“Often injustice lies in what you aren’t doing, not only in what you are doing.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 9.5
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUTOKUFANYA CHOCHOTE…
Kama kuna mambo ambayo siyo sahihi yanafanyika, na wewe ukaamua kutokufanya chochote, maana yake umechangia kwenye mambo hayo kufanyika.
Kama kuna haki inavunjwa, na wewe ukakaa kimya, maana yake umekubaliana na haki hiyo kuvunjwa.
Ubaya siyo tu unafanywa na watu wabaya bali pia unachochewa na watu wema ambao wanachagus kutokufanya chochote.
Na kama alivyowahi kusema Mandela, kama kuna uonevu na wewe ukajiambia haupo upande wowote, maana yake umechagua kukaa upande wa anayeonea na siyo anayeonewa.
Ni wajibu wetu kufanya kilicho sahihi na pia kusimamia kile kilicho sahihi.
Kama kuna kitu kinafanyika na siyo sahihi, tunapaswa kusimama na kukipinga, kwa sababu kukaa kwetu kimya ni kuchochea kitu hicho
Wanasema kukaa kimya maana yake ni kukubaliana na mambo yalivyo.
Hivyo kama kuna kitu ambacho siyo sahihi na hukubaliani nacho, usikae kimya, kisemee.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kilicho sahihi, kusimamia kilicho sahihi na kusema pale ambapo kisicho sahihi kinafanyika.
#FanyaKikichoSahihi #SimamiaKilichoSahihi #UsinyamazieYasiyoSahihi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1