Kama unataka kupika chipsi mayai, lazima kwanza uvunje mayai. Sasa kama unataka kula chipsi na mayai lakini hutaki kuvunja mayai, tayari umeshashindwa kabla hata hujaanza.

Inapokuja kwenye safari ya mafanikio, wapo watu ambao wanataka kufanikiwa, lakini hawataki maisha yao yatikisike.

Yaani wanataka waendelee kuwa na marafiki walionao, waendelee kupata mapumziko wanayopata, waendelee kulala kama ambavyo wamekuwa wanalala na waendelee na starehe ambazo wanazipata kabla hawajafanikiwa.

Hiyo ni sawa na kutaka kula chipsi mayai lakini hutaki kuvunja mayai, kwa kifupi ni kwamba haiwezekani.

Mafanikio yoyote unayoyataka kwenye maisha yako, lazima yatatikisa sana maisha yako. Kama unataka mafanikio makubwa, lazima uwe tayari kwa mtikisiko mkubwa kwenye maisha yako.

Kuna mahusiano yatavunjika, kuna uadui utajengeka, kuna watu watakushambulia na mengine mengi ambayo hukutegemea yatatokea.

Muhimu ni usishangazwe na chochote kinachotokea, badala yake tegemea kitokee na kuwa na maandalizi ya kutosha pale kinapotokea.

Mafanikio makubwa yanakuja na changamoto kubwa, yanakuja na majukumu makubwa. Usijidanganye kwamba utaweza kufanikiwa kwa kuendelea kuishi kama unavyoishi sasa.

Kama unataka kula chipsi mayai, jiandae kuvunja mayai ya kutosha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha