Maisha yanapaswa kuwa ya furaha wakati wote, iwe una kila unachotaka au huna.

Lakini maisha ya wengi yamekuwa siyo ya furaha, kwa sababu wengi wamekuwa wanajiambatanisha na matokeo wanayotaka kupata.

Sasa inapotokea kwamba hawapati matokeo hayo, wanaona maisha yao hayajakamilika na hilo linavuruga furaha waliyonayo kwenye maisha yao.

Hivyo ni muhimu sana uache kujiambatanisha na matokeo unayotarajia kupata. Hili halimaanishi usijitume, badala yake jitume sana, lakini ikitokea hujapata ulichotaka, usijione hufai, badala yake jua ni jambo la kawaida kutokupata kila unachotaka na hivyo kutovuruga utulivu na furaha ya maisha yako.

Sababu nyingine kubwa kwa nini usijiambatanishe na matokeo unayotaka kupata ni kwa sababu huwezi kudhibiti matokeo hayo. Unaweza kujidhibiti kwa kuchukua hatua sahihi, lakini huwezi kudhibiti ni matokeo gani utakayopata.

Hivyo ili kuwa na maisha tulivu na yenye furaha, usijiambatanishe na matokeo unayotegemea.

Badala yake jiambatanishe na tabia zako, hizi ziko ndani ya uwezo wako wa kudhibiti na ukizifanya kuwa bora zaidi unaweza kupiga hatua zaidi.

Pia jiambatanishe na kwa nini yako, lile kusudi kubwa la maisha yako, na kadiri unavyolifanyia kazi, ndivyo unavyosukumwa kuchukua hatua zaidi na kufanikiwa zaidi.

Weka matumaini na mategemeo yako makubwa kwenye vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wako, vitu unavyoweza kuvidhibiti. Kwa vilivyo nje ya uwezo wako, pokea matokeo unayopata na kisha songa mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha