Eneo lolote lenye msongamano mdogo ndiyo eneo lenye fursa kubwa za mafanikio.

Kuanzia kwenye kazi, biashara na mambo mengine ya maisha, kadiri watu wengi wanavyokuwa wanafanya kitu, ndivyo thamani ya kitu hicho inapungua.

Nimekuwa nasema, kama unataka kufanikiwa lakini huna watu waliofanikiwa wa kujifunza kwao, basi angalia kile ambacho wengi wanafanya halafu wewe usikifanye.

Yaani ukishaona kitu kinafanywa na watu wengi, basi usikifanye kabisa, au ukikifanya basi kifanye kwa njia ya tofauti kabisa na wanavyofanya wengine.

Vitu vinavyofanywa na wengi ni vitu rahisi na visivyokuwa na thamani. Huwezi kufanikiwa kwa kufanya vitu rahisi na visivyo na thamani.

Utafanikiwa kwa kufanya vitu vigumu, vitu adimu na vyenye thamani kubwa kwenye maisha ya wengine.

Na huhitaji kumuomba ruhusa mtu yeyote ili kufanya vitu vigumu, adimu na vyenye thamani kubwa. Unahitaji kujiruhusu mwenyewe na kuwa tayari kuwapuuza wanaokukatisha tamaa kwa maneno kwamba haiwezekani au utashindwa.

Kwa sababu unapofanya kitu ambacho wengine hawafanyi, unakuwa tishio kwao na unapokuwa tishio unaanza kupokea mashambulizi mbalimbali. Hilo lisikutishe wala kukurudisha nyuma. Kazana kufanya kile kilicho bora na tofauti na hapo ndipo mafanikio yako yalipo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha