Inapokuja kwenye safari ya mafanikio, kwenye kila eneo la maisha yetu, watu wengi wamekuwa wanakwama kwa sababu hawajui wanachofanya au wanachoamini.

Hivyo watu hawa inakuwa rahisi kwao kufanya chochote, hata kama siyo sahihi, kwa sababu tu wanataka kupata kile wanachotaka. Na hapa wanatengeneza mambo ambayo baadaye yanakuwa kikwazo kwao. Kwa sababu unapofanya kitu chochote ambacho siyo sahihi, hakitakuacha salama.

Wengi pia wamekuwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu hakuna wanachosimamia. Wanakuwa kama bendera ambayo inapeperushwa na upepo kwenye kila uelekeo. Wengi wanaanza wakiwa wanataka kitu fulani, lakini wengine wanakuja kwao na maoni tofauti na hapo wanabadilika. Kwa urahisi huo wa kubadilika wanajikuta kila wakati wanaanza na kuacha mambo, kitu ambacho hakiwapi mafanikio makubwa.

Rafiki, mafanikio ya kweli utayapata kwa kujua nini hasa unachotaka na kufanya kile kilicho sahihi katika kupata kitu hicho. Na pia kujua nini unachoamini na kukisimamia hicho wakati wote.

Unapoianza safari yako ya mafanikio dunia haitakuacha salama, kwanza itakuja kwako na vishawishi mbalimbali vya yasiyo sahihi kufanya, usikubali kushawishika. Pia kila mtu atakuwa na maoni yake kwa nini unachoamini na kusimamia siyo sahihi, usipelekeshwe na maoni.

Kama upo ukweli usikilize, lakini siyo maoni, maoni siyo ukweli, maoni ni hisia za watu tu.

Mara zote fanya kilicho sahihi na simamia unachoamini, hutapata mafanikio kwa haraka, lakini utapata mafanikio kwa uhakika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha