Kwa kila unachofanya au kutokufanya kwenye maisha yako, kuna gharama ambayo unailipa. Inawezekana unailipa sasa au ukaja kuilipa baadaye. Ukweli ni kwamba hutaweza kukwepa kulipa gharama.

Ili kufanikiwa lazima ulipe gharama kubwa sasa, lazima ufanye mambo magumu sasa, lazima usamehe baadhi ya starehe kwa sasa, lazima ujisukume na ujiumize, hakuna mafanikio bila ya gharama.

Lakini pia usipofanikiwa, kuna gharama ambayo utailipa, huenda hutailipa sasa, kwa sasa utaendelea na maisha yako kama unavyotaka, ukipumzika utakavyo, ukifanya kile unachojisikia kufanya kwa wakati unaojisikia kufanya. Lakini baadaye utailipa gharama kubwa, kwa kuwa hujaweka msingi sasa, itakulazimu kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu ili kuweza kuendesha maisha yako, au itakubidi uishi kwa kutegemea wengine, kitu ambacho kitakunyanyasa sana.

Rafiki, maisha ni kuchagua, na hakuna unachoweza kukikimbia, ni unachagua sasa au baadaye. Kikombe cha ugumu na mateso hakitakupita, unaweza kukikabili sasa au ukakikwepa na kikaja kukukabili baadaye.

Ukiianza safari yako ya mafanikio mapema, ukiwa bado una nguvu za kutosha, ukajisukuma na kuumia wakati bado una nguvu, utajijengea uhuru mkubwa kwa baadaye. Lakini kama utaikimbia safari hiyo kwa sasa na utafika wakati ambao nguvu ulizonazo huna tena, lakini utalazimika kujituma na kujitesa zaidi.

Ishi maisha yako leo, usiahirishe chochote, kabiliana na kila aina ya ugumu na kwa hakika utafanikiwa na kuwa na maisha bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha