Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kichekesho kinachosema kila biashara huwa inalipa ukiwa unasimuliwa.
Lakini unapoingia ndiyo unakutana na uhalisia ambao hukusimuliwa.
Kichekesho hiki kina ukweli nusu na ukweli wenyewe ni kila biashara huwa inalipa, ila inategemea na namna ambavyo mtu anaifanya.
Watu wengi biashara haziwalipi kwa sababu wanazifanya vibaya.
Wanaingia kwenye biashara kwa mazoea au kuiga huku wakiwa hawana elimu ya msingi ya biashara.
Kwa kukosa elimu hiyo, wanafanya makosa ambayo yanaigharimu biashara na mwisho biashara inaanguka vibaya.
Hapo ndipo wanapolaumu kwamba walidanganywa kuhusu biashara hizo.

Moja ya kosa kubwa ambalo wengi huwa wanafanya kwenye biashara ni kushindwa kutofautisha mtaji wa biashara na faida inayopatikana.
Kwa kukosa elimu sahihi ya biashara, mtu hudhani kila pesa iliyopo kwenye biashara ni yake. Hivyo anaokuwa na mahitaji anajichukulia tu fedha vile anavyojisikia.
Hilo linapelekea biashara kufa na mtu kuanza kulaumu wengine au hali ya uchumi, wakati ni yeye mwenyewe ameiua biashara yake.
Kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto inayokuzuia kufanikiwa, tunakwenda kujifunza jinsi ya kutenganisha mtaji na faida ili biashara iweze kufanikiwa.
Kabla ya kuangalia hatua za kuchukua, tupate maoni ya wasomaji wenzetu walioomba ushauri kwenye hili.
“Changamoto yangu sijui kutenganisha faida na mtaji kwenye biashara.” – Q. Lyimo
“Changamoto kwenye biashara yangu najikuta natumia faida yote kwenye matumizi ya nyumbani imepekekea mtaji kupungua zaidi.” – N. J. Ryana
Kutenga mtaji wa biashara yako na fiada, zingatia mambo haya matano;
Moja; mtaji ni mali ya biashara.
Kosa moja ambalo wengi wanafanya ni kudhani kwa kuwa wameweka mtaji kwenye biashara, basi mtaji huo ni mali yao.
Hilo ni kosa kubwa, ukishaweka mtaji kwenye biashara hizo siyo fedha zako tena, bali ni fedha za biashara.
Mtaji ni mali inayomilikiwa na biashara, hivyo hupaswi kuuingilia kwa namna yoyote ile.
Unapoweka mtaji kwenye biashara ni sawa na umemkopesha mtu fedha, ni mali yake, huwez kuzichukua tena, bali yeye atakulipa kwa namna mliyokubaliana.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye biashara, ukishaweka mtaji kwenye biashara, hiyo ni mali ya biashara. Hupaswi kuhesabia tena fedha hizo za biashara kwenye mambo yako binafsi.
Unachoweza kukihesabia ni faida inayopatikana.
Hivyo weka mtaji kwenye biashara na jua kabisa hiyo siyo mali yako tena, bali ni mali ya biashara.
Mbili; fuatilia namba muhimu.
Mtaji ni mali ya biashara, faida ndiyo namna biashara inakulipa wewe.
Lakini kwa bahati mbaya sana, watu hawajui ni faida kiasi gani biashara inaingiza.
Hivyo wao wanajichukulia tu fedha kwenye biashara.
Ili uweze kujua faida ambayo biashara inatengeneza, unapaswa kufuatilia namba muhimu kwenye biashara hiyo.
Kuna mamba tano muhimu unazopaswa kuzifuatilia kila wakati ili kuweza kujua faida ya biashara yako.
1. Mtaji unaozunguka, hapa unajua ni kiasi gani cha fedha zilizopo kwenye biashara ni mtaji.
2. Manunuzi/uzalishaji, hapa unajua gharama zilizotumika kununua au kuzalisha bidhaa/huduma inayouzwa.
3. Mauzo, hala unajua kiasi cha mauzo yaliyofanyika.
4. Gharama za uendeshaji, hapa unajua gharama unazoingia kwenye kuendesha biashara.
5. Faida kamili, hii inapatikana kwa kuchukua mauzo kisha kutoa manunuzi na gharama za uendeshaji.
Kama huzijui na kuzifuatilia namba hizi, huwezi kujua faida na hivyo utaona kila fedha ni yako, utaishia kutumia mtaji na biashara kufa.
Tatu; tunza kumbukumbu ya kila kitu.
Wahenga walisema mali bila daftari hutumika bila habari.
Unapaswa kutunza kumbukumbu ya kila kitu kwenye biashara yako.
Kila senti inayotoka na kuingia kwenye biashara inapaswa kuwekwa kwenye kumbukumbu.
Bila utunzaji mzuri wa kumbukumbu huwezi kuzifuatilia namba muhimu za biashara.
Nne; tenga kiwango cha kujilipa.
Pamoja na kwamba faida inayopatikana kwenye biashara ndiyo mali yako, bado huwezi kuiondoa yote, kwani biashara inahitaji uwekezaji endelevu ili iweze kukua.
Hivyo unahitaji kutenga kiwango ambacho utajilipa kutoka kwenye biashara yako.
Unaweza kuchagua kujilipa kiwango fulani cha mshahara na hilo likaingia kwenye gharama za kuendesha biashara.
Au unaweza kuchagua kujilipa asilimia fulani ya faida inayopatikana na hilo lisiingie kwenye gharama za biashara.
Ukishapanga kiwango cha kujilipa, hicho tu ndiyo kiasi cha fedha utakachoondoa kwenye biashara, nyingine usiguse.
Tano; chukulia biashara kama siyo yako.
Tuwe wakweli, mambo haya ni rahisi kusema, lakini kuyatekeleza ni vigumu mno.
Ni vigumu ukubali kulala njaa wakati kuna fedha unaiona ipo kwenye biashara.
Au kuacha kununua kitu unachokipenda wakati una fedha za biashara.
Unahitaji kuwa na roho ngumu kweli kweli kuweza kuteseka wakati fedha za biashara zipo mbele yako.
Ni wachache wenye hiyo roho ngumu na wachache hao ndiyo wanaofanikiwa kwenye biashara.
Ipo njia rahisi ya kujijengea roho ngumu kwenye biashara ili uache kuingilia fedha za biashara.
Njia hiyo ni kuichukulia biashara siyo yako. Wewe jione tu kama mfanyakazi uliyeajiriwa kwenye biashara yako.
Kama umeajiriwa kufanya kazi benki, hata kama huna hela ya kula, huwezi kuchomoa hata elfu moja kwenye fedha za wateja ili ukale. Utaziangalia fedha hizo kwa adabu kabisa pamoja na njaa kubwa uliyonayo.
Kama umeajiriwa mahali kama mhasibu, pamoja na pesa kupita kwenye mikono yako, huzipigii mahesabu yoyote binafsi, kwa sababu unajua siyo zako.
Ni kiwango cha aina hiyo cha nidhamu unachohitaji kuwa nacho ili uweze kutenganisha fedha za biashara na mambo yako binafsi.
Bila ya kufanya hivyo ni vigumu sana kwa biashara kufanikiwa.

Rasilimali muhimu;
Kuna rasilimali muhimu unapaswa kuwa nazo ili uweze kuendesha biashara yako vizuri.
1. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kitakusaidia sana kujijengea nidhamu na tabia sahihi za kifedha..
2. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA kitakusaidia kujenga mfumo sahihi wa kuendeshabiashara.
3. Kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA kitakuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa unaendelea na kazi yako.
Kupata vitabu hivi wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa popote ulipo.
Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kutenganisha mtaji na faids ya biashara na biashara yako iweze kukua na kufikia mafanikio makubwa.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.