Watu wengi huanza wakiwa na ndoto kubwa kwenye maisha yao,

Ndoto hizo zinawasukuma wajitume zaidi, wanaweka juhudi kubwa usiku na mchana bila ya kuchoka wala kukata tamaa.

Kutokana na juhudi kubwa wanazoweka, wanafikia ndoto kubwa walizokuwa nazo.

Lakini baada ya kufikia ndoto hizo wanashangaa kwamba maisha siyo bora kama walivyofikiri. Wanajikuta hawana furaha ya kudumu kama walivyotegemea.

Walipofikia ndoto hizo walipata furaha ya muda mfupi, lakini baada ya hapo kila kitu kinaonekana kawaida.

Japo kwa nje mtu anaweza kuonekana amefika juu na ana furaha sana, lakini ndani ya mtu mwenyewe anakuwa anaona bado kuna kitu hakijakamilika.

Hii ni hali ya kawaida kabisa kwetu sisi binadamu, tunapokuwa tunataka kitu kikubwa, tunakuwa na msukumo mkubwa wa kukitafuta, lakini tukishakipata, tunakichukulia kawaida.

Ubongo wetu umetengenezwa kwa namna ya kutaka vitu vipya kila wakati.

Hivyo basi, ili kuvuka hali hii, kuondokana na hali ya kukosa furaha pale tunapofikia ndoto kubwa tunazokuwa nazo, tunapaswa kuendelea kuota zaidi kila siku.

Hii ina maana kwamba, kama umejiweka ndoto kubwa na kuifikia, usiridhike na kuishia hapo, jiwekee ndoto kubwa zaidi ya hiyo ya awali.

Hii ina maana kwamba maisha yako yote kuna kitu kikubwa unachokuwa unafanyia kazi ili kukifikia. Hili ndiyo linakupa msukumo mkubwa wa kuendelea kujituma na kuona unazidi kukamilika zaidi.

Utaona watu waliofanikiwa sana bado wanaendelea kujituma kila siku kama vile ndiyo wanaanza, ni kwa sababu wanajua wakisharidhika tu na kile walichonacho, basi changamoto zinaanzia hapo.

Kuishi ndoto yako ni kuendelea kuota kila wakati, unachokiona ni kikubwa sana leo, baada ya kukifikia kinakuwa cha kawaida kabisa. Unahitaji kikubwa zaidi cha kuendelea kufanyia kazi kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha