“Indeed, if you find anything in human life better than justice, truth, self-control, courage—in short, anything better than the sufficiency of your own mind, which keeps you acting according to the demands of true reason and accepting what fate gives you outside of your own power of choice—I tell you, if you can see anything better than this, turn to it heart and soul and take full advantage of this greater good you’ve found.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 3.6.1
Ni siku nyingine nzuri, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KAMA KUNA AMBACHO NI BORA ZAIDI…
Tumekuwa tunahangaika na mambo mengi sana, tukiamini mambo hayo ndiyo sahihi kwetu kuwa na maisha bora, yenye utulivu na mafanikio makubwa.
Lakini ni mpaka pale tunapopata kile ambacho tumetafuta sana ndiyo tunagundua ya kwamba kitu hicho siyo muhimu kama tulivyofikiri.
Na hii ndiyo imekuwa sababu ya wengi kutokuishi, wengi wamekuwa wanaahirisha maisha mpaka kifo kinawakuta, wakiwa bado hawajayaishi maisha yao.
Kila wakati kuna kitu wanajiambia wakishakikamilisha basi watakuwa na maisha bora na ya furaha.
Mtu anaanza akiwa shuleni, kwa kujiambia akishahitimu basi atakuwa na maisha ya furaha kwake.
Akihitimu kigezo kinageuka, kinakuwa akishapata kazi ndiyo atakuwa na furaha.
Akipata kazi kigezo kinabadilika, anajiambia akishakuwa na familia basi atakuwa na furaha.
Familia anaipata, kigezo kinabadilika na kuwa akishapata mali fulani.
Mali anazipata na kigezo kinaendelea kubadilika mpaka mtu anapokutwa na mauti.
Rafiki, kuna vitu vinne pekee ambavyo vinakiwezesha wewe kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa popote pale ulipo, bila ya kujali una nini. Vitu hivyo ni;
👉🏼 Haki
👉🏼 Ukweli/Uaminifu
👉🏼 Nidhamu
👉🏼 Ujasiri.
Kwa kuishi maisha yako kwa misingi hiyo minne, yatakuwa bora sana.
Na kama kuna kitu kingine ambacho ni bora zaidi ya vitu hivyo vinne, ambacho kinakupa maisha bora bila ya kujali upo wapi, basi kifanyie kazi.
Lakini kwa tunavyojua mpaka sasa, kwa zaidi ya miaka 2000 imepita na hakujawa na kitu kingine bora zaidi ya vitu hivyo vinne.
Hivyo badala ya kukazana kuja na kitu kipya ambacho kitashindwa, hebu fanyia kazi vitu hivyo vinne ambavyo ni vya uhakika kwa mafanikio yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kwa misingi sahihi ya maisha bora na ya mafanikio.
#Haki #Ukweli #Nidhamu #Ujasiri
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1