#TANO ZA JUMA #27 2019; Unayapoteza Maisha Yako, Mambo Sita Ya Kufanya Kila Asubuhi Ili Kufanikiwa, Hatua Tatu Za Kuondoka Kwenye Umasikini, Tatizo Lako La Kifedha Ni Tatizo La Kitabia Na Hatua Ya Kwanza Kuchukua Ili Kubadili Maisha Yako.

Rafiki yangu mpendwa,

Hongera sana kwa juma hili la 26 ambalo tumekuwa nalo na limefika ukingoni. Ni imani yangu kwamba juma hili limekuwa la kipekee sana kwako, umeweza kujifunza mengi na hata kujaribu mambo mapya yanayokuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Umefika wakati wa kujifunza mambo matano muhimu kabisa ya juma hili tunalomaliza, ambayo yanatupa maarifa na hamasa ya kuweza kupiga hatua zaidi.

Kwenye TANO ZA JUMA hili, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa The Miracle Morning: The Not-So-Obvious Secret Guaranteed to Transform Your Life: Before 8AM, ambacho kimeandikwa na Hal Elrod.

miracle morning

Kupitia kitabu hiki, Hal anatuonesha kwamba nguvu ya kuyabadili maisha yetu, kutoka umasikini na ukawaida mpaka kufika utajiri na mafanikio ipo ndani yetu. Na kwa kuwa kila mtu analalamika kwamba hana muda, Hal ametuonesha jinsi ambavyo kwa kutenga saa moja tu kila siku na kufanya vitu sita muhimu sana, maisha yako yanaweza kubadilika.

Kwa kufuata mafunzo haya ya Hal Elrod, kila siku unaianza na ushindi. Yaani kabla ya saa mbili asubuhi, unakuwa umeshajitangazia ushindi kwenye siku yako na hivyo ukirudia hivyo kila siku, lazima utafanikiwa sana, haijalishi ni nini unafanya.

Karibu sana tujifunze kwa kina kisha tuchukue hatua ili maisha yetu yawe bora zaidi.

#1 NENO LA JUMA; UNAYAPOTEZA MAISHA YAKO.

Pata picha hii rafiki yangu, mtu ameenda kwenye duka la kompyuta, na kuulizia kompyuta yenye uwezo mkubwa sana, akaoneshwa na akaipenda sana. Akainunua na kwenda nayo nyumbani. Lakini kila siku anaitumia kompyuta hiyo kusikiliza muziki tu, hakuna kingine anafanya nayo.

Au fikiria mtu mwingine, ambaye anaenda kununua gari kubwa ya abiria, yenye uwezo wa kubeba abiria 20 kwa wakati mmoja, lakini yeye anaitumia kama gari yake ya kwenda kazini asubuhi na kurudi nyumbani jioni. Mchana kutwa anakuwa ameipaki tu gari hiyo.

Unawezaje kuwaelewa watu wa aina hiyo? Bila shaka utawashangaa, iweje wanunue kitu chenye uwezo mkubwa sana, halafu wakitumie kwa matumizi madogo hivyo? Yaani mtu anunue kompyuta ambayo inaweza kutengeneza programu, kuendesha programu kubwa, kutengeneza picha na video, kuandika vitabu, kuingia kwenye mtandao na kupakua vitu muhimu, lakini mtu huyo anatumia kompyuta hiyo kusikiliza nyimbo tu? Lazima uone kuna shida mahali. Kadhalika kwenye gari, mtu atumie fedha nyingi, kununua gari yenye uwezo wa kubeba abiria wengi, lakini aitumie kama gari binafsi ya kutembelea, ambayo kwa muda mwingi haitumii, ni upotevu wa rasilimali.

Sasa kabla hujaendelea kuwashangaa watu hao na kuona wana matatizo, nikukatize kwa kukuambia hicho ndiyo umekuwa unafanya na maisha yako mpaka sasa.

Ukilinganisha uwezo mkubwa uliopo ndani yako, na yale unayofanya sasa, kwa kweli bado kabisa hujagusa hata asilimia 10 ya uwezo wako. Vitu unavyofanya na maisha yako, ni vidogo sana ukilinganisha na vitu vikubwa zaidi unavyoweza kufanya. Tena yule aliyenunua kompyuta na akaitumia kusikiliza nyimbo ana afadhali kuliko wewe, maana angalau yeye anafurahia nyimbo anazosikiliza kuliko wewe ambaye unakuwa na maisha ambayo huyapendi, lakini pia hakuna hatua unazochukua kuyabadili.

Ndiyo maana nakuambia kwamba unayapoteza maisha yako. Unapoteza uwezo mkubwa sana uliopo ndani yako ambao ungeweza kuutumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Unapoteza maisha kwa sababu unafanya mambo kwa mazoea, unafanya kwa viwango vya juu sana na hujaribu hatua kubwa na za tofauti zinazoweza kukutoa hapo ulipokwama sasa.

