Pesa haiwezi kununua furaha, ni kauli maarufu ambayo imekuwa inatumiwa na wengi, hasa wale ambao hawana fedha.

Wengine wanaotumia sana kauli hii ni wale ambao wamepata pesa kwa njia zisizo halali, labda wizi, ufisadi, utapeli na nyinginezo.

Tusisahau kundi la tatu, la watu ambao wanapata fedha nyingi kwa wakati mmoja, hata kama ni kwa njia halali, wengi huishia kulaumu wingi wa fedha wanazokuwa wamepata umeharibu maisha yao.

Swali ni je kauli ya kwamba fedha haiwezi kununua furaha ni ya kweli?

Jibu ni ndiyo na hapana.

Jibu ni ndiyo fedha haiwezi kununua furaha, kama hujui furaha yenyewe inauzwa wapi. Hebu fikiria uko jangwani na una fedha, lakini hakuna maji kabisa, fedha hiyo itakuwa na msaada gani?

Jibu ni hapana, kwamba fedha inaweza kununua furaha kama unajua wapi pa kununua furaha hiyo.

money-happiness.jpeg

Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza wapi pa kununua furaha kwa fedha unazotafuta.

Kwenye kitabu kinachoitwa Thinking, Fast and Slow kilichoandikwa na Daniel Kahneman ameeleza kwa kina sana jinsi mtu unavyoweza kuwa na maisha bora na yenye furaha, kwa kuanzia kwenye fikra zetu.

Anachotuambia Daniel ni kwamba, ubora wa maisha unaanzia kwenye fikra zetu kabla ya kitu kingine chochote. Iwe una fedha au huna, furaha ni zao la fikra zako kabla ya kitu kingine chochote.

Lakini fikra pekee haziondoi nafasi ya fedha, hivyo pamoja na kufanyia kazi fikra kama ambavyo Daniel anakwenda kutufundisha, lazima pia ufanyie kazi upande wa fedha.

Kuna tafiti nyingi za kiuchumi na kisaikolojia ambazo Daniel ameshirikisha kwenye kitanu hicho, na hapa nakwenda kukushirikisha mbili, kisha tutajifunza jinsi ya kununua furaha kwa fedha zako kwa maneno mengine, jinsi ya kuziweka fikra zako sawa ili uwe na furaha.

Ufukara unaondoa furaha.

Kwenye moja ya tafiti ambazo Daniel ametumia kwenye kitabu chake, inaonesha kwamba wale ambao wako kwenye umasikini mkubwa, ambao wanaishi chini ya kiwango cha kawaida cha maisha, wanakuwa na wakati mwingi wa kukosa furaha kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.

Mfano kitendo tu cha kuumwa na kichwa, kinawapelekea walio kwenye ufukara kupatwa na wasiwasi zaidi kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.

Katika changamoto za kawaida za maisha, kama kuumwa, kufukuzwa kazi, biashara kufa, kutengana na mwenza, zinawaumiza zaidi walio kwenye umasikini kuliko wale ambao hawapo kwenye umasikini.

Na kikubwa zaidi ambacho Daniel ametushirikisha kwenye hili ni kwamba kwa walio masikini, maamuzi yoyote anayofanya ni ya kupoteza.

Iko hivi, sisi binadamu huwa tunaepuka hali ya kupoteza na kupenda hali ya kupata. Hivyo hatua yoyote ya kupoteza tunayochukua, huwa tunajisikia vibaya na hilo linachangia kukosa furaha.

Kwa kuwa masikini ana uhaba wa fedha, kila fedha aliyonayo haimtoshi, hivyo akitumia fedha hiyo kupata kitu fulani, anakuwa amechagua kukosa kitu kingine. Una elfu 5 mfukoni, unataka kwenda kujiburudisha mahali, ungependa kununua chakula na kinywaji, lakini fedha hiyo haitoshi, hivyo utaishia kupata chakula tu, au kinywaji tu.

Haijalishi chakula utakachopata au kinywaji utakachokunywa kitakuwa kizuri kiasi gani, akili yako haitaangalia kile ulichopata, bali itafikiria kile ulichokosa. Hilo ndiyo linachangia hali ya kukosa furaha kwa walio masikini.

Maumivu ya kukosa ni makubwa kuliko raha ya kupata. Ukipoteza elfu 10, utaumia kuliko raha utakayoipata kwa kuokota kiasi hicho hicho cha fedha.

SOMA; Hatua Tatu (03) Zitakazokutoa Kwenye Umasikini Na Utegemezi Na Kukufikisha Kwenye Utajiri Na Uhuru Wa Kifedha.

Kiwango cha ukomo wa furaha kwenye utajiri.

Kwa walio kwenye umasikini wa kupindukia, kila ongezeko la fedha au utajiri litamfanya mtu awe na furaha zaidi. Kadiri utajiri unavyokua, ndivyo mtu anavyofanya maamuzi ya kupata zaidi kuliko kupoteza.

Hivyo mtu anajikuta anaweza kupata kila anachotaka, hivyo halazimiki kuvumilia kupoteza kimoja ili kupata kingine. Muda wote akili yake inafikiria vile anavyopata, na hivyo anakuwa na furaha kwa muda mwingi.

Lakini usidanganyike, hali haitaendelea hivyo kadiri utajiri unavyokua.

Na hapa ndipo Daniel anapotushirikisha utafiti mwingine ambao unaonesha kuna kiwango cha juu cha utajiri ambacho mtu akishafikia, ongezeko zaidi la utajiri halileti furaha.

Kwa nchini Marekani, ambapo ndipo utafiti huo ulifanywa, kiwango hicho ni pato la mwaka la dola 75,000 (wastani wa tsh milioni 174). Kwa huku kwetu na kulingana na maisha ya mtu, kiwango kinaweza kuwa chini zaidi ya hapo.

Utafiti huo unatuonesha kitu kimoja, kwamba kuna kiwango cha fedha ambazo mtu akishakifikia, ongezeko zaidi halimletei furaha. Chini ya kiwango hicho, kila kipato kinapoongezeka furaha nayo inaongezeka. Baada ya kufikia kiwango hicho, nyongeza ya kipato haiongezi furaha kwa mtu.

Mwandishi anaenda mbali zaidi na kueleza kwamba kinachofanya fedha zaidi isilete furaha kwa wale ambao tayari ni matajiri ni kadiri fedha inavyoongezeka, ndivyo vitu vidogo vidogo vinavyokosa thamani kwao. Mfano ukiwa huna fedha nyingi, kwenda mapumziko kwenye eneo lolote utafurahia. Lakini ukiwa na fedha nyingi, kufanya maamuzi ya eneo lipi ukafanye mapumziko inakuwa vigumu, na hata ukienda eneo moja, bado unaona ungefurahia zaidi kama ungeenda eneo jingine.

Hilo linakurudisha pale pale kwenye hali ya kupoteza, ambapo sasa hupotezi kwa kuwa huna fedha, bali unapoteza kwa sababu fedha inakupa machaguo mengi.

Mahali sahihi pa kununua furaha.

Tumeona kwenye tafiti hizo mbili, kwa nini ukiwa masikini sana unakosa furaha na ukiwa tajiri sana unakosa furaha.

Swali ni je hatua zipi unazoweza kuchukua ili uweze kuwa na furaha kwenye maisha yako, bila ya kujali upo kwenye umasikini au utajiri?

Hatua kuu kabisa ni moja; kudhibiti fikra zako, hasa mfumo wa kwanza wa kufikiri ambao kwenye kitabu chake Daniel anauita mfumo unaofikiri kwa haraka, unaotumia mihemko na taarifa zinazopatikana kwa urahisi.

Na njia ya kudhibiti fikra zako ni kuacha kuangalia ulichopoteza au kukosa na kuangalia kile ambacho tayari unacho, kile ulichopata.

Ulikuwa na elfu tano yako mfukoni na ukataka ujiburudishe, ukagundua huwezi kupata chakula na kinywaji kwa kiasi hicho, badala ya kula chakula huku unafikiria kinywaji ulichokosa, kula chakula huku ukifikiria jinsi kilivyo kitamu, jinsi ambavyo hujawahi kukila kwa muda mrefu na jinsi ambavyo kuna wengine hawawezi kupata chakula kama ulichopata wewe.

Kwa njia hii, akili yako itaangalia mazuri, itaachana na mabaya, itaona hakuna unachopoteza na utajisikia vizuri, kitu ambacho kitafanya maisha yako yawe na furaha.

Furaha kwenye maisha ni matokeo ya pale unapopeleka fikra zako na siyo kinachoendelea kwenye maisha yako kwa ujumla. Kwenye kitabu hicho hicho, mwandishi ameshirikisha tafiti nyingine zinazothibitisha hilo.

Ulifanyika utafiti ambao ulihusisha jaribio la mtu kuokota fedha. Katika utafiti huo, watu waligawanywa katika makundi mawili na kundi moja waliulizwa wajibu ubora wa maisha yao, kundi la pili waliombwa waende kuchapa karatasi na kwenye mashine ya kuchapa kuna fedha ilikuwa imewekwa, hivyo kuona wameokota fedha hiyo, baada ya hilo waliulizwa kuhusu ubora wa maisha yao. Wale waliookota fedha walijibu kwamba maisha yao ni bora kuliko wale ambao hawajaokota fedha. Hii inaonesha jinsi ambavyo kile kinachoendelea kwa wakati huo kwenye maisha ya mtu ndiyo kinachotumika kufanya tathmini. Anayeokota fedha anajiona ana bahati na hivyo kuona maisha yake ni bora.

Ukiweza kuweka hilo kwenye maisha yako, kwa kuona kila kinachoendelea ni bahati kwako, akili yako itafikiria unapata na hupotezi, kitu ambacho kitakuondolea maumivu yanayotokana na hali ya kupoteza, kama tulivyojifunza awali.

SOMA; Povu La Pesa Kwa Wale Wanaosema Pesa Ni Chanzo Cha Maovu.

Mambo mengine muhimu kuzingatia kwenye fedha.

Kudhibiti fikra zako na kuziweka kwenye yale unayopata badala ya unayopoteza ni hatua ya kwanza kwenye kuwa na furaha.

Yapo mengine muhimu ya kuzingatia kwenye upande wa fedha, ili uondoke kwenye umasikini ambao utakubughudhi mara nyingi.

  1. Kazana kukuza zaidi utajiri wako, kuwa kwenye umasikini ni mzigo unaoumiza, epukana nao.
  2. Fanya kitu unachopendelea kufanya, kazi au biashara isiwe mzigo kwako, bali iwe kama mchezo kwako.
  3. Fanya mapumziko ambayo yanakutaka ufanye kitu (active) kuliko mapumziko ya kukaa tu (passive). Mfano wa mapumziko ya kufanya kitu ni matembezi, michezo, mazoezi, mazungumzo na wengine. Mfano wa mapumziko ya kukaa ni kuangalia tv, kuperuzi mitandao na kutumia vilevi.
  4. Usidharau vitu vidogo vidogo kwenye maisha, hata kama utajiri wako umekuwa mkubwa kiasi gani. Ni vitu vidogo vidogo ndivyo vinavyoleta furaha kwenye maisha.
  5. Tambua kwamba, hakuna chochote kwenye maisha kitakachobadili hali yako ya furaha kwa muda mrefu zaidi ya ilivyo sasa. Hata ukipata ajali na ukawa kilema, baada ya muda utarudi kwenye hali yako ya furaha ya sasa. Hata ukishinda bahati nasibu ya kiasi kikubwa cha fedha, utakuwa na furaha siku za mwanzo, baada ya muda utarudi kwenye kiwango chako cha awali. Hivyo wajibu wako, ni kukuza kiwango chako cha kawaida cha furaha, kwa kuweka umakini wako kwenye yale mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako.

Rafiki, yapo mengi sana ya kujifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha Thinking, Fast and Slow na nimekichambua kwa kina kabisa sehemu zote tano za kitabu chenye sura 38 huku kukiwa na mengi ya kujifunza kwenye kila sura kuhusu kufanya maamuzi sahihi na kuwa na maisha bora.

Karibu upate uchambuzi kamili wa kitabu hicho kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua; www.t.me/somavitabutanzania Kisha bonyeza JOIN CHANNEL na utapata uchambuzi wa kitabu hicho na vingine vingi.

Pia usikose kupata na kusoma vitabu hivi vitatu vitakavyokusaidia sana kwenye safari yako ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa;

  1. ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambapo utajifunza kuanzia kuongeza kipato, kudhibiti matumizi, kuweka akiba na kuwekeza.
  2. BIASHARA NDANI YA AJIRA, ambapo unajifunza jinsi ya kuanzisha na kukuza biashara ukiwa kwenye ajira ili kufikia uhuru wa kifedha.
  3. TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA, ambapo utajifunza siri 50 za mafanikio, utapata chambuzi 50 za vitabu vizuri vya mafanikio pamoja na mafunzo mengine mazuri.

Vitabu hivyo vitatu ni nakala ngumu na kuvipata wasiliana na mtu wa mauzo kwa namba 0752 977 170. Kama upo Dar utaletea ulipo na kama upo mkoani utatumiwa au kuunganishwa na wakala aliye karibu.

Karibu upate maarifa sahihi yatakayokuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha na kufanikiwa.

Nisisahau kukukumbusha kwamba kama bado hujawa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unajinyima mengi na kujiweka kwenye hatari ya kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Tuma sasa ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapata maelekezo ya kujiunga.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

elimu fedha 2