Mpendwa rafiki yangu,
Mzazi amepewa mamlaka ya kuongoza familia pamoja na kuwapa watoto malezi bora. Msingi wa mzazi bora ndiyo chimbuko la mtoto bora. Malezi bora mzazi anayomfundisha mtoto wake yatamsaidia kuishi vema katika hii dunia.
Dunia huwa haina huruma iko kama vile sheria, kama hujui sheria siyo kigezo cha wewe kusamehewa na ndivyo dunia ilivyo. Kama hujui kuishi misingi yake utakua unaumia kila siku. Watoto wanatakiwa kupewa malezi bora ambayo yatawawezesha kusimama wao wenyewe na miguu yao na siyo kulelewa mpaka hali ya utu uzima.
Malezi ni kama msingi wa nyumba, unapokuwa na msingi wa nyumba mzuri basi utakua na nyumba bora halikadhalika kwa mtoto, unapokuwa na mtoto ambaye umemjenga katika malezi mazuri naye atasimama vizuri.
Kila mzazi anapaswa kuwa na sifa hizi mbili;
Moja, mzazi unapaswa kuwa kondoo yaani kuwa mnyenyekevu. Kuna wakati mzazi unatakiwa kuwa mnyenyekevu katika malezi ya watoto, unawaelekeza watoto kwa upendo na tena katika hali ya kujishusha. Unatakiwa uwe na hali ya urafiki kwa mtoto au watoto wako, kuna wakati unatakiwa kusimama na kuwa rafiki yako. Na kama tunavyojua mtu anakuwa anajiachia sana akiwa na rafiki yake yaani yuko huru kuongea kile anachopenda bila hofu.
Wewe kama mzazi unatakiwa muda mwingine uwe myenyekevu, jishushe pale unapotaka kumlea mtoto vizuri, mwelekeze kwa mfano, fanya vile ambavyo unataka mtoto wako awe.
SOMA;Hii Ndiyo Haki Ambayo Hupaswi Kumnyima Mtoto Wako
Mbili, kuwa mbwa mwitu yaani hapa kuwa mkali, baada ya kuwa mnyenyekevu, unamfundisha mtoto na hatii kile unachomwambia kuwa mbwa mwitu mara moja, vaa uhusika upya. Mpe adhabu anayostahili na siyo kumyima, kwani imeandikwa kuwa usimnyime mtoto adhabu unapomwadhibu unamwokoa na kuzimu.
Changamoto ya siku hizi wazazi wengi hawataki kuwa wakali hata pale watoto wanapokwenda kinyume, hawakemei, wengine wanaogopa hata kuwasema watoto eti kisa watakasirika na kuwaudhi. Mtoto akifanya kosa inabidi aonywe na siyo kumwachia afanye kile anachotaka. Ndiyo maana nimekuambia kuna wakati unatakiwa kuwa mkali na kuwa na wakati kuwa mpole.
Hatua ya kuchukua leo; kuwa na hali ya unyenyekevu na ukali pale ambapo mtoto anakwenda nje ya mstari usikubali kulifumbia macho, unapoona mtu anakwenda kinyume badilika haraka na mrudishe katika mstari njia sahihi.
Kwahiyo, unaweza kumlea mtoto wako kikondoo lakini jua kabisa unamtengenezea nafasi kuteseka hapa duniani, usifurahie pale unapoona mtoto anakwenda vibaya bali chukua hatua na msahihishe mwambie hivi hapana tunapaswa kwenda hivi na atatii lakini wewe usimfundisha ataona ni sahihi kwake.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana