“As Plato said, every soul is deprived of truth against its will. The same holds true for justice, self-control, goodwill to others, and every similar virtue. It’s essential to constantly keep this in your mind, for it will make you more gentle to all.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.63

Siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tuna wajibu mkubwa mbele yetu, wa kwenda kuweka juhudi kubwa sana leo ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WASAMEHE KWA SABABU HAWAJUI…
Kuna wakati watu wanatuudhi, wanatukwaza na hata kutusumbua kiasi kwamba tunakasirika sana kwa yale ambayo wanayufanyia.
Tunajiuliza kwa nini wafanye hivyo kwetu.
Lakini ambacho hatujiulizi ni je watu hao wanajua kwa kiasi gani usahihi wa kile wanachofanya?

Unapochunguza, unagundua kwamba watu wengi hawajui yale wanayoyafanya.
Hawajui kama ni sahihi au siyo sahihi, na hawajui madhara yake kwa wale wanaowafanyia.
Hivyo hata ukikasirishwa na watu hao, bado haitakusaidia wewe wala wao.
Hivyo hatua sahihi ni kuwasamehe wale ambao wanafanya mambo ya kukukwaza, kukuudhi au kukuumiza.
Badala ya kukasirika na kuumia, waeleze wazi wanachofanya siyo sahihi, kisha usitake kusikiliza utetezi au maelezo yao, maana watajitetea kwamba ni sahihi, wakati hawajui.
Wewe wasamehe.

Mtoto mdogo akifanya kitu ambacho siyo sahihi unamsamehe, unajua ni mtoto, hajui na hivyo atajifunza.
Lakini mtu mzima anapofanya kitu ambacho siyo sahihi unaona amefanya kwa kusudi, na hivyo kukasirika sana. Unapokosea ni kufikiri kwamba kila mtu mzima anajua anachofanya.
Wengi sana wanaendesha maisha yao, hawajui hata wanaenda wapi, sembuse kujua kipi sahihi kufanya?
Wasamehe watu kwa sababu hawajui wanalofanya, na maisha yako hayatakuwa na matatizo madogo madogo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwasamehe wale ambao wanafanya tofauti na matarajio yako, kwa sababu hawajui wanalofanya.
#WasameheWasiojua #UsikubaliKukasirishwa #DhibitiHisiaZako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1