Kiwango chako cha mafanikio kwenye maisha ni sawa sawa na kiasi cha milango unayofungua kwenye maisha, na siyo milango unayofunga.

Unafungua milango pale unapokuwa tayari kwa fursa zinazoendana na kile unachofanya na kuhakikisha wale unaowalenga wanajua kuhusu uwepo wako na wanajua wanawezaje kunufaika na wewe.

Unafunga milango pale unapokosa maandalizi ya fursa na kuogopa kuwafanya watu wajue kuhusu uwepo wako au jinsi ya kunufaika na wewe.

Kila siku kazana kufungua milango zaidi, kwa kuhakikisha una maandalizi sahihi yanayoendana na zile fursa ambazo unafanyia kazi. Asiwepo mtu mwingine yeyote ambaye anajua kuhusu unachofanya zaidi ya unavyojua wewe. Bobea kwenye kile unachofanya, watu wanapokuwa na uhitaji, basi wanajua ni wewe unayeweza kuwapa kilicho bora zaidi.

Lakini kubobea pekee hakutoshi, haijalishi unajua kiasi gani, kama hakuna anayekujua basi ujuaji wako hautasaidia. Hivyo sehemu ya pili muhimu kwenye kufungua milango yako ni kufanya masoko. Kuhakikisha kila mtu mwenye uhitaji wa kile unachofanya au kutoa basi anajua kuhusu uwepo wako, uwepo wa kitu hicho na jinsi ambavyo kitamsaidia. Usiwe mtu wa kujificha kwa kile unachofanya, tumia kila fursa kujitangaza zaidi, kila unapokutana na watu waeleze kuhusu unachofanya.

Usione aibu kujitangaza kwa kile unachofanya, usijidanganye kwamba ukiwa mzuri kwenye kile unachofanya basi watu watakutafuta wenyewe. Kwa sasa watu wamevurugwa, wanakutana na kelele nyingi sana kwenye siku yao, hivyo ili wajue kuhusu uwepo wako, lazima uwe na njia bora ya kuwafikia.

Fungua milango zaidi na utaweza kufanikiwa zaidi. Jua sana unachofanya na wafikie wengi zaidi na hakuna kitakachoweza kukukwamisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha