#TANO ZA JUMA #30 2019; Hatujui Kunena, Sanaa Ya Unenaji, Njia 8 Za Kushinda Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Kadamnasi, Kutengeneza Kipato Kupitia Unenaji Na Vitu Viwili Unavyohitaji Ili Watu Wakusikilize.

Karibu rafiki yangu kwenye TANO ZA JUMA hili la 30 la mwaka huu 2019.

Kwenye tano za juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu sanaa ya unenaji, kitu ambacho ni muhimu sana kwa mafanikio yetu.

Ili ufanikiwe, unahitaji kuwashawishi wengine wakubaliane na wewe, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla. Utaweza kuwashawishi wengine kama utaweza kuongea vizuri. Na kitu kimoja ambacho unaweza kuwa hujui mpaka sasa ni kwamba, hujui kuongea. Na kwenye neno la juma hili nitakuonesha kwa nini.

Sanaa hii ya unenaji tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa The Art of Public Speaking ambacho kimeandikwa na waandishi Dale Carnegie na J. Berg Esenwein.

art of public speaking

Kwenye kitabu hiki, waandishi wametushirikisha maarifa na mbinu sahihi za kuweza kuongea mbele ya wengine kwa kujiamini na kwa ushawishi ili tuweze kupata kile tunachotaka na hata kuwanufaisha wengine pia.

Karibu sana ujifunze sanaa ya unenaji, utoke hapa ukiwa na maarifa sahihi ya kukupa kujiamini na ushawishi wa kuongea mbele ya wengine na wakubaliane na wewe.

#1 NENO LA JUMA; HATUJUI KUNENA.

Hiki ni kitu ambacho huenda mpaka sasa hujui, lakini ni ukweli. Katika watu milioni moja, ni mmoja pekee anayejua jinsi ya kunena kwa usahihi. Na ndiyo maana tumekuwa na viongozi wachache sana ambao waliweza kuleta mabadiliko makubwa duniani kupita unenaji.

Kabla hatujaendelea tuwekane sawa kwanza kuhusu kuongea na kunena. Unapoongea na mtu mwingine, hapo unakuwa na maongezi ya kawaida, lakini unapoongea mbele ya watu wengine, hapo unanena. Haijalishi unaoongea nao ni wapi na kuhusu nini, pale tu unapokuwa na zaidi ya mtu mmoja anayekusikiliza hayo siyo mazungumzo tena, bali ni unenaji. Iwe ni nafasi ya kutoa neno la shukrani kwenye shughuli kama sherehe au msiba, iwe unawafundisha wengine, iwe unahubiri, iwe unawashawishi watu kukubaliana na wewe au kununua unachouza na iwe unawaomba watu wakupigie kura, hapo unanena.

Mafanikio yako kwenye kupata kile unachotaka kupitia kuongea na watu wengine yanategemea sana jinsi ambavyo unaweza kunena vizuri.

Lakini kama ninavyokuambia kwenye neno la juma hili, wengi hatujui kunena, tunajua kuongea, kwa kuyatoa maneno kwenye vinywa vyetu, lakini hatujui jinsi ya kuyapangilia maneno hayo vizuri kwa namna ambayo yataleta ushawishi na kuaminika kwa wale ambao tunawalenga.

Na hakuna cha kushangaza kwa nini wengi hatujui kunena, kwa sababu hatujawahi kufundishwa. Tumezaliwa na kuiga wale wanaotuzunguka jinsi wanavyoongea na kuamini hiyo ndiyo njia sahihi.

Tatizo linakuja pale tunapojikuta tunapaswa kuongea mbele ya kundi kubwa la watu. Hapa sasa ndiyo tunagundua kumbe hatujui kunena, tunapatwa na hofu kubwa kama vile watu hao watatuua kwa kuongea mbele yao. Na tafiti zinaonesha, sehemu kubwa ya watu wako radhi wazikwe hai kuliko kuongea mbele ya kundi kubwa la watu.

Na hii yote inatokana na kitu kimoja, hatujui jinsi ya kunena, hatujawahi kufundishwa na sisi wenyewe hatujawahi kuchukua hatua kujifunza.

Wachache baina yetu ambao wameweza kuwa wanenaji wazuri wengi wanakuwa wamezaliwa na vipaji hivyo na kujifunza kwa kujaribu na kukosea. Ni wachache sana ambao wamejitoa kweli kuwa wanenaji bora na kujifunza sanaa ya unenaji.

Umefika wakati sasa wa kuondokana na hali hii ya kutokujua kunena, imetosha sasa kwa fursa nzuri ambazo tumezipoteza za kuwashawishi wengine kupitia mawazo yetu.

Tunapaswa kujifunza sanaa ya unenaji, ili pale tunapopata nafasi ya kuongea mbele ya wengine, basi tuweze kuongea kwa usahihi na kuweza kupata kile ambacho tunakitaka.

Unenaji hauna tofauti kubwa sana na mazungumzo ya kawaida, bali kwenye unenaji unahitaji mtazamo tofauti na ule ambao unakuwa nao unapokuwa unaongea na watu wako wa karibu.

Kwenye kitabu cha juma hili tutajifunza kwa kina sanaa hii ya unenaji na jinsi tunavyoweza kuwa wanenaji wazuri, wenye ushawishi mkubwa na kufanikiwa kupitia unenaji.

Lakini hapa nitakwenda kukupa msingi mkuu wa unenaji, ambao kama hutajifunza chochote zaidi basi ondoka na hiki; mafanikio katika unenaji yanaanza na kujiamini wewe mwenyewe, kuwa na kitu cha kunena na kuweka mbele maslahi ya wale ambao unawanenea. Ukizingatia vitu hivyo vitatu, utaweza kuwa mnenaji mwenye mafanikio makubwa.

WhatsApp Image 2019-07-13 at 19.06.36

#2 KITABU CHA JUMA; SANAA YA UNENAJI.

Dale Carnegie alikuwa ni mmoja wa waalimu bora kabisa kwenye sanaa ya unenaji. Kupitia vitabu vyake na kozi zake za unenaji, watu wengi waliweza kujifunza kwake na kuwa wanenaji wazuri.

Kupitia kitabu cha THE ART OF PUBLIC SPEAKING ambacho alishirikiana na J. Berg Esenwein kukiandika, wametushirikisha mambo yote muhimu tunayopaswa kuyajua kuhusu sanaa ya unenaji na jinsi ya kuwa wanenaji wazuri na wenye mafanikio makubwa.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, ambapo tutajifunza mambo 30 muhimu kuhusu unenaji kama ambavyo yamefundishwa kwenye kitabu cha SANAA YA UNENAJI.

MOJA; ANZA KWA KUJIAMINI.

Ili kuwa mnenaji mzuri lazima uanze kwa kujiamini wewe mwenyewe. Na kujiamini kunatokana na kuwa na maandalizi bora na kuwa na mazoezi ya kutosha katika unenaji. Kitu chochote ambacho unahofia kufanya, hofu hiyo hupotea kadiri unavyofanya kitu hicho. Hivyo kama unahofia kuongea mbele ya wengine, kuwa na maandalizi kisha tafuta nafasi za kuongea mbele ya wengine na ongea mara kwa mara, hofu hiyo itapotea yenyewe.

MBILI; ACHA KUJIFIKIRIA WEWE MWENYEWE.

Unapoongea mbele ya wengine, unapaswa kujisahau wewe na kuwafikiria wale unaoongea nao. Hii ndiyo njia pekee itakayokufanya wewe uongee kwa usahihi na kwa ushawishi. Kama utatumia muda mwingi kujifikiria zaidi wewe, sauti unachoongea kinakosa nguvu na watu hawahamasiki kukusikiliza au kuchukua hatua. Pia badili mfumo wako wa maongezi kwa kuacha kuongea kwa mtindo mmoja wakati wote.

TATU; UFANISI KUPITIA MKAZO.

Katika kuongea kwako, hupaswi kuyapa maneno yote uzito sawa, kwa kufanya hivyo utawachosha watu na hawatajua kipi muhimu cha kuondoka nacho na kwenda kufanyia kazi. Hivyo kama unataka maongezi yako yawe na ufanisi, unapaswa kuweka mkazo kwenye yale maneno muhimu ambayo unataka mtu aondoke nayo na kwenda kufanyia kazi. Unapofika kwenye maneno hayo unayatamka kwa mkazo, kwa sauti ya juu na kwa utaratibu. Hivi ndivyo watu wanavyosikiliza na hata kusoma, kuchagua yale maeneo muhimu ya kufanyia kazi.

NNE; UFANISI KUPITIA KUBADILI SAUTI.

Katika unenaji unaweza kuwa unatumia sauti ya chini, sauti ya kati au sauti ya juu. Kama utatumia sauti ya aina moja katika mazungumzo yako yote watu watakuchoka na kukosa hamasa ya kukusikiliza. Lakini kama utakuwa unabadili sauti kadiri unavyokwenda, unawahamasisha watu kukufuatilia kwa umakini. Unaweza kuwa unaongea kwa sauti ya kati, lakini unapofika kwenye maneno muhimu unabadili na kwenda sauti ya juu au ya chini. Hilo linawafanya watu kujiandaa kupokea pale wanapoona sauti inabadilika.

TANO; UFANISI KUPITIA KUBADILI KASI.

Ukiwa ndani ya gari ambayo inaenda kwa mwendo kasi ambao haubadiliki, unaweza kusahau kama upo kwenye gari, kila kitu kinakwenda sawa. Lakini pale dereva anapoongeza au kupunguza mwendo kwa haraka ndipo unapoona mabadiliko makubwa. Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye unenaji, kama unaenda kwa kasi ya aina moja, watu wanakosa hamasa ya kukusikiliza na wengine watasinzia. Lakini kama utaongeza na kupunguza kasi kadiri unavyokwenda, watu wanakufuatilia vizuri. Mfano unaweza kuwa unaongea kwa haraka, lakini unapofika kwenye maneno muhimu ambayo unataka mtu aelewe na kufanyia kazi, unapunguza kasi yako ya kuongea, hapo mtu anajua yanayofuata ni maneno muhimu.

SITA; NGUVU YA KUSIMAMA.

Kuongea mfululizo bila ya kusimama ni moja ya makosa ambayo wengi wanayafanya na kushindwa kuwa na ushawishi. Unapoongea mbele ya wengine moja ya njia ya kupata nguvu kupitia maongezi yako ni kusimama kwa muda, hasa baada ya kutoa maneno au sentensi ambayo ni muhimu. Unaposimama kwa muda unaipa hadhira yako nafasi ya kuelewa sentensi uliyotoa na pia inakupa wewe mnenaji nafasi ya kutafakari utakachoendelea kusema. Hivyo jifunze kusimama kwa muda kila baada ya kusema kitu muhimu na hilo litaongeza nguvu kwenye mazungumzo yako.

SABA; PANGILIA MANENO YAKO VIZURI.

Watu wawili wanaweza kusema sentensi moja lakini wasikilizaje wakaondoka na maana au hamasa tofauti kulingana na namna mtu amesema sentensi hiyo. Kwa kuanza na jinsi maneno yanavyokuwa yamepangiliwa na msisitizo unaowekwa kwenye kila neno. Jifunze kupangilia maneno yako vizuri ili yaeleweke na kuleta ushawishi kwa wale wanaosikiliza.

NANE; MKAZO KATIKA UWASILISHAJI.

Wanenaji wengi wamekuwa wanakosa wakati wanawasilisha kwa kufikiria kile wanachokwenda kuongea baadaye. Yaani mtu anaongea sentensi hii, lakini mawazo yake yapo kwenye sentensi inayofuata baada ya hiyo. Hili limekuwa linapunguza nguvu ya kile ambacho mtu anakuwa anaongea kwa wakati huo. Ili kuwa na nguvu na ushawishi kupitia unenaji wako, weka nguvu zako zote kwenye ile sentensi unayokuwa unaongea. Mawazo yako yote yanapaswa kuwa kwenye sentensi hiyo, hilo linaipa nguvu na hata hadhira yako itaweka nguvu kwenye sentensi hiyo. Unapokuwa unaongea mbele ya wengine, usifikirie kitu kingine chochote bali kile tu unachozungumza. Wacha mazungumzo yaende yenyewe na utakuwa na unenaji bora sana kuliko kufikiria kile unachokwenda kusema baada ya kumaliza unachosema sasa.

TISA; NGUVU.

Ili kile unachoongea kiweze kueleweka na kuwa na ushawishi kwa wengine, kinapaswa kuwa na nguvu ndani yake. Wengi wanashindwa kwenye unenaji kwa sababu wanashindwa kuweka nguvu kwenye kile ambacho wanazungumza. Ili kuweka nguvu kwenye kile unachozungumza zingatia yafuatayo;

 1. Hakikisha unachoongea ni ukweli.
 2. Amini bila ya shaka yoyote kwenye kile unachoongea.
 3. Anza maongezi kwa maneno yanayovuta umakini wa watu na maliza kwa maneno yanayoonesha utofauti.
 4. Ongea kwa mamlaka, na siyo kwa kupendekeza au kama unatoa maoni.
 5. Tamka maneno yako kama kauli ya mwisho, kwamba hakuna tena ukweli zaidi ya huo.

Kama huwezi kuongea kwa kujiamini na kwa uhakika, ni bora kukaa kimya.

KUMI; HISIA NA HAMASA.

Binadamu ni viumbe wa hisia kuliko fikra. Huwa tunadhani tunafanya maamuzi yetu kwa kufikiri, lakini ukweli ni kwamba tunafanya maamuzi kwa hisia, halafu baadaye tunayahalalisha kwa kufikiri. Hivyo ili unenaji wako uwe na ushawishi, unapaswa kugusa hisia za wale unaoongea nao. Kama maongezi yako hayagusi hisia, huwezi kumhamasisha yeyote. Na njia bora ya kugusa hisia za wengine kwenye unenaji ni kuweka maslahi ya watu hao mbele, kugusa yale maeneo wanayoyajali zaidi. Weka hisia kwenye unenaji wako, kwa kujali zaidi kuhusu wale unaozungumza nao na hilo litawapa hamasa ya kuchukua hatua.

KUMI NA MOJA; UFASAHA KUPITIA MAANDALIZI.

Ufasaha wako kwenye kile unachozungumzia unatokana na maandalizi ambayo unayo. Maandalizi yanaanzia kwenye ujuzi na uzoefu ulionao kuhusu kitu hicho na namna ambavyo unakwenda kukisema kwa wengine. Unapaswa kuwa na maandalizi mazuri kabla ya kusimama na kuongea mbele ya wengine. Unahitaji kujua kwa hakika kile unachokwenda kukizungumzia na pia unapaswa kuwa na maandalizi ya namna utakavyokisema, maeneo ya kuweka mkazo na hatua ambazo unataka watu wachukue. Wanenaji wenye mafanikio makubwa huwa wanafanya maandalizi mazuri, na hata muda mfupi kabla ya kuongea, huwa wanafanya mazoezi ya jinsi watakavyoongea kile walichoandaa. Maandalizi yanahitaji kazi na kujifuatilia ili kukazana kuwa bora kila wakati. Na hivyo ndivyo mafanikio kwenye jambo lolote yanavyopatikana.

KUMI NA MBILI; SAUTI.

Sauti ni kiungo muhimu sana kwenye unenaji, unaweza kuwa na maandalizi mazuri lakini sauti yako ikakuangusha kama hujajipanga vizuri. Unapaswa kuwa na sauti ambayo inasikika vizuri na wale unaoongea nao, isiwe ya kelele sana na wala isiwe ya chini sana. Sauti yako inapokuwa sahihi, maongezi yako yanakwenda vizuri.

Hapa kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili kuwa na sauti sahihi wakati wa maongezi.

 1. Usijaribu kulazimisha sauti yako pale inapokuwa inakwaruza, hapo unazidisha tatizo.
 2. Usinywe kinywaji cha baridi wakati unaongea.
 3. Epuka kuanza maongezi na sauti ya juu sana. Unapogundua sauti ipo juu, ishushe.
 4. Pumua vizuri na kwa kina wakati unazungumza, ukiishiwa pumzi sauti haitatoka.
 5. Usijisikilize wakati unaongea, kumbuka fikra zako zote zinapaswa kuwa kwenye kile unachozungumzia na siyo jinsi unavyokizungumzia.

KUMI NA TATU; SAUTI YA UCHESHI.

Jinsi unavyotoa sauti yako kunaathiri nguvu na ushawishi wa mazungumzo yako. Sauti inaweza kutoka kwa huzuni au kwa furaha. Jifunze kutoa sauti ambayo ina furaha na ucheshi ndani yake na hilo litawahamasisha wale wanaosikiliza.

KUMI NA NNE; UTOFAUTI NA USAHIHI WA MATAMSHI.

Matamshi yako yanaathiri sana jinsi ambavyo watu wanapokea kile unachosema. Unapaswa kutamka maneno kwa usahihi kuanzia kwenye silabi zake na hata sauti yake. Hapa kuna changamoto ya mazoea ambapo watu hukosea matamshi ya baadhi ya maneno, mfano badala ya neno HARAKA mtu anasema HALAKA. Unapaswa kutumia maneno na matamshi sahihi ili watu waweze kukuchukulia kama mtu unayeelewa kile unachozungumza na hivyo kukuamini na kushawishika.

KUMI NA TANO; ISHARA ZA MWILI.

Unapokuwa unaongea, kuna ishara ambazo mwili wako huwa unaonesha, hasa kwenye mikono, miguu na hata kichwa. Tatizo la ishara hizi zinaweza kukosekana kabisa na hivyo mtu akawa kama sanamu lililosimama na kuongea au zikazidi na mtu akaonekana kama mwenye wasiwasi na asiyejua anachoongea. Ishara za mwili ni matokeo ya kile ambacho kinaendelea ndani ya mtu. Mtu anapokuwa amejipanga vizuri kwenye kile anachoongea, anakuwa na kiasi sahihi cha ishara za mwili. Lakini anapokuwa hajajipanga vizuri, atakosa kabisa ishara za mwili au zitakuwa nyingi kupitiliza. Ishara za mwili unazoonesha hazipaswi kuwafanya watu waache kufuatilia unachozungumza na kuanza kufuatilia ishara hizo za mwili. Na kama ambavyo tumejifunza, weka mawazo yako yote kwenye kile unachozungumzia na hayo mengine yatakaa sawa yenyewe.

KUMI NA SITA; NJIA ZA KUWASILISHA UNENAJI.

Zipo njia nne za kuwasilisha unenaji kwa hadhira yako.

 1. Kusoma hotuba, njia hii inaleta usahihi kwenye kile ambacho umeandaa, lakini inaondoa ile ladha ya unenaji. Kwa sababu unaposoma hakuna kipya unachoongeza.
 2. Kusoma na kuongezea maelezo zaidi, hapa unaandika hotuba ambayo utaisoma, lakini katika kuisoma kuna maelezo zaidi ambayo utayaongeza kama ufafanuzi. Hili linahitaji muda mwingi wa kutoa unenaji wako.
 3. Kuongea kutoka kwenye maandishi. Hapa unakuwa umeandika kile unachokwenda kuzungumzia, kisha kukielezea kwa kina zaidi. Hii ni njia inayotumika na waalimu au wahadhiri, ambao wanakuwa wameandaa maelezo ya kile wanachozungumzia na kisha kuyazungumzia hayo.
 4. kuongea kutoka kichwani. Hapa mnenaji anakuwa hana maandishi au maelezo yoyote anayoyafuata, bali anaongea moja kwa moja kutoka kwenye mawazo yake. Aina hii ya uwasilishaji huwa ina nguvu sana, lakini inahitaji maandalizi makubwa, wakati mwingine mtu kukariri mazungumzo yake yote kisha kuyatoa kama yalivyo kutoka kwenye mawazo yake.

Kwa kuanza, anza na ile njia ambayo inakufaa kwa sasa, kisha endelea kuboresha zaidi. Mfano unaweza kuanza na njia ya kusoma na kufafanua au njia ya kuwa na maelezo yaliyoandaliwa kwa maandishi na kuyafafanua zaidi. Lakini lengo ni kufika kwenye hatua ya kuweza kuongea kutoka kichwani bila ya kusoma au kufuata popote. Hii ndiyo njia bora ya kuwa na ushawishi kupitia unenaji wako.

KUMI NA SABA; NGUVU YA AKIBA KIFIKRA.

Unapokuwa mbele ya wengine kwa ajili ya kuzungumza, unapaswa kuwa na akiba kifikra, yaani uwe na maandalizi ya kutosha kiasi kwamba huwezi kuishiwa kitu cha kusema. Kwa chochote unachozungumzia, kuwa na uelewa wa kutosha na mifano ya kutosha kiasi kwamba unapoanza kuongea unafikiri akile unachoongea na ukimaliza tayari kuna kingine kimeshakuja kwa ajili ya kuongea. Unapokosa maandalizi ya kutosha, unakuwa huna akiba na hivyo kile unachoongea kinapoisha unajikuta huna kingine cha kuongea na hapo ndipo unapoanza kuongea vitu visivyo husika na kuharibu kabisa mazungumzo yako. Kwenye lile eneo unalozungumzia unapaswa kuwa chemchem isiyokauka, mara zote inatiririsha mawazo mazuri kuhusu eneo hilo.

KUMI NA NANE; MADA NA MAANDALIZI.

Unapaswa kuchagua mada unayozungumzia, ambayo utafanya maandalizi ya kutosha ili unaponena mbele ya wengine waweze kunufaika.

Zipo njia mbili za kuchagua mada yako ya kuzungumzia.

 1. Kuchagua kiholela, hapa unachagua chochote na kukizungumzia. Unaweza kuchagua mwenyewe au kuwaomba wengine wakuchagulie.
 2. Mada kuanzia ndani yako, hapa kuna kitu kinakuwa ndani yako, kitu ambacho unapenda kukifuatilia, au unakijua au kuwa na uzoefu nacho. Hapa unaendelea kile ambacho tayari unacho.

Njia bora ya kuchagua mada yako ni kuanzia ndani yako, kwa sababu hapo unaanza na kitu ambacho tayari unakijali na hivyo utaweza kuweka maandalizi ya kutosha.

Ukishachagua mada yako, unapaswa kuweka muda wa kufanya maandalizi. Unapaswa kujifunza kupitia vitabu, kupitia watu wengine, kupitia mazingira na kadhalika. Tenga muda wa kujifunza kuhusu mada yako na pia kujifunza jinsi ya kuwasilisha mada hiyo kwa wengine.

Maswali muhimu ya kujiuliza na kujipa majibu wakati wa kuandaa mada yako;

 1. Ni tukio la aina gani unalokwenda kuzungumza?
 2. Ni watu wengi kiasi gani watakaohudhuria?
 3. Watu hao wanatokea kwenye maisha ya aina gani?
 4. Ni watu gani wengine wataongea kwenye tukio hilo?
 5. Ni muda kiasi gani nimepewa wa kuzungumza?

Jipe majibu ya maswali hayo ili uweze kuwa na maandalizi sahihi ya mazungumzo yako.

KUMI NA TISA; USHAWISHI KUPITIA UFAFANUZI.

Ili watu waweze kuelewa vizuri kile unachozungumzia, unapaswa kutoa ufafanuzi wa jumla wa mada yako. Hapa unawapa watu picha kubwa ya kile unachozungumzia, kwa namba ambayo wataelewa dhana nzima ya mada yako. Ufafanuzi ni wa jumla na unamfanya mtu kuwa upande mmoja na wewe kupitia mada yako. ufafanuzi wa kina unautoa kwenye maelezo kama utakavyojifunza hapo chini.

ISHIRINI; USHAWISHI KUPITIA MAELEZO.

Baada ya kuwapa watu ufafanuzi, sasa unahitaji kuwapa maelezo ya kina kwenye kile unachozungumzia. Kwenye ufafanuzi uliwapa picha kubwa ya kile unachozungumzia, kwenye maelezo unakwenda ndani zaidi kuzungumzia kile hasa kilichopo ndani. Wazungumzaji wengi wamekuwa wanaanza kuwapa watu maelezo kabla ya kuwapa ufafanuzi, kitu ambacho kinafanya mada yao kuwa ngumu kueleweka. Wafanye watu waielewe mada kwa ujumla kwanza kabla hujaingia kufafanua kila kilichopo ndani.

Rafiki, kama nilivyokuambia, kuna mambo 30 ya kujifunza na kufanyia kazi kwenye kitabu hiki cha SANAA YA UNENI, hapa tutaishia kwenye mambo haya 20, mambo kumi ambayo yanakamilisha yale 30 utayapata kwenye #MAKINIKIA ya juma ambayo yatapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Jinsi ya kujiunga na mtandao huo soma mwisho wa makala hii.

Mambo kumi utakayokwenda kujifunza ni; USHAWISHI KUPITIA SIMULIZI, USHAWISHI KUPITIA MAPENDEKEZO, USHAWISHI KUPITIA HOJA, UHAWISHI KUPITIA MVUTO, USHAWISHI KUPITIA KUNDI, USHAWISHI KUPITIA TASWIRA, KUKUZA MISAMIATI YAKO, KUKUZA KUMBUKUMBU, KUTENGENEZA HAIBA BORA NA MAONGEZI KWENYE MATUKIO MBALIMBALI.

Kujifunza haya karibu kwenye channel ya tano za juma kwenye mtandao wa telegram.

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.49

#3 MAKALA YA JUMA; NJIA 8 ZA KUSHINDA HOFU YA KUONGEA MBELE YA KADAMNASI.

Kuongea mbele ya wengine ni moja ya vitu vinavyowatisha watu wengi mno. Haijalishi ukubwa wa watu, mtu anapojikuta kwenye hali ambayo inambidi aongee mbele ya kundi kubwa la watu, hofu huwa inamtawala na kujikuta akisahau alitaka kuongea nini au kuongea kwa namna ambayo watu wanaomsikiliza wanasinzia kabisa.

Kama ambavyo nimeshakuambia na nitaendelea kukuambia tena, mafanikio yako yanategemea zaidi ushawishi wako, na ushawishi wako ni matokeo ya namna unavyoweza kuongea mbele ya watu kwa kujiamini na kwa ushawishi.

Kwenye makala ya juma hili tumejifunza njia nane za kujijengea kujiamini na kuishinda hofu ya kuongea mbele ya wengine. Unapaswa kuzijua njia hizi nane na kuzifanyia kazi kama unataka kupiga hatua kwenye maisha yako.

Zisome njia hizo nane hapa; Njia Nane (8) Za Kujijengea Kujiamini Na Kuishinda Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Kundi Kubwa La Watu.

Kila siku endelea kutembelea mtandao wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA ujifunze na kuhamasika kisha kuchukua hatua na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#4 TUONGEE PESA; KUTENGENEZA KIPATO KUPITIA UNENAJI.

Kitu kimoja ninachoweza kukuambia wewe rafiki yangu ni hiki, sehemu kubwa ya kipato chako inategemea unenaji wako. Hii ina maana kwamba kama wewe ni mnenaji mzuri basi utakuwa na kipato kikubwa. Na kwa upande mwingine, kama kipato chako kipo chini, basi unenaji wako unaweza kuwa ni moja ya vitu vinachangia kipato hicho kuwa chini. Hivyo kama utaboresha unenaji wako, utaongeza kipato chako.

Nimekuwa nakuambia kitu kimoja, kwamba kila mmoja wetu kuna kitu anauza. Kama umeajiriwa unauza muda wako, utaalamu wako na hata uzoefu wako kwa mwajiri wako. Kadiri unavyoweza kumshawishi mwajiri wako kuhusu kile unachoweza kumsaidia, ndivyo unavyoweza kupata nafasi za kufanya zaidi na hatimaye kuongeza kipato chako zaidi. Utaweza kuwa na ushawishi mzuri kama utakuwa mnenaji mzuri.

Kama umejiajiri au unafanya biashara, unahitaji kuwashawishi watu wengine wanunue bidhaa au huduma unazotoa. Sasa haijalishi una bidhaa au huduma bora kiasi gani, kama huna ushawishi mkubwa kwenye kile unachouza, hakuna atakayenunua. Na tena kwa zama hizi za kelele, zama ambazo watu wapo ‘bize’ na ‘wamevurugwa’ kweli kweli, kama huna ushawishi, hutapata watu wakununua unachouza. Kuwa mnenaji mzuri kutakusaidia kuwa na ushawishi mkubwa kwa wale unawalenga na wakaweza kununua. Jinsi unavyojiamini na kuamini kwenye kile unachouza, na kisha kuyajua mahitaji halisi ya wateja wako na kuweza kuwaeleza vizuri kuhusu kitu hicho na kinavyoweza kuwasaidia, utawashawishi wengi kununua kwako.

Tunaona wazi jinsi unenaji ulivyo muhimu kwenye kutengeneza kipato. Hivyo tunaweza kujumuisha kwa kusema zipo njia mbili za kutengeneza kipato kupitia unenaji.

Njia ya kwanza ni kuboresha unenaji wako kupitia kazi au biashara unayofanya, kujua vizuri kile unachofanya, na kuwa na njia bora ya kukielezea kwa wengine, kwa namna ambayo itagusa hisia zao na kuwasukuma kuchukua hatua. Kila mmoja wetu kupitia anachofanya kuna namna anaweza kuwashawishi wengine na wakampa kazi zaidi, biashara zaidi au fursa zaidi. Kaa chini na uangalie kazi au biashara unayofanya sasa, ni wapi ukiweka unenaji mzuri utatengeneza ushawishi mkubwa zaidi na anza kuchukua hatua.

Njia ya pili ni kupitia unenaji wenyewe. Hapa unalipwa kunena. Na tunaona kila siku waendesha shughuli mbalimbali (MC) wanavyoongezeka. Pia walimu, wahadhiri na wahamasishaji mbalimbali wamekuwa wanalipwa kupitia unenaji wao. Wale wanaofanikiwa sana kwenye eneo hili, ni wale ambao unenaji wao una ushawishi mkubwa kwa wale wanaosikiliza na wale wanaoweza kuwasukuma watu kuchukua hatua sahihi. Hivyo kama kuna eneo ambalo unalijua vizuri na unaona wengine wanaweza kunufaika kupitia ujuzi na uzoefu wako, ingia kwenye tasnia ya unenaji. Jifunze kuwa mnenaji mzuri kwa kuanza na haya tuliyojifunza hapa na kufanyia kazi huku ukiendelea kujifunza zaidi. Kisha omba nafasi za kunena kwenye maeneo madogo na kisha kwenye maeneo makubwa na baada ya muda utakuta watu wanakuhitaji unene kwenye shughuli zao mbalimbali na watakulipa.

Rafiki, kwa vyovyote vile, utaongeza kipato chako kwa kuwa mnenaji mzuri. Hebu jifunze sasa unenaji, fanyia mazoezi na ona kipato chako kikiongezeka zaidi na zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; VITU VIWILI UNAVYOHITAJI ILI WATU WAKUSIKILIZE.

“There is only one excuse for a speaker’s asking the attention of his audience: he must have either truth or entertainment for them.” ― Dale Carnegie

Kama unataka watu wakusikilize unapoongea, unapaswa kuwa na moja au vyote kati ya vitu hivi viwili; ukweli au burudani.

Watu wanapenda kusikiliza ukweli, ukweli ambao unawawezesha kufanya maamuzi sahihi na kupiga hatua kwenye maisha yao, ukweli unaowafanya waone wapi walikuwa wanakosea na hatua sahihi za kuchukua ni zipi. Unapokuwa na ukweli, watu wanakusikiliza, hasa pale unapokuwa na ushahidi wa ukweli huo. Japokuwa wakati mwingine ukweli huwa unaumiza na watu wengi kuukataa, lakini unapousimamia unapata watu wa kukusikiliza. Hii ndiyo inayosababisha tunawasikiliza waalimu, washauri, au viongozi mbalimbali, ambao tunajua wana ukweli ambao tunauhitaji.

Watu wanapenda burudani, watu wanapenda kusahau changamoto zao za maisha kwa muda na kucheka kidogo. Na hapa ndipo wasanii na wachekeshaji wanapopata nafasi ya kuwafikia wengine kupitia sanaa zao. Watu watamsikiliza mtu kama wanaburudika kwa kumsikiliza.

Hivyo rafiki, kama unataka kuwa mnenaji mzuri, kazana kuweka vitu hivi viwili kwenye unenaji wako, ukweli na burudani. Kila unapopata nafasi ya kuongea mbele ya wengine, jua ni ukweli gani ambao unataka watu hao wajue, labda kuhusu wewe, kuhusu mada unayozungumzia au kuhusu bidhaa au huduma unayotaka kuwauzia. Ukweli huu uwafanye waondoke na kitu ambacho hawakuwa wanakijua awali na wawe na hatua za kuchukua ambazo hawakuwa wanachukua awali. Pia waburudishe watu kupitia unenaji wako, kuwa na hadithi, mifano au visa ambavyo vinaufukisha ukweli huo kwa njia ambayo inawaburudisha watu. Unahitaji kuwa na maandalizi ya mifano au hadithi utakazotumia kwenye unenaji wako, ambavyo vitafikisha ukweli na kuwaburudisha watu pia.

Zingatia vitu hivyo viwili katika unenaji, ukweli na burudani na watu watapenda kukusikiliza kila wakati bila ya kuchoka.

Rafiki, ni imani yangu kwamba TANO ZA JUMA hili zimekupa mwanga mkubwa kuhusu umuhimu wa kuwa mnenaji na njia bora za wewe kujifunza unenaji ili uweze kuongeza ushawishi wako, kukuza kipato chako na kufikia mafanikio makubwa. Sasa kazi ni kwako kuyaweka haya uliyojifunza kwenye matendo na pia kuendelea kujifunza zaidi kuhusu unenaji ili uwe bora zaidi eneo hilo na uweze kupiga hatua kwenye maisha yako.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili tunakwenda kujifunza mambo kumi katika yale 30 ya kujifunza kwenye sanaa ya unenaji. Maelezo ya kujiunga na channel ya TANO ZA JUMA yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu