“Whenever you have trouble getting up in the morning, remind yourself that you’ve been made by nature for the purpose of working with others, whereas even unthinking animals share sleeping. And it’s our own natural purpose that is more fitting and more satisfying.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.12

Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata fursa nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUFANYA WEWE KUWA MTU…
Kitu pekee kinachokufanya wewe kuwa mtu,
Kitu kinachokutofautisha wewe na wanyama,
Ni kazi unayofanya yenye mchango kwa watu wengine.
Kama hakuna unachofanya, chenye mchango kwa wengine unakuwa umeacha kuwa mtu na huwezi kujitofautisha na wanyama.

Unapojisikia uchovu na uvivu kuamka asubuhi, jikumbushe kwamba hata wanyama wanaweza kulala watakavyo siku nzima.
Lakini kinachokutofautisha wewe na wanyama hao ni kazi unayofanya, yenye mchango kwa wengine.
Hivyo amka ukiwa na nguvu na hamasa ya kwenda kuchukua hatua kubwa, kutoa mchango wako kwa wengine kupitia kile unachofanya.

Kila wakati jikumbushe kinachokufanya wewe kuwa mtu na chukua hatua sahihi za kukamikisha utu wako.
Bila ya kazi utu wako haujakamilika.
Bila ya kuwa ya kuwa na mchango kwa wengine, huna tofauti na wanyama, tena wakati mwingine wanyama wana manufaa kama kutoa nyama, mayai, maziwa, ulinzi na kadhalika.

Kuwa mtu, kwa kufanya yake ambayo watu wanapaswa kufanya, kutoa mchango wao kwa wengine kupitia kazi au biashara wanazofanya.
Na pale unapokuwa umekata tamaa au hujisikii kufanya, jikumbushe kuna watu wanakutegemea wewe kwa kile unachofanya.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa mtu kwa kutoa mchango wako kwa wengine, kupitia kazi au biashara unayofanya.
#KuwaMtu #UtuNiKazi #JitumeZaidi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1