“Whenever disturbing news is delivered to you, bear in mind that no news can ever be relevant to your reasoned choice. Can anyone break news to you that your assumptions or desires are wrong? No way! But they can tell you someone died—even so, what is that to you?”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.18.1–2

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu leo,
Tumeipata nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HABARI MPASUKO…
Tunaishi kwenye zama ambazo taarifa zinazoendelea dunia nzima zipo kwenye kiganja chetu.
Hivyo kila wakati kuna habari mpasuko inakufikia,
Watu wameuawa, ajali imetokea, mtu kajiua, mwingine kaua mwenzake, watu wameiba, wengine wamefunguliwa kesi…
Orodha ya habari mpasuko haiwezi kuisha, maana hata maisha binafsi ya watu nayo yamekuwa habari mpasuko.

Habari hizi mpasuko zimekuwa zinapokelewa kwa hisia kali na watu na hivyo kuvuruga saba utulivu wa mtu.
Hebu pata picha umeianza asubuhi yako ya leo kwa habari hizi tano;
1. Watu 20 wamekufa kwenye ajali ya gari.
2. Mtu mmoja amemuua mwenza wake.
3. Viongozi wakubwa watatu wanakabiliwa na mashtaka ya kuima fedha nyingi za serikali.
4. Vitu vinapanda bei kwa kasi.
5. Watu wamefunga biashara zao kwa sababu ya hali ngumu.

Hebu niambie kwa habari hasi kama hizo utapataje nguvu ya kuianza siku yako ukiwa na hamasa kubwa ya kifanikiwa?
Jibu ni huwezi, habari hizo zitaibua hisia kali ndani yako, hisia za hofu, chuki na kukata tamaa.

Hivyo wajibu wetu wa kwanza ni kuhakikisha haturuhusu habari mpasuko zinazoendelea kila dakika kuvuruga utulivu wetu wa ndani.
Ndiyo kuna mtu kamuua mwenza wake, sasa wewe una nini cha kufanya ili kusaidia hilo?
Kuishia tu kusikitika na kusema watu wana roho mbaya haina msaada kwako wala kwa aliyeua au aliyeuawa. Hivyo ni upotevu wa muda wako, nguvu zako na kuvuruga utulivu wako.

Haimaanishi usijali kabisa yale yanayoendelea, bali usiruhusu yakuvuruge kwa namna yoyote ile.
Kama kuna kitu kimetokea na kuna hatua unaweza kuchukua kukifanya kuwa bora zaidi chukua hatua hizo.
Kama hakuna hatua unazoweza kuchukua basi achana na kitu hicho.
Huu ndiyo msimamo pekee utakaokuwezesha kuwa na utulivu kwenye zama hizi za kelele na habari mpasuko zisizo na kikomo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuzuia habari mpasuko zisivuruge utulivu wako na siku yako pia.
#LindaSanaUtulivuWako #UsihangaikeNaHabariMpasuko #HangaikaNaYaliyoNdaniYaUwezoWako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1