Unakazana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, halafu unashangaa pale unapopata matokeo ya tofauti. Unakimbilia kuiga na kushindana na wengine, halafu unashangaa pale maisha yako yanapokuwa yamekwama.

Hatua ya kwanza ya kuchukua ili uache kupoteza maisha yako ni kutambua kwamba wewe ni wa tofauti na wa kipekee sana. Kutambua kwamba chochote unachofanya sasa ni kwa kiwango cha chini sana ukilinganisha na uwezo mkubwa ulionao wa kufanya makubwa zaidi.

Ukishatambua hilo muhimu, sasa unachagua kuliishi kila siku. Kila siku kazana kuwa bora kuliko jana. Usikubali kufanya chochote kwa mazoea. Usikubali hata mara moja kufikiria kwamba umeshafika juu kabisa. Haijalishi unajiona umefika juu kiasi gani, bado unaweza kwenda juu zaidi.

Kupitia kitabu cha juma hili, utajifunza njia za kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi ya hapo yalipo sasa.

#2 KITABU CHA JUMA; MAMBO SITA YA KUFANYA KILA ASUBUHI ILI KUFANIKIWA.

Karibu rafiki kwenye uchambuzi wa kitabu chetu cha juma. Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa The Miracle Morning: The Not-So-Obvious Secret Guaranteed to Transform Your Life: Before 8AM, ambacho kimeandikwa na Hal Elrod.

Kwenye kitabu hiki ambapo tunakwenda kujifunza siri muhimu sana za mafanikio kwenye maisha na mambo sita ya kufanya asubuhi ili uweze kuwa na umiliki mkubwa wa siku yako na kuweza kufanya makubwa.

MOJA; ANDIKA HADITHI MPYA YA MAISHA YAKO.

Hal Elrod anaanza kitabu hiki kwa kutushirikisha historia fupi ya maisha yake na nyakati ngumu mbili ambazo amepitia kwenye maisha yake. Moja ni alipata ajali mbaya sana, ambayo ilipelekea kuvunjika mifupa mingi ya mwili na hata kufa kwa dakika 6 kabla hajaokolewa na madaktari. Baada ya ajali hii madaktari walimwambia hataweza kutembea tena wala kuwa na maisha ya kawaida. Lakini hakukubaliana na hilo, kwa kutambua na kutumia nguvu kubwa ya akili yake, aliweza kurudi kwenye maisha ya kawaida licha ya ajali kuharibu sana mwili na akili yake.

Kitu cha pili kigumu alichopitia Hal ni pale alipofilisika kabisa na kujikuta kwenye madeni makubwa baada ya kuwa amefikia mafanikio makubwa kifedha. Hali hii ilimletea hali ya kukata tamaa na kuona maisha yake hayawezekani tena. Lakini kwa kurudi kwenye nguvu yake, aliweza kuondoka kwenye madeni na kuwa na maisha bora tena.

Hivyo yale anayotushirikisha kwenye kitabu hiki, ni mambo ambayo yamemsaidia yeye binafsi kurudi kwenye maisha mazuri baada ya mambo kwenda vibaya kwenye nyakati mbili tofauti za maisha yake.

Hal anasema kila mtu anayo nafasi ya kuandika upya hadithi ya maisha yake. Badala ya kukubaliana na kila kinachotokea, unachagua kutengeneza kile unachotaka wewe.

Hebu leo hii kaa chini na jikumbushe hadithi ambazo unajipa kwa nini hujafanikiwa mpaka sasa. Je unajiambia huna elimu kubwa, huna wa kukusaidia au huthaminiwi? Je unajiambia huna bahati au wakati wako bado? Hizi ni hadithi za zamani zisizo na mashiko.

Leo hii kaa chini na andika hadithi yako mpya, hadithi ya mafanikio na anza kuishi hadithi hiyo, utaweza kuyabadili sana maisha yako na kupiga hatua.

MBILI; AMKA UKIWA NA UWEZO WAKO WOTE.

Jinsi unavyoamka asubuhi yako, kuna madhara makubwa sana kwenye matokeo unayopata kwenye siku yako na maisha yako kwa ujumla.

Watu wengi wamekuwa wanaamka asubuhi wakiwa hawana mpango wowote, hawana hamasa na wala hawana vipaumbele. Hivyo wanachelewa kuamka, lakini hata wanapoamka, hakuna kitu cha maana wanafanya zaidi ya kuanza kuhangaika na matukio ya dunia, kupitia mitandao ya kijamii na kufuatilia habari.

Hii ni njia ambayo siyo sahihi ya kuianza siku yako, unakuwa unatumia vibaya uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Anza kubadili jinsi unavyoamka na kuianza siku yako na utayaona maisha yako yakibadilika sana. Kwenye kitabu hiki tunakwenda kujifunza jinsi ya kubadili uamkaji wetu.

TATU; DUNIA YAKO YA NJE NI TASWIRA YA DUNIA YA NDANI.

Ukisimama mbele ya kioo, halafu kioo kikaonesha kwamba sura yako imevimba wakati wewe hutaki ivimbe, kusema kioo kinakudanganya ni kujidanganya wewe mwenyewe.

Hii ni kwa sababu kioo hakitengenezi sura yako, bali kinakuonesha sura hiyo jinsi ilivyo. Hivyo kama unataka kile unachoona kibadilike, unapaswa kuubadili kwanza mwili wako.

Hivi ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu. Tabia zinazoonekana nje yetu ni matokeo ya kile kinachoendelea ndani yetu, yaani fikra na mitazamo yetu. Hivyo kukazana kubadili vitu vya nje ni kupoteza muda kwa sababu hutaweza kupata matokeo unayotaka.

Kama kinachotokea nje yako hukipendi, basi unapaswa kuanza kubadili ndani yako. Anza kubadili fikra na mitazamo yako, anza kubadili hatua unazochukua na utaona matokeo unayopata yakibadilika yenyewe.

NNE; KWA NINI UMEAMKA ASUBUHI YA LEO?

Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa mazoea kiasi kwamba hakuna tena kinachowasukuma kuamka asubuhi. Mtu anakuwa anafanya kazi ambayo haipendi, au biashara inayomchosha kiasi kwamba alamu inapoita asubuhi kwamba muda wa kuamka umefika anajisikia kuchoka zaidi na kutokuamini kwamba muda wa kulala umeisha.

Na licha ya alamu kuita, wengi wamekuwa hawaamki mara moja, badala yake huendelea kujilaza wakijiambia wanajipa dakika 5 tu. Wanakuja kustuka nusu saa baadaye, wanaianza siku wakiwa wameshachelewa na hapo wanaiharibu siku nzima.

Hatua ya kwanza ya kuwa na maisha ya mafanikio ni kuwa na sababu kubwa ya kuianza siku yako. Unapaswa kuianza siku yako ukiwa na hamasa kubwa na mapenzi makubwa kwenye maisha yako binafsi na kazi unazofanya.

Pale alamu yako inapolia, unafurahia kuamka ukijua unakwenda kuigusa dunia kwa kile unachofanya. Ni wale wanaozianza siku zao kwa hamasa kubwa ndiyo wanaofanikiwa, kwa sababu wanazianza mapema na kutenga muda wa kufanya yale muhimu zaidi.

Hatua ya kwanza ya kukuwezesha kuamka ukiwa na hamasa na mapenzi makubwa ni kwenda kitandani ukiwa na nia ya kuamka ukiwa vizuri. Watu wengi huingia kitandani wakijiambia wamechoka na watachelewa kuamka, na hivyo ndivyo mwili unavyofanya. Lakini unapoenda kitandani ukijiambia kwamba utaamka mapema na ukiwa huna uchovu, mwili unafanya hivyo. Nikupe mfano mdogo, kumbuka siku ambazo una safari muhimu sana inayokutaka uamke asubuhi na mapema, unawahi kuamka kabla hata alamu haijaita, na unapoamka unakuwa huna uchovu kabisa.

TANO; MAMBO SITA YA KUFANYA KILA SIKU ASUBUHI ILI UWE NA SIKU BORA NA MAFANIKIO MAKUBWA KWENYE MAISHA YAKO.

Watu wengi wamekuwa wanaweka nguvu zao nyingi na umakini wao kwenye vitu ambavyo siyo muhimu. Mfano watu wengi wamekuwa wanahangaika sana na yale yanayotokea kwenye maisha yao, badala ya kuweka nguvu zao kwenye kile kilichopo ndani yao.

Wewe siyo yale yanayotokea kwenye maisha yako, bali wewe ni mtu, nafsi ambayo imebeba vitu vyake tofauti kabisa na yale yanayotokea kwenye maisha yako.

Maisha yako yana maeneo manne muhimu ambayo ndiyo unapaswa kuweka nguvu zako na umakini kama unataka kuwa na maisha bora. Maeneo hayo ni afya ya mwili, akili, hisia na imani. Afya ya mwili inahusisha hali ya mwili na hata nguvu ambazo mtu unazo. Akili inahusisha fikra zako na mtazamo ulionao. Hisia inahusisha zile hisia unazokuwa nazo kwenye maisha. Na imani inahusisha roho na nguvu kubwa isiyoonekana ambayo inatutawala wote.

miracle morning 2

Ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio, unapaswa kuyaboresha maeneo hayo manne kila siku. Na njia ya kuboresha maeneo hayo manne ni kufanya mambo haya sita kila siku asubuhi.

JAMBO LA KWANZA; KUKAA KIMYA (SILENCE)

Watu wengi wamekuwa wanaanza siku zao wakiwa na msongo wa mawazo kwa sababu wanakimbilia kuikabili dunia na kila kinachoendelea kabla hawajajitengenezea utulivu wa ndani.

Hatua ya kwanza kuchukua pale unapoianza siku yako ni kutenga muda wa kukaa kimya. Kukaa kimya kuna manufaa makubwa sana kwenye maisha yako, kwanza kunaituliza akili yako, kunakuondolea msongo wa mawazo na kukuwezesha kujitambua zaidi.

Katika zoezi hili la kukaa kimya, hukai tu kimya bila ya mpangilio wowote. Bali kuna mambo unayafanya kwa kukaa kwako kimya. Baadhi ya vitu unavyoweza kuvifanya kwenye ukimya wako ni kama;

 1. Kufanya tahajudi (meditation)
 2. Kusali/kuomba.
 3. Kutafakari kwa kina.
 4. Kupumua kwa kina.

Muda wa kufanya hili ni dakika tano. Unapoamka, dakika tano za kwanza kaa kimya ukisali, kutahajudi au kutafakari kwa kina maisha yako. Utaweza kuianza siku yako ukiwa na utulivu mkubwa.

JAMBO LA PILI; KUJIAMBIA KAULI CHANYA (AFFIRMATIONS)

Kila mtu huwa anaongea na yeye mwenyewe, lakini sehemu kubwa ya maongezi hayo huwa ni hasi. Watu ni wazuri sana kwenye kujikatisha tamaa wao wenyewe na hivyo kujizuia kufanikiwa. Na hili huwa juu sana wakati mtu anapoamka, anapokuwa amechoka na hapendi kile anachofanya, basi ni rahisi kujiambia kila aina ya kauli hasi.

Kuondokana na hilo, unapaswa kubadili namna unavyoianza siku yako, kwa kuianza kwa kujiamba kauli chanya. Chagua kauli chanya ambazo zinaonesha uwezo wako mkubwa na jinsi ya kuufikia kisha jiambie kauli hizi kwa kujirudia rudia.

Tengeneza kauli inayoeleza unataka kuwa nani, unataka kukamilisha nini na utakwendaje kukamilisha kitu hicho. Kauli iwe chanya tu na ujiambie kwa kujirudia rudia na kwa sauti. Tulishajifunza kwamba akili zetu za ndani (subconscious mind) huwa haziwezi kutofautisha uhalisia na kinachoigizwa, hivyo kwa kujiambia kauli chanya, akili yako inachukulia hayo ndiyo maisha yako na kutengeneza mazingira ya wewe kuweza kufikia maisha hayo.

Kitu kingine muhimu ni kuweka hisia wakati unajiambia kauli hizo chanya. Hisia zinaongeza nguvu zaidi kwa mwili wako kuamini kile unachojiambia ndiyo ukweli.

Mfano wa kauli chanya unayoweza kujiambia kama wewe ni mwandishi; mimi ni mwandishi bora kabisa, nimeandika vitabu maarufu na vilivyowasaidia wengi. Kwenye fedha unaweza kutumia kauli kama; mimi ni tajiri, utajiri wangu una thamani ya dola bilioni mbili na zaidi. Unapojiambia kauli hizi unaweka na hisia ambazo mtu unakuwa nazo kama kauli hizo tayari ni kweli.

Muda wa kufanya hili ni dakika tano. Hivyo baada ya dakika tano za kukaa kimya, chukua dakika tano nyingine za kujiambia kauli hizo chanya kwa sauti na huku ukiweka hisia.

JAMBO LA TATU; KUTENGENEZA TASWIRA CHANYA (VISUALIZATION)

Jambo la tatu kufanya kwenye asubuhi yako ni kutengeneza taswira chanya kwenye akili yako, za kile unachotaka kwenye maisha yako. Hapa unatengeneza taswira ya jinsi maisha yako yatakuwa baada ya kufika kule unakotaka kwenda. Kisha unaiweka picha hiyo kwenye akili yako na kujiona kama tayari umeshapata kile unachotaka au kufika unakotaka. Kutengeneza taswira kuna nguvu kama ya kujiambia kauli chanya, akili yako inachukulia ni kitu ambacho kimeshatokea na hivyo kukuweka kwenye mazingira ya kukamilisha hilo.

Tengeneza taswira za maono yako makubwa ya maisha, malengo uliyonayo, kile hasa unachotaka kufikia. Jione kama tayari umeshafika kule unakotaka kufika. Kama lengo lako ni kuwa mwandishi mwenye mafanikio basi jione kama tayari umeshafikia hilo, ona vitabu vyako vikiwa vinasomwa na mamilioni ya watu. Kama lengo lako ni kuwa tajiri mkubwa basi jione ukiwa tayari kwenye utajiri huo, ukiwa na kila ambacho unataka kuwa nacho ukishakuwa na utajiri huo.

Ukishatengeneza picha hizo za maisha unayotaka, kila asubuhi pitisha picha hiyo kwenye akili yako kama vile unatizama televisheni. Unapofanya hivi, tengeneza zile hisia ambazo utakuwa nazo baada ya kufikia hatua unazotaka kufikia. Kwa njia hii unaifanya akili yako ifanye kazi ya ziada kuhakikisha unachotengeneza kwenye akili yako kinatokea.

Lakini pia unahitaji kuianza siku yako kwa kutengeneza taswira ya siku bora kwako. Ona kila unachokwenda kufanya kwenye siku yako kwa mafanikio makubwa. Hili linakuandaa kuwa na siku bora sana.

Unahitaji dakika tano kufanya hili. Hivyo baada ya kukaa kimya, ukajiambia kauli chanya, unahitaji dakika nyingine tano za kutengeneza taswira chanya kwenye akili yako.

JAMBO LA NNE; KUFANYA MAZOEZI (EXERCISE)

Mazoezi yana manufaa mengi sana kwenye afya ya mwili, akili na hata hisia zetu. Na mazoezi ya asubuhi ndiyo yenye nguvu kubwa zaidi, kwa sababu yanakupa manufaa ambayo utanufaika nayo kwa siku nzima.

Mazoezi yanaboresha afya yako, yanaongeza nguvu zako, yanaimarisha kinga ya mwili na yanaifanya akili ifikiri kwa usahihi.

Hivyo kila unapoamka asubuhi, tenga muda wa kufanya mazoezi. Kwa kufanya mazoezi asubuhi siyo tu unapata manufaa hayo ya mazoezi, lakini pia unajihakikishia kupata muda wa mazoezi. Kwa sababu ukijiambia utafanya mazoezi baadaye, ni kitu kigumu sana kupata muda.

Tenga dakika 20 kila asubuhi za kufanya mazoezi ya mwili. Unapoamka unapaswa kuwa tayari umeshaandaa mazoezi gani unafanya na vifaa vya kufanya mazoezi hayo ili usipoteze muda kufikiria mazoezi gani unafanya.

JAMBO LA TANO; KUJISOMEA (READING)

Njia ya mkato, ya haraka na rahisi kubadili maisha yako ni kupitia usomaji. Unaposoma kitabu, unajifunza mambo ambayo mtu mwingine ametumia muda mwingi sana lakini wewe utatumia muda mchache kuyasoma.

Huwezi kuwa na maisha bora na yenye mafanikio kama hujifunzi, hasa kupitia usomaji wa vitabu. Vitabu vina hazina kubwa. Chochote unachosumbuka nacho kwenye maisha yako, kuna majibu yake kwenye vitabu, ni wewe kujua vitabu gani, kuvisoma na kisha kuchukua hatua.

Hivyo tenga muda wa kujisomea kwenye asubuhi yako. Na unasoma vitabu, siyo habari, magazeti au mitandao ya kijamii. Soma vitabu.

Jiwekee lengo la kusoma angalau kurasa 10 za kitabu kila siku. Kwa mpango huo, kila mwezi utakamilisha kusoma kitabu kimoja na kwa mwaka utasoma vitabu ambavyo siyo chini ya 10. Sasa ukisoma vitabu 10 tu kwa mwaka na ukafanyia kazi yale unayojifunza, hutabaki pale ulipo sasa.

Hili linahitaji angalau dakika 20, hivyo tenga dakika 20 za asubuhi yako mahususi kwa zoezi hili la usomaji.

JAMBO LA SITA; KUANDIKA MAWAZO YAKO (SCRIBING)

Akili yako huwa inapata mawazo mengi sana, mengi mazuri na mengine siyo mazuri. Kuna mawazo mazuri huwa unayapata, unajiambia baadaye utayakumbuka lakini unayasahau. Hii hutokea kwa kila mtu. Sasa ili kuondokana na hali hii ya kupoteza mawazo yako mazuri, jifunze kuandika mawazo yako, hili linayatunza, lakini pia linakufundisha kupangilia vizuri mawazo yako.

Hivyo kila asubuhi tenga muda wa kuandika kile kilichopo kwenye akili yako. Kitabu chako maalumu cha kuandika hayo (journal) au pia unaweza kutumia njia ya mtandao kuandika na kutunza mawazo yako.

Kwenye kitabu chako unaandika mawazo mapya unayoyapata, yale unayojifunza, mpenyo unaopata, magumu unayokutana nayo na jinsi unavyoyavuka na kadhalika. Kumbuka uandishi huu ni kwa ajili yako wewe, na siyo kwamba unaandika ili wengine wasome.

Kila mtu anapaswa kuwa na utaratibu huu wa kuandika mawazo yake, siyo kwa waandishi pekee. Kwa sababu unapoandika kitu, kwanza unakielewa zaidi na pili unakuwa umekitunza kwa marejeo ya baadaye.

Unahitaji dakika tano za kuandika mawazo yako kwenye kijitabu chako.

JINSI UNAVYOTUMIA SAA MOJA YA ASUBUHI YAKO.

Rafiki, mambo hayo sita tuliyojifunza hapa, ndivyo unavyotumia saa yako moja na ya kwanza kabisa ya siku yako.

Dakika 5 unakaa kimya, dakika 5 unajiambia maneno chanya, dakika 5 unapata taswira chanya, dakika 20 unafanya mazoezi, dakika 20 unasoma na dakika 5 unaandika. Jumla dakika 60.

Kama utaianza kila siku yako kwa kutumia saa yako ya kwanza kwa mambo hayo sita pekee, utaanza kuona jinsi ambavyo maisha yako yanabadilika na kuwa bora.

Muhimu; mpangilio wa kipi kianze na kipi kifuate unachagua wewe mwenyewe. Na pia muda wa kufanya kila jambo hapo unaweza kupanga mwenyewe kulingana na nafasi uliyonayo.

Kuna changamoto mbili ambazo zinaweza kukuzuia usinufaike na saa hii moja ya asubuhi, changamoto hizo ni kuchelewa kuamka na kukosa muda wa saa moja ya kufanya hayo. Kwenye #MAKINIKIA tutakwenda kujifunza jinsi ya kuvuka changamoto hizo mbili, kwa kuwa na mbinu za kuamka mapema, lakini pia kuweza kufanya mambo hayo 6 kwa dakika 6 pekee na ukapata manufaa makubwa. Je haupo tayari kutumia dakika 6 za siku yako kuyaboresha zaidi maisha yako? basi usikose makinikia ya juma hili.

SITA; ITENGENEZE ASUBUHI YAKO KULINGANA NA MAISHA YAKO.

Mwandishi anatuambia ili kupata manufaa ya haya anayotufundisha, tunapaswa kuamka asubuhi na mapema, saa moja kabla ya muda wako uliozoea kuamka.

Lakini siyo kila mtu au kila wakati mtu anaweza kuamka asubuhi na mapema. Kuna ambao wanafanya kazi za usiku, au wanachelewa kulala na hivyo kuchelewa kuamka.

Mwandishi anatuambia usiache mpango huu kwa sababu tu ratiba zako zinakuzuia kuamka asubuhi na mapema. Badala yake anasema muda wowote tunaoamka, saa moja ya kwanza tuitumie kwa mambo hayo sita. Mfano kama unaamka saa nne asubuhi, basi saa ya kwanza unaitenga kwa mambo hayo sita.

Kwa njia hii utanufaika sana bila ya kujali umelala au kuamka saa ngapi.

SABA; MCHAKATO WA KUBADILI TABIA NDANI YA SIKU 30.

Kuweza kuamka asubuhi na kufanya mambo haya 30 halitakuwa zoezi rahisi. Litakuwa zoezi gumu kwa sababu kwa sasa tayari una mazoea mengine ambayo yanapingana na kile unachopaswa kufanya.

Hivyo unahitaji kujenga tabia mpya. Sasa kwenye ujengaji wa tabia, mengi yamefundishwa, hasa kwenye muda kiasi gani unahitaji ili kujenga tabia mpya. Wapo wanaosema siku 21, wengine siku 30, wengine siku 90.

Mwandishi anasema kwa uzoefu wake na wale ambao amewakochi, siku 30 zinatosha kabisa kubadili na kujenga tabia yoyote.

Na kwa siku hizo 30 amezigawa kwenye makundi matatu.

Kundi la kwanza; siku 1 – 10; Isiyovumilika.

Katika siku ya kwanza mpaka ya 10 ya kujenga tabia mpya ni wakati mgumu sana. Kila wakati utakuwa unapata mawazo ya kuachana na tabia hiyo. Ni wakati mgumu na usiovumilika. Usipojua ugumu wa kipindi hichi cha kwanza, utakata tamaa, na hapa ndipo wengi huishia. Wewe jua ni siku 10 tu, hivyo endelea nazo na zitapita.

Kundi la pili; siku 11 – 20; Isiyofaa.

Baada ya siku 10 za kwanza ngumu sana, zinakuja siku kumi nyingine ambazo ule ugumu wa mwanzo haupo. Lakini siku hizi kumi za pili, bado utakuwa hujisikii vizuri kufanya tabia hiyo mpya. Katika siku hizi unakuwa umeanza kupata matokeo mazuri, lakini bado utekelezaji wa tabia hiyo ni mgumu kwako, kwa sababu unakuwa haujawa mazoea. Hiki ni kipindi ambacho ukikivuka basi tabia inajengeka vizuri.

Kundi la tatu; siku 21 – 30; Isiyozuilika.

Baada ya siku 20 za kwanza, tabia inaanza kuleta matokeo mazuri na pia inakuwa imeshazoeleka, hapa ndipo mtu anafikia hatua ambayo hawezi kuzuilika tena.  Hapa tabia inakuwa imeshajijenga kwa mtu na inakuwa sehemu ya maisha yake.

Hivyo rafiki, kama kuna tabia yoyote unayotaka kujenga kwenye maisha yako, panga kufanya tabia hiyo kwa siku 30 bila ya kuacha hata siku moja na utaweza kujenga tabia hiyo kwenye maisha yako. Kadhalika kama kuna tabia unataka kuivunja, acha kuifanya kwa siku 30 na utaweza kuiondoa kabisa.

Tenga siku 30 za kujijengea tabia mpya kulingana na yale uliyoifunza kwenye kitabu hiki, anza kwa kuamka asubuhi na mapema kuliko ulivyozoea. Fanya hivyo kwa siku 30. Na ili kuhakikisha huishii njiani, tafuta mtu ambaye atakusimamia kwa karibu, anaweza kuwa mtu wako wa karibu au kocha wako. Kwa kufanya hivi, utaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora sana kwa chochote unachotaka kuwa nacho au kufikia.

Hivi ndivyo unavyoweza kuyabadili maisha yako kwa kutawala asubuhi yako na kufanya mambo sita muhimu. Chukua hatua kwa yale uliyojifunza ili siku zako na maisha yako kwa ujumla yawe bora sana.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA TATU ZA KUONDOKA KWENYE UMASIKINI.

Kwenye jamii yoyote ile, kwenye nchi, na hata kwenye dunia kwa ujumla, kuna mgawanyo wa utajiri na mafanikio unaofanana. Ukienda popote na kuchagua watu 100, watu 95 watakuwa na maisha ya kawaida au ya chini na watu watano pekee ndiyo watakaokuwa na maisha bora na ya mafanikio. Katika watu hao 100 pia utakuta mtu mmoja, ana mafanikio makubwa sana kuliko wale 99 ukiwachanganya kwa pamoja.

Hivyo jamii imekuwa inagawanywa kwa asilimia, kuna asilimia 5 wenye mafanikio makubwa na asilimia 95 wenye maisha ya kawaida. Lakini pia kuna asilimia 1 wenye mafanikio makubwa mno, kuliko asilimia 99 inayobaki.

Swali ambalo wengi hujiuliza nani anapanga namba hizi? Na kwa nini namba hizi zinajitokeza kila mahali?

Tafiti nyingi zilizofanywa eneo la mafanikio, zinaonesha kwamba kinachowatofautisha watu kwenye mafanikio ni tabia ambazo watu hao wanazo. Vigezo ambavyo wengi wamekuwa wanafikiria vinachangia, vitu kama elimu, mazingira, na hata bahati havina nguvu kubwa kama tabia.

Kwenye makala ya juma hili, nimekushirikisha hatua tatu za kutoka kwenye maisha ya chini na umasikini kwenda kwenye utajiri na mafanikio ambazo mwandishi Hal Elrod ametushirikisha kwenye kitabu tulichojifunza juma hili. Hatua hizi tatu zinahusisha kujenga tabia bora kabisa zinazokuwezesha kufanikiwa.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya juma hili, unaweza kuisoma sasa hapa. Fungua maandishi haya kuisoma; Hatua Tatu (03) Zitakazokutoa Kwenye Umasikini Na Utegemezi Na Kukufikisha Kwenye Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Pia endelea kutembelea www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz kila siku ili ujifunze na kuweza kuwa bora zaidi.

#4 TUONGEE PESA; TATIZO LAKO LA KIFEDHA NI TATIZO LA KITABIA.

Nenda eneo lolote la kazi, ambapo watu wameajiriwa na wanalipwa kwa mwezi, kisha fuatilia watu mbalimbali tangu wanapolipwa mshahara mmoja mpaka kufikia mshahara mwingine. Chagua watu ambao wana vipato tofauti kabisa, yaani wenye mshahara wa chini kabisa na wa juu kabisa, lakini wote wanafanya kazi sehemu moja.

Picha utakayoipata ni hii, kabla ya mshahara mwingine kufikiwa, kila mtu atakuwa hana tena fedha. Yaani anayelipwa laki 3 kwa mwezi atakuwa hana fedha, na pia anayelipwa milioni tatu kwa mwezi naye pia anakuwa hana fedha.

Hivyo utaweza kujionea mwenyewe kwamba matatizo ya kifedha hayaanzii kwenye kipato kama wengi wanavyofikiri. Maana wenye kipato cha chini huwa wanafikiri siku kipato chao kikiongezeka basi wataondoka kwenye matatizo ya kifedha. Lakini wanachoshindwa kuelewa ni kwamba kuna wenzao ambao wana kipato kikubwa sana lakini bado wana matatizo ya kifedha.

Rafiki, matatizo ya kifedha yanaanzia kwenye tabia, na ndiyo maana watu wana matatizo ya kifedha bila ya kujali kipato chao.

Hivyo njia pekee ya kukabiliana na matatizo ya kifedha ni kubadili kwanza tabia ambazo mtu unazo. Bila ya kubadili tabia, haijalishi kipato chako kitaongezeka kiasi gani, bado utaendelea kuwa kwenye matatizo ya kifedha.

Zifuatazo ni tabia mbaya kifedha unazopaswa kuziacha;

 1. Kuruhusu matumizi kuwa makubwa kuliko kipato.
 2. Kutokuweka akiba.
 3. Kuruhusu matumizi yaongezeke pale kipato kinapoongezeka.
 4. Kununua vitu kwa kusukumwa na hisia, vitu ambavyo hukupanga kununua.
 5. Kuwa na njia moja pekee ya kuingiza kipato.

Zifuatazo ni tabia nzuri kifedha unazopaswa kujijengea.

 1. Hakikisha matumizi yako yanakuwa kidogo kuliko kipato chako.
 2. Kuweka akiba kwanza kabla hujaanza kutumia kipato chako.
 3. Kuwekeza akiba hiyo kwenye maeneo yanayoweza kuzalisha.
 4. Kununua vitu kwa mpangilio na uhitaji, kuacha kuishi maisha ya maigizo.
 5. Kuwa na vyanzo vingi vya kukuingizia kipato.

Ukiweza kujijengea tabia bora, basi utaweza kutatua changamoto nyingi za kifedha ulizonazo.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HATUA YA KWANZA KUCHUKUA ILI KUBADILI MAISHA YAKO.

“The moment you accept responsibility for EVERYTHING in your life is the moment you can change ANYTHING in your life.” – Hal Elrod

Hatua ya kwanza kuchukua ili kubadili maisha yako, ni kukubali kwamba kila kitu kwenye maisha yako ni wajibu wako. Hapa unaondokana kabisa na kulaumu au kulalamikia wengine pale ambapo maisha yako hayaendi vizuri.

Pale ambapo unaona maisha yako hayako kama unavyotaka yawe, basi jua hilo ni jukumu lako.

Kama unashindwa, jua wewe ndiye mwenye jukumu la maisha yako.

Kama unataka kufanikiwa, jua ni wewe pekee unayeweza kujifikisha kwenye mafanikio yako.

Hata kama kuna wengine wanakukwamisha kufanikiwa, kubali hilo kama jukumu na tatizo lako, kisha chukua hatua sahihi za kulitatua ili kufanikiwa zaidi kwenye maisha yako.

Kulalamika na kuwalaumu wengine ni kujiondoa kwenye nafasi ya kufanikiwa. Kwa sababu unapolaumu mtu mwingine, maana yake unampa jukumu la maisha yako, na hakuna aliye tayari kubeba jukumu la maisha yako.

Kama unataka kufanikiwa, kama unataka kuwa na maisha unayotaka na kuondoka kwenye maisha magumu, kubali maisha yako na kila kinachotokea kama wajibu wako, na kisha chukua hatua sahihi za kukutoa hapo ulipo sasa na kukufikisha mbali zaidi.

Rafiki, hizi ndiyo TANO ZA JUMA la 27, naamini umeondoka na vitu muhimu vya kwenda kufanyia kazi, muhimu zaidi kuimiliki asubuhi yako kwa kupata muda wa kukaa kimya, kujiambia kauli chanya, kujijengea taswira chanya, kufanya mazoezi, kusoma na kuandika mawazo yako. Kwa kufanya vitu hivi sita kila siku, utaweza kuwa na maisha bora sana. Pia jijengee tabia nzuri kifedha na beba jukumu la maisha yako kwa kutokulalamika au kumlaumu yeyote.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma kutoka kitabu hiki cha juma, nitakwenda kukushirikisha mbinu za kukuwezesha kuamka asubuhi na mapema kwa wale ambao wanapata shida ya kufanya hivyo. Hapa utaweza kuamka mapema na kutenga saa yako moja ya maajabu ambapo utafanya yale mambo sita tuliyojifunza. Pia nitakushirikisha jinsi ya kufanya mambo hayo sita ndani ya dakika sita. Yaani kwa zile siku ambazo umebanwa kweli na huwezi kutega saa nzima ya kufanya mambo hayo sita, unaweza kufanya ndani ya dakika sita tu na manufaa yake yakawa makubwa kwako kwa siku nzima. Usikose #MAKINIKIA ya juma hili ili ujifunze mambo haya muhimu kwa mafanikio yako.

#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM. Kujiunga na channel hiyo fuata maelekezo yaliyopo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu