Basi sababu kubwa ni kwamba hujaanza kuyaishi maisha.

Kuwa na kila unachotaka ni sentensi ngumu sana kuielewa. Kwa sababu kwenye jamii zetu ni wachache sana wanaojua ni nini hasa wanachotaka kwenye maisha yao.

Na hii ni kwa sababu tangu tunazaliwa, tunakua mpaka tunakuwa watu wazima, wengi hawajawahi kupata nafasi ya kukaa na kufikiri wao wenyewe kuhusu maisha yao na nini hasa wanachotaka.

Kila kitu ambacho watu wanafanya, ni kwa sababu wameambiwa hicho ndiyo sahihi kufanya. Mfano tangu utoto mtu unaambiwa soma kwa bidii, utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Unapomaliza masomo ya chini na kwenda masomo ya juu ya kuchagua fani ya kusomea, unaambiwa chagua fani ambayo itakulipa vizuri na yenye kazi za uhakika. Au chagua fani ambayo ufaulu wako unaruhusu.

Watu wanafuata hilo, wanachagua fani ambazo zinaonekana kulipa sana kwa wale walionazo. Mtu anasoma kwa bidii na kuhitimu masomo yake. Na baada ya muda huenda anapata kazi ya fani aliyosomea, na kwa kuwa fani hiyo inalipa vizuri basi anapata kile ambacho wengine nao wanacho. Fedha za kutosha, mali na mengine ambayo watu wa nje wanaona mtu huyo amefanikiwa. Lakini ndani ya mtu huyo bado kuna utupu ambao hauzibiki.

Hili pia lipo kwenye biashara, mtu anataka kuingia kwenye biashara lakini kigezo kikuu ni kuangalia biashara gani inalipa zaidi. Anaipata na kuingia, anafanya vizuri kwenye biashara, lakini bado maisha yake yanaonekana hayajakamilika.

Kukamilika kwa maisha, kuwa na furaha na maisha ni kitu ambacho kinaanzia ndani ya mtu na siyo nje. Kitu ambacho mtu anaweza kukipata kama atapata nafasi ya kujijua yeye mwenyewe, kujitafakari na kuweza kuchukua hatua sahihi kwa maisha yake.

Kama huna furaha kwenye maisha yako, bila ya kujali upo kwenye ngazi ipi ya maisha, sababu kubwa ni kwamba hujaanza kuyaishi maisha yako. Unaishi maisha ya wengine, hivyo hata kama utaonekana umeshinda kwa viwango vyao, kwa viwango vyako mwenyewe unakuwa umeshindwa, tena vibaya sana.

Kazana kujijua wewe mwenyewe, kujua nini hasa unataka kwenye maisha yako na kuweka juhudi kufikia lile kusudi la maisha yako. Utakuwa na furaha zaidi kwa kuishi kusudi la maisha yako hata kama kwa nje huonekani kushinda au kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha