Mpendwa rafiki yangu,
Kuongea mbele ya watu ni sanaa ya unenaji. Watu wengi wanaogopa sana kuongea mbele ya watu na wengi pia hawajui kuongea mbele ya watu.
Kila mtu anaweza kuongea mbele ya watu kwani hakuna mtu ambaye hajawahi kuongea mbele ya watu zaidi ya wawili. Tunapoongea mbele ya watu tunakuwa tunauza mawazo yetu kwa wengine.
Unapoongea mbele ya watu unakuwa wewe ndiyo mnenaji, hivyo unatakiwa kujiamini na kuamini pia kile unachoongea. Kabla hujaingia kuongea hakikisha umekifanyia kazi kile unachotaka kuongea hii itakupa nguvu kubwa ya kujiamini wakati unaongea.
Udhaifu mmoja wa watu wengi pale wanapoongea na watu ni kutowaangalia usoni wale anaoongea nao yaani hadhira yake. Unapoongea mbele ya watu hakikisha unawaangalia usoni wale unaoongea nao. Kitendo cha kuangalia chini au kuwaonea aibu wale unaongea nao ni ujinga sana, unaonesha kuwa na udhaifu na hujiamini.
Shabaha yangu kubwa leo ni kujifunza lugha ambayo tunapaswa kuiepuka kama mnenaji pale unapoongea na watu. Lugha ambayo unapaswa kuiepuka kuitumia wewe kama mnenaji ni lugha ya taaluma fulani. Kwenye kila taaluma fulani huwa wana lugha yao ambayo wakikaa wao kwa wao wanaelewana lakini watu ambao wako nje na hiyo taaluma hawawezi kuielewa vizuri.
Lugha hiyo kwa huitwa jargon, hizi ni lugha ambazo hutakiwi kuzitumia kabisa pale unapoongea kama mnenaji. Kwa mfano, labda wewe ni daktari sasa umealikiwa kuwa kama mnenaji badala ya kuongea misamiati migumu inayohusiana na lugha yako ongea rahisi ili watu wakuelewe.
Mara nyingi unapowasilisha jambo usitumie lugha ngumu ambayo unajiua wewe, bali tumia lugha rahisi ambayo kila mtu anaweza kuielewa. Unapotumia lugha ngumu za kitaaluma unakuwa bado hujafikisha ujumbe kwa wengine.
Hatua ya kuchukua leo; ongea lugha rahisi ambayo kila mtu ataelewa kirahisi. Usitumie lugha za kitaaluma yaani jargon zenye misamiati migumu. Kuongea misamiati migumu ili uonekani ni mtu makini huo ni ujinga. Umakini wa mtu unapimwa pale anapoweza kuwasilisha jambo kwa watu na kueleweka kwa urahisi.
Kwahiyo, pale unapoongea tumia lugha rahishi, lakini pia pendelea kukazia au kurudia zile pointi muhimu ambazo unataka mtu azielewe na kuondoka nazo. Ongea taratibu na kazia yale mambo muhimu kwa sauti tofauti au hata kuyarudia ili wale wanaokusikiliza wakuelewe vema.
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa http://kessydeo.home.blog
vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana