Moja ya njia ambazo watu wamekuwa wanajizuia kujifunza na kukua zaidi wao wenyewe ni kuchagua kutokuwasikiliza watu ambao wanatofautiana nao.
Watu wengi huona wale ambao wanafikiri au kufanya tofauti na wao wanavyofanya wanakosea au hawajui wanachofanya.
Lakini hilo ni kosa kubwa, kwa sababu hata wao wanakuchukulia hivyo, wanakuona unakosea au hujui unachofanya.
Kama utachagua kuwasikiliza wale ambao wanatofautiana na wewe, utapata nafasi ya kujifunza kwa kina zaidi, nini kinawafanya wafikiri na kufanya tofauti na pia utaweza kupata uelewa wa kina kwa nini wewe unafikiri na kufanya tofauti na wao.
Dunia ya sasa imetengeneza mazingira ya watu kuchagua kuwasikiliza wale tu ambao wanakubaliana nao.
Kama kuna mtu hukubaliani naye kwenye mitandao ya kijamii basi unaweza kumzuia usione vitu vyake au kufuta naye urafiki kabisa.
Unaweza kuchagua kufuatilia habari zile unazopenda tu, zile unazokubaliana nazo.
Unaweza kuchagua kusoma vitabu unavyotaka kusoma pekee, vile ambavyo vinaendana na mtazamo ulionao.
Lakini kwa kufuata wale unaokubaliana nao, kupata habari zinazoendana na wewe na hata kusoma vitabu unavyokubaliana navyo tu siyo njia bora kwako kujifunza. Badala yake unakuwa unatengeneza upendeleo, unakuwa unajijaza upepo wako mwenyewe, ambao ni rahisi sana kukupoteza.
Kitu kingine muhimu ni kwamba unaposhindwa kuwasikiliza wale wanaotofautiana na wewe, unashindwa kujifunza msingi muhimu sana kwenye maisha ambao ni kuwavumilia wengine.
Kama mtu akipishana na wewe kauli mtandaoni hapo hapo unamfungia (block) au unafuta naye urafiki (unfriend/unfollow) basi inaonesha kwamba huna uvumilivu kwa wengine, kitu ambacho ni hatari sana kwenye maisha yako.
Hapa duniani, hakuna chochote utakachofanya na kila mtu akakubaliana na wewe. Unaweza kufanya kazi kwa juhudi kubwa, ukapata fedha zako kwa taabu sana, na ukaamua kuzitoa fedha hizo kama msaada kwa wale wenye uhitaji. Wewe si unaona ni jambo zuri na la maana? Nakuhakikishia kuna watakaoona ulichofanya siyo sahihi, na watakuwa na sababu zinazoonekana za msingi kwa nini unachofanya siyo sahihi na ungepaswa kufanya kitu kingine ambacho kwao ni sahihi.
Katika hali kama hii, hupaswi kupata hasira, hupaswi kuwafungia watu au kufuta nao urafiki. Bali unapaswa kuwasikiliza, kuwaelewa na kisha kufanya kile ambacho ni sahihi. Kama ulichokuwa unafanya awali ndiyo sahihi basi unaendelea kukifanya. Kama kile wanachokuambia wengine ndiyo sahihi basi kifanye hicho.
Kinachotufanya tuweze kuishi hapa duniani ni uwezo wetu wa kuvumiliana, kitu ambacho kwa sasa kinapungua sana kutokana na uwezo wa kuwazuia wale tusiokubaliana nao wasitufikie.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,