#TANO ZA JUMA #32 2019; Uuzaji Umebadilika, Kuuza Ni Ubinadamu, Maeneo Matatu Ya Kuzingatia Ili Kuwa Na Ushawishi Zaidi, Kama Unataka Pesa Uza Zaidi Na Elimu Ya Darasani Inapokwama.

Hongera sana rafiki kwa kumaliza juma la 32 la mwaka huu 2019. Mwaka tuliouita mpya siku siyo nyingi unazidi kutuacha. Imani yangu ni kwamba unapiga hatua kadiri muda unavyozidi kwenda. Maana hilo ndiyo jambo muhimu zaidi.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA la 32 ambapo tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu uuzaji. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia kwenye tano za majuma yaliyopita, kuna maeneo matatu muhimu sana ambayo nashauri kila mmoja wetu aweke nguvu kubwa na ataweza kufanikiwa zaidi.

Eneo la kwanza ni UUZAJI, kama tunavyojua, kila mmoja wetu ni muuzaji, iwe umeajiriwa au umejiajiri, kuna kitu ambacho unauza. Kadiri unavyoweza kuuza kwa ubora, ndivyo utakavyofanikiwa zaidi. Kwenye tano za juma hili tutajifunza zaidi kuhusu uuzaji.

Eneo la pili ni UNENAJI, kwa kuwa kila mtu anauza, na kwa kuwa tunachouza tunataka wengine wakinunue, tutaweza kuuza zaidi kama tunaweza kunena vizuri. Hivyo kila mmoja wetu ni muhimu ajifunze na kuwa mnenaji mzuri. Ni kupitia unenaji ndiyo unaweza kuwashawishi watu kununua unachouza. Kwenye tano za juma la 30 nilikushirikisha kwa kina kuhusu unenaji, soma zaidi kwa kubonyeza maandishi haya.

Eneo la tatu ni UANDISHI, njia nyingine ya kupata ushawishi kwa chochote unachouza ni kupitia uandishi. Iwe unaandika barua, ujumbe wa simu, barua pepe, makala, tangazo au chochote, zipo mbinu za kuleta ushawishi zaidi kupitia uandishi. Unapaswa kujifunza na kuwa mwandishi bora ili uweze kuwa na ushawishi kwa wengine. Kwenye juma la 31 tumeifunza kwa kina kuhusu uandishi, unaweza kusoma zaidi kwa kubonyeza maandishi haya.

Juma hili la 32 tunakwenda kujifunza kuhusu uuzaji kutoka kitabu kinachoitwa To Sell Is Human: The Surprising Truth About Moving Others kilichoandikwa na Daniel H. Pink.

to sell is human.jpg

Kwenye kitabu hiki, mwandishi anatuonesha kwamba kila mtu sasa yupo kwenye mauzo na kwamba mauzo kwa sasa yamebadilika sana. Anatushirikisha misingi mipya ya kufanikiwa kwenye uuzaji pamoja na mbinu sahihi za kupata ushawishi kwa wengine.

Karibu sana tujifunze ili tuweze kuwa wauzaji bora katika zama hizi ambapo uuzaji umebadilika sana.

#1 NENO LA JUMA; UUZAJI UMEBADILIKA.

Rafiki, uuzaji umebadilika, siyo kidogo, bali sana. Wale ambao hawajifunzi na kubadilika, wanapata taabu sana kwenye zama hizi mpya.

Zamani wauzaji walikuwa kama miungu watu, kwa sababu walikuwa wana taarifa nyingi kuhusu kile wanachouza kuliko mnunuaji. Hivyo waliweza kuamua ni kiasi gani wamweleze mteja kuhusu kile wanachouza na waliweza kudanganya, kuongeza chumvi au kuondoa baadhi ya taarifa ambazo mteja akizijua asingeweza kununua. Hali hii iliwapa nafasi ya kuuza zaidi kwa wateja wasiokuwa na taarifa za kutosha.

Zamani pia wauzaji walikuwa wachache, hivyo mteja alilazimika kukubaliana na yule anayemuuzia na hakuwa na njia ya kulinganisha ubora au bei baina ya wauzaji wengi.

Kwa sasa mambo yamebadilika, kwanza hakuna tena utofauti wa taarifa. Wateja kwa sasa wana taarifa nyingi, tena wakati mwingine kuliko hata muuzaji. Taarifa zinapatikana kwa urahisi kupitia mtandao wa intaneti, hivyo kabla mteja hajaenda kutafuta anachotaka, anaingia mtandaoni kwanza kusaka taarifa na maarifa. Hivyo mpaka anafika kwa muuzaji, tayari anajua vitu vingi kuhusu kile anachotaka.

Pili, wauzaji ni wengi, hivyo mteja ana wigo mpana wa kuongea na watu wengi na kulinganisha ubora na bei kabla hajafanya maamuzi ya kununua. Wakati mwingine mteja hahitaji hata kutoka nyumbani kwake, analinganisha bei mtandaoni, anaagiza na kuletewa kile anachotaka.

Mabadiliko haya makubwa yanaonekana kufuta kabisa nafasi ya wauzaji, lakini kama tunavyoona kwamba kila mtu anauza, basi uuzaji siyo tu kwamba haujafutwa, bali umefanya kuwa imara zaidi.

Wale wanaotaka kufanikiwa kwenye uuzaji kwa zama hizi, lazima wayajue mabadiliko yanayoendelea na wabadilike pia. Lazima wajifunze misingi mipya ya uuzaji na kuisimamia. Lazima wajijengee tabia na sifa nzuri na kuziishi hizo ili wateja wao wawe na imani kwao.

Kwenye kitabu cha juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina mabadiliko haya yanayoendelea na misingi mipya ya kujijengea kwenye uuzaji. Karibu sana tujifunze ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanikiwa sana kwenye maisha yako.

#2 KITABU CHA JUMA; KUUZA NI UBINADAMU.

Kuuza ni ubinadamu kwa sababu kila mmoja wetu anategemea kitu fulani kutoka kwa mwenzake ili kupiga hatua kwenye maisha yake. Unaweza kupata kile unachotaka kutoka kwa wengine kama utaweza kuwa na ushawishi mzuri kwao. Na ili kuwa na ushawishi, ni lazima ujue mbinu na misingi sahihi ya mauzo.

Kwenye kitabu cha To Sell Is Human: The Surprising Truth About Moving Others mwandishi Daniel H. Pink anatupa mbinu na mikakati sahihi ya kufanikiwa kwenye mauzo katika zama hizi ambapo mambo mengi yamebadilika. Kama ambavyo tumeona kwenye neno la juma hapo juu, mabadiliko ya kiteknolojia yamebadili sana eneo la mauzo. Kwa sasa muuzaji hawezi tena kumdanganya mnunuaji ili kumuuzia kitu, kwa sababu taarifa zinapatikana kwa urahisi.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu, ujifunze mbinu na mikakati sahihi ya kufanikiwa kwenye mauzo, kupitia kile ambacho unafanya.

MOJA; WOTE TUPO KWENYE MAUZO.

Hii ni kauli ambayo umeshaisikia mara nyingi kutoka kwangu, ni kauli ambayo mwandishi ameanza nayo kama sura ya kwanza ya kitabu hiki cha To Sell Is Human. Mwandishi anatuambia takwimu za nchini Marekani ambazo pia zinaakisi dunia kwa ujumla, zinaonesha mtu mmoja kati ya watu tisa anaingiza kipato chake moja kwa moja kupitia mauzo. Lakini ukiangalia zaidi takwimu hizo, hata wale watu nane ambao hawaonekani kutegemea mauzo moja kwa moja kuingiza kipato, bado pia wapo kwenye mauzo.

Mwandishi anasema utajijua kama upo kwenye mauzo kama kazi au biashara unayofanya inakuhusisha kuwashawishi wengine kuchukua hatua fulani.

Kama ulikuwa bado hujakubali uko kwenye mauzo, basi leo ni siku ya kufanya hivyo. Cha kufanya chagua wiki moja iliyopita, kisha orodhesha kila kitu ambacho umekifanya kwa juma zima. Andika kila ulichofanya, kila uliyeongea naye, kila ujumbe uliotuma na kadhalika. Kisha fanya tathmini, ni yapi kati ya uliyofanya yanahusisha kuwashawishi wengine kuchukua hatua fulani. Kama yapo unayofanya yanayohusisha wengine, basi upo kwenye mauzo. Na kama upo kwenye mauzo, basi ni vyema kujifunza mbinu na mikakati sahihi ya mauzo.

MBILI; UJASIRIAMALI NA MAUZO.

Moja ya vitu vilivyofanya watu wengi kuwa kwenye mauzo ni ukuaji wa ujasiriamali. Kwa sasa watu wengi wamejiingiza kwenye ujasiriamali, wakianza biashara zao ndogo ndogo na kuziendesha wao wenyewe au wakiwa na wasaidizi wachache.

Unapoingia kwenye ujasiriamali kwa hatua ndogo, wewe ndiyo unakuwa kila kitu kwenye biashara yako, huna watu ambao unawaajiri kwa vitengo maalumu, yaani labda kuwa na timu ya mauzo na kadhalika. Hivyo unakuwa ndiyo mtu wa masoko, mtu wa mauzo, mtu wa fedha na kadhalika.

Kama upo kwenye ujasiriamali au biashara ndogo yoyote, wewe ni muuzaji na hivyo jifunze mbinu sahihi za mauzo.

TATU; MABADILIKO NA MAUZO.

Kipindi cha nyuma, makampuni makubwa yalikuwa yana vitengo ambavyo vilikuwa inaendeshwa na watu wanaobobea kwenye vitengo hivyo tu. Kunakuwa na kitengo cha mauzo ambazo kinafanya kazi ya mauzo pekee na kitengo cha masoko ambacho kinafanya masoko pekee. Kadhalika vitengo vingine muhimu.

Lakini kwa sasa mabadiliko makubwa yanayotokea, yanamfanya kila mtu kwenye biashara kuhusika na vitengo mbalimbali. Ile hali ya kuwa kwenye kitengo kimoja pekee haipo tena. Na vitengo kama mauzo na masoko, hivi vinamtaka kila mtu kwenye kampuni au biashara avielewe. Hivyo hata kama umeajiriwa kwenye taasisi kubwa, wewe ni mtu wa mauzo, na kadiri unavyokuwa bora kwenye mauzo, ndivyo unavyofanikiwa zaidi.

NNE; UKUAJI WA SEKTA YA ELIMU NA AFYA.

Mwandishi anatuambia sekta ya ELIMU NA AFYA ndiyo sekta pekee ambayo inakua kwa kasi sana duniani. Sekta hii inatoa fursa nyingi za kibiashara na hata nafasi nyingi za kazi. Sekta hii inahusisha mambo yote yanayoingia kwenye elimu, kuanzia elimu rasmi na isiyo rasmi, na kwenye afya, kuanzia afya ya kitaalamu na hata afya mbadala.

Ukuaji na hata kufanikiwa kwenye sekta hii kunategemea sana mauzo. Mwalimu anaweza kufanikiwa kama anaweza kuwashawishi wale anaowafundisha na wakaelewa anachowafundisha. Kadhalika daktari anafanikiwa kama anaweza kumshawishi mgonjwa kuchukua hatua sahihi za kujenga na kuboresha afya yake.

Kama upo kwenye sekta hizo mbili, elimu na afya, iwe ni kwenye mfumo rasmi au siyo rasmi, mafanikio yako yanategemea zaidi uuzaji. Jifunze mbinu bora za mauzo na utaweza kupiga hatua zaidi.

MASWALI MANNE YA KUJITATHMINI KAMA UPO KWENYE MAUZO AU LA.

Hapo juu tumeona jinsi ya kujitathmini kama upo kwenye mauzo, hapa kuna maswali manne ambayo yatakuonesha kama upo kwenye mauzo au la.

Jiulize na kujipa majibu ya maswali haya manne na utaweza kujua upo upande gani;

  1. Je unaingiza kipato chako kupitia kuwashawishi wengine kununua bidhaa au huduma ulizonazo? Kama jibu ni ndiyo upo kwenye mauzo, kama jibu ni hapana nenda swali la 2.
  2. Je umejiajiri au unaendesha biashara yako mwenyewe, hata kama ni pembeni ya ajira yako? Kama jibu ni ndiyo upo kwenye mauzo, kama jibu ni hapana nenda swali la 3.
  3. Je kazi unayofanya inakutaka kujihusisha na vitengo mbalimbali au kufanya majukumu tofauti tofauti? Kama jibu ni ndiyo upo kwenye mauzo, kama ni hapana nenda swali la 4.
  4. Je unafanya kazi kwenye sekta ya elimu au afya? Kama jibu ni ndiyo upo kwenye mauzo, kama ni hapana na namba 1 mpaka tatu hapo juu ni hapana basi haupo kwenye mauzo.

Mpaka kufika hapa nina imani ni dhahiri kwako kwamba upo kwenye mauzo, sasa twende tukajifunze mbinu sahihi za kufanikiwa kwenye mauzo.

Sehemu ya kuanzia ni maeneo matatu muhimu ya kugusa ili kuweza kuwashawishi wateja kununua. Maeneo hayo matatu yanapatikana kwenye makala ya juma, angalia kipengele namba tatu hapo chini.

TANO; MUUZAJI KUWA MAKINI.

Kipindi cha nyuma, tahadhari ilikuwa inatolewa kwa wanunuaji kwamba wawe makini. Tahadhari ilieleza wazi kwamba kama mnunuaji hatakuwa makini, anaweza kulaghaiwa na baadhi ya wauzaji.

Lakini sasa mambo yamebadilika, anayepaswa kuwa makini siyo mnunuaji tena, bali muuzaji. Hii ni kwa sababu taarifa zote zipo wazi sasa, huwezi kumdanganya tena mteja kuhusu sifa za kitu au ufanisi wake. Na pia huwezi kumlaghai mteja na ukamkimbia.

Mteja anaweza kupata taarifa za kitu chochote kwa kutafuta mtandaoni na hata kuuliza watu kwenye mitandao ya kijamii. Unapompa mteja huduma ambayo hakuridhika nayo anaweza kuwaambia watu kwenye mitandao ya kijamii na sifa yako ikaharibika.

Hivyo wewe kama muuzaji kuwa makini, jua kabisa mteja mpaka anafika kwako, ameshatafuta sana na hivyo ana taarifa nyingi, mweleze ukweli kuhusu kile unachouza na tekeleza kila unachoahidi. Kadiri unavyojenga mahusiano bora na wateja wako, ndivyo unavyoweza kufanikiwa kwenye mauzo.

SITA; UWASILISHAJI WENYE USHAWISHI.

Unaweza kuwa na bidhaa, huduma au wazo bora sana, ambalo wengine wanalihitaji ili wapige hatua, lakini jinsi unavyowasilisha kwao ikawa siyo sahihi, ukashindwa kuwashawishi na hivyo wasichukue hatua.

Hivyo wewe kama muuzaji unapaswa kujifunza njia bora za kuwasilisha bidhaa, huduma au wazo lako kwa wengine, kwa namna ambayo itaibua ushawishi ndani yao na waweze kuchukua hatua.

Ushawishi kwenye uwasilishaji huwa unaanza kwenye sekunde 30 za kwanza. Ukishakosea hapo unakuwa umempoteza mtu. Kwa sasa watu hawana muda kabisa, hivyo wanachukua muda mchache sana kufanya maamuzi. Kama unaanza uwasilishaji wako kwa njia ambayo haina ushawishi, utakuwa unawapoteza watu kabla hata hujawaeleza kile chenye manufaa kwao.

Hivyo unapaswa kutengeneza uwasilishaji wako kwa yule unayetaka achukue hatua kwa namna ambayo inaibua ushawishi na tamaa kwake ndani ya sekunde 30 za kuanza kwa mazungumzo yako.

Kuna aina sita za uwasilishaji ambazo mwandishi ametushirikisha kwenye kitabu hiki. Aina hizi nitakushirikisha kwenye #MAKINIKIA ya juma ambayo yanapatikana kwenye channel ya telegram ya TANO ZA JUMA. Kama bado hujawa kwenye channel hii, nenda mwisho wa makala hii kuna maelekezo ya namna ya kujiunga.

Kwa kujua aina hizi sita za uwasilishaji ambazo tunakwenda kujifunza, hakuna tena mtu atakayeweza kukuponyoka kwa sababu hajakuelewa au hajashawishika, maana aina hizi sita zinagusa maeneo yote ya ushawishi kwa watu. Karibu tujifunze kwa kina aina hizo sita za uwasilishaji pamoja na mifano ya jinsi ya kutumia kila aina.

SABA; MAMBO MATATU YA KUZINGATIA WAKATI A UWASILISHAJI.

Unapokuwa unaongea na mteja au yeyote unayetaka kumshawishi, kuna mambo matatu muhimu sana ya kuzingatia ili uweze kufika mwisho mzuri wa mtu huyo kuchukua hatua ambayo unataka achukue.

Jambo la kwanza; SIKILIZA.

Watu wengi siyo wasikilizaji wazuri, wanatumia muda mwingi kuongea na hilo linawakosesha fursa ya kuwajua vizuri wale wanaoongea nao. Weka juhudi kubwa kwenye kusikiliza kwa makini, sikiliza siyo kwa kujiandaa kujibu, bali sikiliza ili kuelewa. Unaposikiliza, watu wanakuwa tayari kuweka mambo yao wazi na hapo utajua njia gani bora ya kuwashawishi zaidi. Kuwa msikilizaji.

Jambo la pili; sema ‘NDIYO NA’

Fikiria umemwambia mtu kitu, ambacho ni cha manufaa kwake na unajua kabisa kamba kitamsaidia, lakini anakuja na pingamizi, anakueleza kwa nini kitu hicho hakitamfaa au siyo sahihi kwake. Katika hali kama hii, wengi hukimbilia kukataa pingamizi hilo, humbishia mteja kwamba pingamizi lake siyo sahihi. Na hapo mchakato wa mauzo unakufa, maana ukishamkatalia mteja anajenga upinzani na hatonunua. Kuondokana na hali hiyo, unapaswa kukubaliana na mteja na kisha kumpa sababu sahihi kwa nini anapaswa kuchukua hatua unayomwambia.

Mfano unauza kitu na mteja anakuambia kitu hicho ni bei ghali sana. Badala ya kumwambia HAPANA siyo bei ghali, au kumwambia NDIYO ni bei ghali LAKINI kinakufaa, tumia ‘NDIYO NA’, mwambie NDIYO ni bei ghali NA kwa ukubwa huo wa bei anapata thamani zaidi, ubora zaidi na hatapoteza fedha kununua tena ukilinganisha na akinunua cha bei rahisi. Kwa kila hali, kubaliana na mteja na endelea kumpa manufaa ziadi, ataona upo upande wake na atakuwa tayari kununua.

Jambo la tatu; MPE USHINDI.

Kipindi cha nyuma mauzo ilikuwa kama vita, ni wewe uweze kumlaghai mteja na kunufaika au mteja aweze kukulaghai wewe na akanufaika zaidi. Lakini kwa sasa hiyo haifanyi kazi tena. Hivyo unapaswa kumpa ushindi mteja wako katika uwasilishaji au mazungumzo yenu ya mauzo. Lengo lako linapaswa kuwa kumpa mteja wako ushindi, kumfanya apate thamani zaidi ukilinganisha na gharama anazoingia. Unapofanya hivi kwa uaminifu wateja wanajua, wanakuamini na kuendelea kununua kwako na hata kuwaleta wengine wanunue pia.

NANE; HUDUMIA.

Msingi mkuu wa mauzo ni kutoa huduma kwa wengine, kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Hiki kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kabla hata wewe hujapata faida. Kwa sababu kama utapata faida lakini wateja wako wakaumia, hutakuwa na wateja siku zinazokuja. Unapojitoa kuwahudumia wateja wako, kwa kuwapa zaidi thamani na kuweka maslahi yao mbele, wanajenga mahusiano bora na wewe na kukaa na wewe kwa muda mrefu.

Katika kutoa huduma bora kwa wateja wako, kuna mambo mawili ya kuzingatia;

Jambo la kwanza ni lifanye kuwa jukumu binafsi.

Jinsi unavyochukulia kitu, kuna maana kubwa sana ndani yako na hatua unazochukua. Kama utachukulia kile unachofanya kama jukumu lako binafsi la kuhakikisha wale unaowagusa wanakuwa na maisha bora, utasukumwa zaidi na utaweza kuwashawishi zaidi. Kama watu wanapokosa kile unachotoa unaona ni kushindwa kwako, utakazana kuhakikisha wanakipata.

Jambo la pili ni lifanye kuwa jukumu lenye maana.

Usifanye kitu kwa sababu tu unataka kupata fedha, badala yake fanya kwa sababu ni kitu chenye maana kwako. Hivyo chochote unachouza, usiuze tu kwa sababu utapata fedha, bali uza kwa sababu kuna maana kubwa zaidi ya fedha. Tafiti zinaonesha maana huwa ina nguvu kubwa kwenye kuwasukuma watu na hata kuleta hali ya kuridhika kuliko fedha. Hivyo tengeneza maana kupitia kile unachouza, na maana hiyo itakusukuma zaidi. Utaweza kutengeneza maana kama kuna thamani unayotoa kupitia unachouza, kama unaona jinsi maisha ya wengine yanavyokuwa bora zaidi kupitia unachouza.

Rafiki, haya ndiyo mambo muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi ili kuweza kufanikiwa kwenye mauzo. Jua kwamba upo kwenye mauzo, jua maeneo matatu ya kugusa ili kutengeneza ushawishi, sikiliza na usibishane na mteja na tengeneza maana kupitia kile unachouza.

Kilicho muhimu kabisa ni uwasilishaji wenye ushawishi, ambapo kuna aina sita za uwasilishaji wenye ushawishi mkubwa. Tutajifunza aina hizi kwenye #MAKINIKIA YA JUMA, usikose kwenye channel ya TANO ZA JUMA. Tuma ujumbe kwa kutumia app ya telegram mesenger wenye maneno TANO ZA JUMA kwenda namba 0717396253 na utaunganisha na kuendelea kujifunza.

#3 MAKALA YA JUMA; MAENEO MATATU YA KUZINGATIA ILI KUWA NA USHAWISHI ZAIDI.

Kama tunavyoendelea kujifunza, uuzaji umebadilika sana katika zama hizi. Zamani uuzaji ulikuwa wa kutumia presha na kumsukuma mteja kununua sasa. Njia hiyo ilifanya kazi kwa sababu wateja hawakuwa na taarifa za kutosha na hawakuwa na machaguo mengi.

Lakini kwa sasa wanunuaji wana taarifa za kutosha na machaguo ni mengi. Hivyo kama utataka kutumia njia ya kusukuma na presha watu watakukimbia.

Kuna njia mpya ya kuuza ambayo ina ushawishi mkubwa kwa wengine. Njia hii inagusa maeneo matatu ambayo yanamfanya mteja kushawishika na kuchukua hatua.

Kwenye makala ya juma hili nimekushirikisha maeneo matatu ya kuzingatia ili uweze kuwa na ushawishi mkubwa kwenye uuzaji. Ukiyazingatia maeneo hayo matatu, utaweza kuwashawishi watu kununua bila ya kuwasukuma au kuwapa presha. Watu watajiona wamechukua maamuzi ya kununua wao wenyewe na siyo kusukumwa. Na hicho ndicho kila muuzaji anakihitaji ili kuuza kwa mafanikio zaidi.

Kama hukusoma makala ya juma hili kuhusu ushawishi, isome sasa hapa; Zingatia Maeneo Haya Matatu Na Utaweza Kushawishi Na Kuuza Zaidi.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku ili kuweza kujifunza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

#4 TUONGEE PESA; KAMA UNATAKA PESA UZA ZAIDI.

Kama kipato chako ni kidogo na hakitoshelezi, tatizo lako kubwa ni moja, unauza kidogo. Na ili kuondoka kwenye hali hiyo ya kipato kidogo na kisichotosheleza unahitaji kuchukua hatua moja; KUUZA ZAIDI.

Usiniambie wewe umeajiriwa na hivyo huwezi kuuza zaidi, kumbuka kuna kitu ambacho unamuuzia mwajiri wako, sasa muuzie hicho zaidi. Mfano moja ya vitu unamuuzia mwajiri wako ni muda wako. Hivyo kuna muda wa makubaliano wa kufanya kazi kwa siku na kwa juma. Sasa wewe muuzie mwajiri wako muda zaidi, kwa kuweka muda wa ziada kwenye majukumu ambayo ni muhimu kwa mwajiri lakini yanakosa muda wa kufanyika. Kadhalika kwenye ujuzi na uzoefu wako, ambavyo ni vitu vingine unavyomuuzia mwajiri wako, jiulize ni wapi mwajiri ana uhitaji au changamoto na wewe unaweza kusaidia zaidi, kisha mshawishi akupe nafasi hiyo kwa mbinu za mauzo ambazo umejifunza.

Kila mtu anaweza kuuza zaidi, na hilo ndiyo suluhisho la kifedha kwa kila aliyekwama.

Unaweza kuuza zaidi kwa wateja ulionao sasa, hapa unawapa bidhaa au huduma ambayo hukuwa nayo awali. Ni njia rahisi kuanzia kwa sababu wateja ulionao tayari wanakujua hivyo hawana wasiwasi sana na wewe.

Lakini pia unaweza kuuza zaidi kwa kuwafikia wateja wapya. Hapa unatafuta wateja ambao bado hawajanufaika na bidhaa au huduma zako kisha unawashawishi wanunue, hivyo unaongeza wateja na mauzo pia.

Kwa vyovyote vile, kila wakati kazana kuuza zaidi, kwa wateja ulionao sasa wauzie zaidi ya wanavyonunua sasa na pia wafikie wateja wapya ambao hawajawahi kununua kwako.

Na kwa mbinu bora za MAUZO ambazo tumejifunza kwenye kitabu hiki na vingine, mbinu bora za UNENAJI na UANDISHI ambazo tulishajifunza, kila mtu anaweza kuwashawishi wengine na kuuza zaidi.

Hivyo rafiki, kila wakati unapokuwa unajiuliza unawezaje kupata fedha zaidi, badili swali na jiulize unawezaje kuuza zaidi. Maana ni kupitia kuuza ndiyo unaongeza kipato chako zaidi. Anza sasa, anzia hapo ulipo, tafuta mteja mpya wa kumuuzia na tafuta kitu kipya cha kuuza kwa wateja ulionao sasa, na kwa hakika utapiga hatua zaidi.

Njia pekee ya kuongeza kipato chako ni kuuza zaidi, acha kulalamikia udogo wa kipato na anza kuuza zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; ELIMU YA DARASANI INAPOKWAMA.

 

“In the new world of sales, being able to ask the right questions is more valuable than producing the right answers. Unfortunately, our schools often have the opposite emphasis. They teach us how to answer, but not how to ask.” ― Daniel H. Pink

Kwenye ulimwengu mpya wa mauzo, kuuliza maswali sahihi ni bora kuliko kuwa na majibu sahihi. Kwa sababu tayari mteja anajua mengi zaidi, jukumu lako kama muuzaji ni kuuliza maswali yatakayokupa wewe fursa ya kumjua mteja zaidi.

Lakini kwa bahati mbaya sana, elimu ya darasani iko kinyume na hili. Miaka yote ambayo tumekaa shuleni tumekuwa tunafundishwa jinsi ya kujibu maswali ili kufaulu mtihani. Hivyo unakuwa vizuri sana kwenye kujibu maswali, lakini unapofika mtaani unakuta tayari kila mtu ana majibu. Hivyo elimu ya darasani inakwama hapo.

Ili kupiga hatua kwenye kitu chochote unachofanya kwenye maisha yako, jifunze jinsi ya kuuliza maswali sahihi, maswali ambayo yatakupa nafasi ya kumjua mtu zaidi na mahitaji yake, ili uweze kumhudumia zaidi.

Kadiri unavyoweza kuuliza maswali sahihi na kusikiliza kwa makini majibu yanayotolewa, ndivyo unavyoweza kujifunza na kujua hatua sahihi za kuchukua.

Rafiki, hizi ndizo TANO ZA JUMA la 32, ambapo tumejifunza kwa kina kuhusu uuzaji kwenye ulimwengu mpya. Yaweke haya kwenye matendo ili uweze kuwa na ushawishi zaidi kwa wale unaowataka wachukue hatua kupitia kile unachofanya.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili tunakwenda kujifunza aina sita za uwasilishaji (pitch) wenye ushawishi kwa wengine. Aina hizi zinakuwezesha kuwafanya watu wakuelewe kwa haraka, kukusikiliza zaidi na kuchukua hatua. Tutajifunza aina hizo sita kwa mifano na itakuwa rahisi kwako kutumia aina hizo za uwasilishaji kupata ushawishi zaidi kwa wengine.

Usikose #MAKINIKIA ya juma kwa kuhakikisha umejiunga na channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Maelekezo ya kujiunga yako hapo chini. Yasome na uchukue hatua sasa.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu