo inavyokuwa tabia kwao na kunufaika nayo baadaye.

Hayo ndiyo mambo muhimu ya kujifunza ili kuweza kutengeneza mfumo wa FAIDA KWANZA KWENYE biashara yako na maisha kwa ujumla. Yafanyie kazi ili uweze kunufaika sana.

Usikose #MAKINIKIA ya juma hili ambapo tutajifunza makosa nane ambayo wengi huwa wanayafanya wanapotumia mfumo wa FAIDA KWANZA na kupelekea kutokupata matokeo mazuri. Na pia utaondoka na mpango kamili wa kutekeleza mfumo wa FAIDA KWANZA kwenye biashara yako, ukiwa na hatua za kuchukua kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka. Utaratibu wa kupata #MAKINIKIA upo mwisho wa makala hii.

#3 MAKALA YA JUMA; JINSI YA KUIONA FAIDA HALISI YA BIASHARA YAKO.

Biashara nyingi zimekuwa zinatengeneza faida kwenye makaratasi, lakini ukirudi kwenye uhalisia, mfanyabiashara hawezi kuiona faida hiyo. Yaani wahasibu wanapofanya mahesabu ya biashara kwa kipindi cha nyuma, hesabu zao zinaweza kuwaonesha kwamba biashara imetengeneza faida ya kiasi kadhaa. Lakini ukiwaambia wafanyabiashara wakuoneshe faida ambazo hesabu hizo za biashara zimeionesha, hawajui iko wapi, na hata hao wenyewe wanashangaa.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya faida inayoonekana kwenye makaratasi na faida halisi ambayo mtu anaweza kuiona kwenye biashara yake. Na hii inatokana na hesabu isiyo sahihi ya uhasibu ambayo imekuwa inatumika kwenye biashara. Kama unataka kuiona faida halisi ya biashara yako, basi unapaswa kuanza kutumia kanuni mpya ya uhasibu, ambayo inaweka kipaumbele kwenye faida.

Kwenye makala ya juma la 38, tumepata nafasi ya kujifunza jinsi unavyoweza kuiona faida halisi kutoka kwenye biashara yako. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma sasa hivi kwa kufungua maandishi haya; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuiona Faida Halisi Kutoka Kwenye Biashara Yako.

Endelea kutembelea mitandao ya AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku ili upate mafunzo na hamasa zitakazokuwezesha kuchukua hatua kubwa na kufanikiwa sana.

#4 TUONGEE PESA; NJIA BORA YA KUDHIBITI MATUMIZI YAKO.

Matumizi yetu ya fedha, hayana tofauti na matumizi ya dawa ya meno. Tunapokuwa na dawa ya meno kwa wingi, wakati chupa ya dawa hiyo imejaa, huwa tunaiweka nyingi kwenye mswaki. Na kama kwa bahati mbaya wakati tunaiweka imedondoka chini, huwa tunaweka nyingine, si imejaa kwenye kichupa chake?

Pale ambapo dawa hiyo imeisha kabisa kwenye kichupa chake, huwa tuna ubunifu wa kipekee mno kuhakikisha tunapata dawa. Huwa tunaminya kichupa hicho kwa ustadi, kuanzia chini mpaka juu na kuhakikisha tunapata angalau dawa kidogo ya kusafisha kinywa. Wengine huenda mbali zaidi na kupasua kabisa kichupa cha dawa ya meno ili kukomboleza ndani ya kichupa hicho.

Hiyo ndiyo tabia tuliyonayo kwenye fedha pia.

Tunapokuwa na fedha, matumizi huwa hayakosekani, chochote kinachopita mbele yetu na tukakipenda, hatuchelewi kukinunua, kwa sababu fedha ipo. Mtu akilia shida kidogo hatufikirii mara mbili, tunatoa fedha na kumpa. Unanunua vitu ambavyo huna uhitaji nao mkubwa, unawapa watu vitu au fedha ambazo hazina ulazima sana.

Pale unapokuwa huna fedha, ndipo akili yako inafanya kazi vizuri. Unahakikisha fedha kidogo uliyonayo inatosha kwa yale matumizi muhimu na ya msingi pekee. Chochote ambacho siyo muhimu sana kinawekwa pembeni. Chochote kinachoweza kusubiri basi kinasubiri. Mtu anapolia shida, unaangalia kwanza je ni shida yenye uharaka, kama siyo basi inashukuru. Na hakuna wa kukulaumu, si fedha huna?

Unapokuwa huna fedha unazijua njia za mkato kwenye mambo mengi, unajua jinsi ya kupunguza gharama kwenye kila unachofanya na unavijua kwa hakika vipaumbele vyako na kufuata hivyo tu. Ukiwa huna fedha hakuna mtu anayeweza kukuyumbisha, akili yako inafanya kazi sawasawa.

Kwa kuangalia tabia zetu hizi wakati tuna fedha na wakati hatuna fedha, tunajifunza msingi mmoja muhimu sana kwetu kufanyia kazi ili kuweza kudhibiti matumizi yetu na hivyo kuweka akiba nzuri na kuwekeza pia.

Msingi huo ni kujilazimisha kuishiwa muda wote, kutokujiruhusu kuwa na fedha ya akiba kwa wakati wowote ule. Hivyo unapopokea kipato chako, sehemu ya kipato hicho iweke mbali kabisa, mahali ambapo huwezi kuifikia kwa namna yoyote ile. Halafu kazana kuendesha maisha yako kwa kiasi kilichobaki.

Kwa kufikiria unaweza kuona hilo ni gumu sana, lakini nikuhakikishie umekua unafanya hivyo mara nyingi tu unapokuwa huna fedha na hujafa, na kama hujafa, basi umezidi kua imara.

Hivyo kuanzia sasa, unapopokea kipato chochote kile, sehemu ya kipato hicho iweke pembeni na isahau kabisa. Tumia ile sehemu iliyobaki na kama haitoshelezi basi umiza kichwa chako kujua unawezaje kuifanya itosheleze. Ukiwa kwenye hali hiyo, akili yako itafanya kazi kweli.

Anza kujilazimisha kuishiwa na utaendesha maisha yako vizuri kwa kiwango kidogo cha fedha, huku ukiweza kujiwekea akiba na kuwekeza fedha yako kwa manufaa zaidi ya baadaye.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KUONGEZA FAIDA, PUNGUZA WATEJA.

“All revenue is not the same. If you remove your worst, unprofitable clients and the now-unnecessary costs associated with them, you will see a jump in profitability and a reduction in stress, often within a few weeks. Equally important, you will have more time to pursue and clone your best clients.” ― Mike Michalowicz

Mapato yote kwenye biashara hayafanani. Kuna mapato mazuri na mapato mabaya. Mapato mazuri yanatokana na wateja wazuri ambao wananunua kwa bei iliyowekwa na hivyo kuiwezesha biashara kutengeneza faida. Mapato mabaya yanatokana na wateja wasio wazuri, ambao wanataka punguzo kwenye kila unachowauzia.

Sasa kama unakimbilia kuuza tu, unaweza kuona kupunguza haina shida, si unauza? Lakini ukweli ni kwamba shida ipo, kwa sababu unauza kwa hasara na hiyo inaigharimu biashara yako.

Kama unataka kuongeza mapato na faida kwenye biashara yako, basi unapaswa kuwapunguza wateja wako. Na wateja unaopaswa kuwapunguza ni wale ambao hawaleti faida, wale ambao wanataka punguzo kwenye kila kitu na hawalipi kwa wakati.

Kwa kupunguza wateja hawa siyo tu unaokoa hasara inayotokana nao, bali pia unapunguza msongo unaotokana na kuwahudumia wateja hao, maana wengi huwa ni wasumbufu sana, kuanzia kuwauzia mpaka kuwafuatilia walipe.

Ukipunguza wateja hao wasumbufu, unatoa nafasi ya kuwahudumia vizuri wale wateja ambao ni bora kwako na hivyo mapato na faida vinaongezeka mara dufu.

Kwenye biashara yako, usikimbilie tu kuuza, bali kazana kufanya mauzo yenye faida kwa wateja ambao ni wazuri. Unaweza kuuza kwa wachache ambao ni bora ukapata faida kubwa kuliko kuuza kwa wengi ambao siyo bora.

Hizi ndizo TANO ZA JUMA la 38 la mwaka 2019 ambazo zimejikita kwenye kuendesha biashara inayozalisha faida tangu siku ya kwanza. Fanyia kazi haya uliyojifunza na kwa hakika biashara yako itaweza kupiga hatua sana.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma la 38 tunakwenda kujifunza makosa nane ambayo wengi huwa wanayafanya wanapotumia mfumo wa FAIDA KWANZA na kupelekea kutokupata matokeo mazuri. Na pia utaondoka na mpango kamili wa kutekeleza mfumo wa FAIDA KWANZA kwenye biashara yako, ukiwa na hatua za kuchukua kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka. Hatua hizo zinakuwezesha kufanikiwa zaidi kwenye biashara yako.

Kupata #MAKINIKIA haya, hakikisha umejiunga na channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Kama bado hujajiunga maelezo kuhusu channel hiyo yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu