Rafiki yangu mpendwa,

Kila mmoja wetu anauza, ndiyo, hapo ulipo kuna vitu unauza. Kama upo kwenye biashara unauza bidhaa au huduma zako. Kama umeajiriwa unauza muda wako, utaalamu wako na uzoefu wako kwa mwajiri wako. Na kama wewe ni kiongozi unauza sera na maono yako kwa wale unaowaongoza.

Kuna njia mbili za kufikisha ushawishi wako kwa wale ambao unawauzia. Njia hizi ni kupitia kuongea na kuandika. Hizi ni njia mbili ambazo unapaswa kujua jinsi ya kuzitumia kwa usahihi ili kuweza kuwashawishi wengine wakubaliane na wewe kwa kile unachouza.

copywriting

Lakini cha kushangaza ni kwamba watu huwa wanajifunza vitu vigumu sana kwenye maisha na visivyo na msaada mkubwa kwao, lakini hawajifunzi njia bora za kufikisha ushawishi wao kwa wengine kupitia maandishi na maongezi.

Juma lililopita nilikushirikisha njia za kuwa na ushawishi kupitia unenaji, na tukapata uchambuzi wa kina wa kitabu cha sanaa ya unenaji kwenye makala ya TANO ZA JUMA. Kama hukupata nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu unenaji, basi rejea kwenye makala ya TANO ZA JUMA kwa kubonyeza maandishi haya.

Leo tunakwenda kujifunza eneo la pili la kubobea ili kuweza kuwa na ushawishi kwenye kile tunachouza. Eneo hilo ni uandishi.

Unaweza kujiambia wewe siyo mwandishi, na hivyo makala hii haikuhusu, lakini utakuwa umefanya kosa kubwa sana. Kwa sababu iwe unajua au hujui, wewe ni mwandishi. Njia bora kabisa za mawasiliano tunazotumia sasa, zinasimama kwenye uandishi.

Unaandika ujumbe kwa watu kwa njia ya simu, unaandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, unawatumiwa watu barua pepe, unatuma barua za kawaida, zote hizo ni njia ya uandishi.

Kwa upande wa pili kuna wale ambao maisha yao yanategemea uandishi, kama waandishi wa makala na vitabu, waandishi wa habari, waandishi wa matangazo na kadhalika.

Kama unauza, na kwa sababu kila mmoja wetu kuna kitu anauza, basi uandishi bora utakusaidia kuuza zaidi.

Leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kuandika nakala bora ya mauzo, yenye ushawishi mkubwa na itakayowasukuma watu kununua unachouza.

Tunajifunza haya kutoka kitabu kinachoitwa HOW TO WRITE COPY THAT SELLS; The Step-By-Step System For More Sales, to More Customers, More Often ambacho kimeandikwa na RAY EDWARDS, ambaye ni mmoja wa waandishi bora kabisa wa matangazo na nakala za kuuza (sales copy).

Uandishi wa nakala za mauzo (copywriting) ni sanaa ya kutengeneza ushawishi kwa kutumia maandishi. Wengi tumezoea ushawishi ni kwa njia ya mazungumzo na maandishi ni kuonesha ukweli. Lakini kumbe uandishi unaweza kutumiwa kufikisha na kuibua hisia kwa wengine na kuwasukuma kununua kile kinachoelezwa kwenye nakala hiyo au kuchukua hatua ambayo wanapaswa kuchukua.

Katika kuhakikisha nakala unayoandika inauza na kuwa na ushawishi kwa wengine, Ray Edwards anatushirikisha hatua sita za kufuata. Fuata hatua hizi tano na utaweza kuwa na uandishi wenye ushawishi mkubwa kwa wale unaowalenga. Iwe unaandika tangazo, ujumbe, makala, kitabu au chochote kile ambacho unataka watu wachukue hatua fulani.

TAHADHARI; Kabla hujaingia kujifunza njia hizi sita, mwandishi anatoa tahadhari moja muhimu sana. Njia hisi sita zina nguvu kubwa sana, usipozitumia vizuri unaweza kuwahadaa na kuwatapeli watu, ukawafanya wanunue kitu ambacho hawakitaki. Hilo litakunufaisha kwa muda lakini litakuangusha. Hivyo mwandishi anatuomba sana tuwe waaminifu na waadilifu na tutumie njia hizi kwa usahihi.

Hatua Sita Za Kuandika Nakala Ya Mauzo Inayowavutia Watu Kusoma Na Kushawishika Kununua Unachouza.

HATUA YA KWANZA; MTU, TATIZO, MAUMIVU.

Ili kupata ushawishi, anza kwa kuchagua ni mtu wa aina gani ambaye unamlenga. Lazima ujumbe unautuma uwe unamlenga mtu wa aina fulani, mwenye sifa fulani. Kuandika ujumbe ambao unataka kumlenga kila mtu ni kuchagua kutokumlenga yeyote yule. Anza na sifa za mtu au mteja unayetaka kumshawishi kupitia ujumbe wako.

Ukishachagua mtu unayemlenga, jua ni matatizo gani aliyonayo ambayo wewe unaweza kuyatatua kupitia kile ambacho unataka kumuuzia. Kumbuka watu hawatanunua kama hawana tatizo, na kama huna kile ambacho kinatatua tatizo walilonalo, hawatasukumwa kununua kwako au kufanya kile unachowataka wafanye.

Kwa kujua tatizo walilonalo ambalo unalitatua, jua ni maumivu kiasi gani tatizo hilo linawapa. Ni kupitia maumivu ambayo mtu huyu anayo ndiyo unaweza kuwashawishi na kuwasukuma kuchukua hatua ambazo unataka wachukue.

Unapoandika nakala yako ya mauzo, hakikisha inamlenga mtu fulani, ikieleza suluhisho ulilonalo ambalo linatatua matatizo na kuondoa maumivu yake.

Kumbuka; MTU, TATIZO, MAUMIVU.

HATUA YA PILI; KUZA TATIZO, IBUA TAMAA.

Baada ya kujua mtu unayemlenga, tatizo alilonalo na maumivu anayopata, hatua ya pili ni kukuza tatizo hilo. Kumbuka watu huwa hawachukui hatua kama hakuna kinachowasukuma kufanya hivyo. Hivyo unachopaswa kufanya ni kumwonesha mteja jinsi tatizo lilivyo kubwa kuliko anavyofikiri, au kumwonesha jinsi ambavyo tatizo litazidi kuwa kubwa kama hatochukua hatua sasa. Ni kupitia kukuza tatizo ndiyo unamsukuma mteja kuchukua hatua. Lakini kumbuka hili muhimu sana, usidanganye wala kulaghai.

Katika hatua hii ya pili pia unapaswa kuibua hisia za tamaa kwa wateja wako, hapa tengeneza picha ya mambo kuwa mazuri pale wanapopata kile ambacho unataka wanunue au kuchukua hatua ambayo unataka wachukue.

Sisi binadamu huwa tunafanya maamuzi kwa hisia na kisha kuyahalalisha kwa kufikiri. Na hisia mbili zinazotusukuma kufanya maamuzi ni MAUMIVU NA TAMAA. Kama kuna maumivu tunapata tutachukua hatua, kama kuna kitu tutapata tutachukua hatua.

Hivyo nakala yako ya mauzo hakikisha inakuza tatizo kwa kuonesha maumivu na kuibua tamaa kwa kuonesha vitu vizuri ambavyo mtu atapata kwa kuchukua hatua.

Kumbuka; MAUMIVU NA TAMAA.

HATUA YA TATU; HADITHI, SULUHISHO, MFUMO.

Umeshaeleza tatizo, kulikuza na kuibua tamaa ya kupata kile ambacho unataka watu wachukue hatua. Kinachofuata ni kushirikisha hadithi ya jinsi tatizo hilo linavyoweza kutatuliwa.

Hadithi inategemea na kile unachouza au kutaka watu washawishike. Inaweza kuwa hadithi yako binafsi ya jinsi ulivyotatua tatizo lililokuwa linakukabili kwa njia unayowashawishi watu watumie. Lakini pia inaweza kuwa hadithi kuhusu wengine ambao wamenufaika na kile unachouza au kuwashawishi watu.

Hadithi unazoshirikisha lazima zioneshe jinsi kitu hicho kimeleta suluhisho na mfumo ambao umetumika kuleta suluhisho hilo.

Watu wanaelewa na kupata msukumo wa kuchukua hatua pale wanapoelezwa kwa hadithi rahisi kwao kuelewa.

Kumbuka; HADHITHI, SULUHISHO, MFUMO.

HATUA YA NNE; MABADILIKO NA SHUHUDA.

Kitu muhimu sana unachopaswa kujua ni kwamba watu hawanunui kile unachouza, bali wananunua matokeo ambayo wanataka kuyapata. Mtu anapoenda kununua godoro, hanunui kwa sababu ya sifa ya godoro, bali ananunua usingizi mzuri. Hivyo unapoelezea kile unachouza, usikielezee kwa sifa yake, bali elezea kwa namna kitakavyoleta mabadiliko kwenye maisha ya mtu. Mtu anapoyaona mabadiliko yake, anasukumwa zaidi kuchukua hatua.

Kitu kingine muhimu sana kutumia wakati wa kuandika nakala ya kuuza ni shuhuda za wale ambao wametumia unachouza na maisha yao yakawa bora zaidi. Wanasema kueleza sifa zako mwenyewe ni kujisifia, lakini wengine wanapoeleza sifa zako ndiyo uhalisia.

Wapate wateja ambao wameshanunua au kutumia kile unachouza kisha watoe ushuhuda wao. Unaweza kuwa kwa maandishi, kwa picha au kwa video. Kadiri ushuhuda unavyokuwa halisi, ndivyo wengi zaidi wanashawishika kuchukua hatua.

Kabla mtu hajanunua unachouza, kuna maswali haya matatu ambayo anataka majibu yake;

  1. Je mtu huyu ameweza kufanya kile ambacho anakisema?
  2. Je mtu huyu ameweza kuwafundisha wengine kufanya kile anachoeleza?
  3. Je mtu huyu anaweza kunifundisha mimi kuikia matokeo anayoelezea?

Ukimpa mtu majibu ya maswali hayo matatu, jibu lake litakuwa NDIYO na atanunua au kuchukua hatua.

Kumbuka; MABADILIKO NA SHUHUDA.

HATUA YA TANO; OFA.

Umeshamweleza mteja tatizo lake, na ukaonesha madhara yake kama hatalitatua, ukampa hadithi ya suluhisho na kumwezesha kuona jinsi ambavyo unachomuuzia kitabadili maisha yake, kupitia shuhuda za wengine. Mpaka hapo umempa mteja hamasa, lakini bado hajafikia hatua ya kununua.

Hatua inayofuata ni kumpa mteja ofa, hapa unamweleza ni nini hasa atapata kwako na atakipataje. Katika hatua hii unamweleza mteja kile ambacho atakipata kwako na ambacho kitatimiza yale yote ambayo umekuwa unamwahidi tangu hatua ya kwanza mpaka ya nne.

Unapaswa kuieleza ofa kwa lugha rahisi na ya moja kwa moja, ambayo inamwonesha mteja nini hasa anakwenda kupata.

HATUA YA SITA; HATUA ZA KUCHUKUA.

Watu wengi wamekuwa wanaweka kazi kubwa kwenye hatua tano tulizojifunza hapo juu, halafu wanaishia hapo. Wanakuja kushangaa kwa nini watu hawanunui licha ya kuwaeleza kila kitu kuhusu wanachouza.

Wanachosahau ni kwamba, watu hawatanunua kama hutawaambia wanunue. Hivyo hatua ya sita ni kuwaambia watu wanunue, kuwapa hatua ya kuchukua ili wapate kile ambacho umekuwa unawaeleza.

Katika hatua hii usione aibu kumwambia mteja anunue. Mweleze kwamba ameshajua kila kitu sasa ni wakati wake wa kuchukua hatua, mkumbushe kuhusu maumivu yake na nafasi aliyonayo sasa ya kuchukua hatua.

Kwenye nakala yako ya mauzo weka maelekezo ya hatua ambazo mteja anapaswa kuchukua, labda ni kupiga simu, kutuma ujumbe, kutembelea kwenye biashara, kujibu kitu, kufungua mtandao na kadhalika.

Usimalize kuandika nakala ya mauzo bila ya kuwa na hatua ambayo mtu anachukua. Hata kama ni ujumbe wa salamu umetuma kwa wateja wako, hakikisha unawapa hatua ya kuchukua, hata kama siyo ya kununua.

Watu huwa wanachukua hatua pale wanapoelezwa hatua wanazopaswa kuchukua, maliza nakala yako ya mauzo kwa kuwaeleza wateja hatua za kuchukua.

Rafiki, hizo ndizo hatua sita za kuandika nakala itakayokuwa na ushawishi kwa wateja wako na kukuwezesha kuuza zaidi. Kama ambavyo Ray ametuambia, unaweza kutumia njia hizi kuwatapeli wengine, lakini itakuwa na madhara makubwa kwako baadaye. Hakikisha una bidhaa au huduma ambayo ina msaada kweli kwa watu na kisha andika nakala za mauzo zenye ushawishi kwa wateja wako.

Ili kubobea kwenye hatua hizi ulizojifunza, fanya zoezi la kuandika nakala nyingi sana za mauzo. Kwa kila unachoandika, fuata hatua hizo tano na utaweza kutengeneza ushawishi mkubwa kupitia uandishi wako.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 31 la mwaka 2019, tutakwenda kujifunza kwa kina kuhusu uandishi wa nakala za mauzo.

Kwenye makala hiyo ya TANO ZA JUMA, tutajifunza; jinsi ya kuandika vichwa vya habari vyenye mvuto, jinsi ya kuandika barua pepe zinazouza zaidi, vitu vitatu vitakavyokuwezesha kuuza zaidi kupitia nakala ya mauzo, jinsi ya kutoa ofa ambayo mteja hawezi kuikataa na mchakato wa uzinduzi wa bidhaa au huduma mpya na jinsi ya kuwavutia watu zaidi kwenye uzinduzi.

Usikose makala ya TANO ZA JUMA hili, tembelea mtandao wa AMKA MTANZANIA siku ya jumapili kuhakikisha unaipata na kuisoma ili uweze kuandika kwa ushawishi na kuuza zaidi.

MUHIMU; Jipatie kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA leo kwa bei ya punguzo. Kitabu kinauzwa tsh elfu 20, lakini leo utakipata kwa bei ya tsh elfu 15. Piga simu au tuma ujumbe sasa kwenda namba 0678 977 007. Usikose zawadi hii leo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge