#TANO ZA JUMA #31 2019; Kila Mtu Ni Mwandishi, Jinsi Ya Kuandika Nakala Inayouza Sana, Hatua Sita Za Kuandika Nakala Inayouza, Tengeneza Kipato Kupitia Uandishi Na Ujuzi Uliozalisha Mamilionea Wengi Duniani.

Rafiki yangu mpendwa,

Ni matumaini yangu kwamba juma namba 31 la mwaka huu 2019 limeanza na kuisha vizuri kwa upande wako. Naamini limekuwa juma bora kwako, juma ambalo umejifunza na kupiga hatua kubwa zaidi kuelekea kwenye mafanikio makubwa. Hongera sana kwa hilo.

Nachukua nafasi hii kukukaribisha kwenye TANO ZA JUMA hili, ambapo tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu uandishi wa nakala za kuuza au kama inavyojulikana kwa kiingereza copywriting.

Mara nyingi nimekuwa narudia kauli hii kwamba kila mmoja wetu ni muuzaji, na ni kweli kwamba kila mtu kuna kitu anauza. Sasa mafanikio yako kwenye uuzaji yanategemea vitu viwili vikubwa, moja ni ushawishi wako kwenye kuongea na mbili ni ushawishi wako kwenye kuandika.

Kama utaweza kubobea kwenye vitu hivyo vitatu pekee, yaani kuwa mbobezi kwenye kuuza, ukawa mbobezi kwenye kuongea kwa ushawishi na kuwa mbobezi kwenye kuandika kwa ushawishi, utaweza kupata au kuwa chochote unachotaka kwenye maisha yako. Hilo ni uhakika.

Kwenye TANO ZA JUMA la 30 tulijifunza jinsi ya kuongea kwa ushawishi, kama hukusoma tano hizo za juma, bonyeza maandishi haya.

Moja ya vitabu muhimu sana unavyopaswa kuvisoma ili kubobea kwenye mauzo ni kitabu cha Brian Tracy kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF SELLING. Unaweza kusoma uchambuzi wa kitabu hicho kwa kubonyeza maandishi haya.

How to Write Copy That Sells

Kwenye tano za juma hili la 31 tunakwenda kujifunza jinsi ya kubobea kwenye uandishi, kwa kuweza kuandika nakala yenye ushawishi na inayowasukuma watu kuchukua hatua unayotaka wachukue.

Tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa HOW TO WRITE COPY THAT SELLS; The Step-By-Step System For More Sales, to More Customers, More Often kilichoandikwa na RAY EDWARDS. Mwandishi Ray ni mmoja wa waandishi mashuhuri wa matangazo na nakala za mauzo. Kupitia kitabu hiki anatushirikisha siri na mbinu muhimu ambazo tukizielewa na kuzitumia tutaweza kuandika nakala bora kabisa za kuuza chochote tunachouza.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA, jifunze, chukua hatua na fanikiwa.

#1 NENO LA JUMA; KILA MTU NI MWANDISHI.

Siku za nyuma uandishi ilikuwa ni kazi ya watu wachache, wengi hawakuwa na fursa za kuwasilisha mawazo au hoja zao kwa uandishi. Hivyo hakukuwa na umuhimu mkubwa wa kujifunza uandishi bora.

Lakini sasa zama zimebadilika, kila mtu amekuwa mwandishi. Ukuaji wa mtandao wa intaneti na ujio wa mitandao ya kijamii kumempa kila mtu nafasi ya kuwa mwandishi.

Unapoandika ujumbe mfupi wa simu kwa mtu yeyote, hapo unafanya uandishi. Ujumbe wako unaweza kupokelewa kwa hamasa na mtu akachukua hatua au ukawa wa kawaida na mtu akaupuuza. Je wewe ungependa upande upo hapo?

Unapoingia kwenye mitandao ya kijamii na kushirikisha mambo mbalimbali unafanya uandishi. Unaweza kuandika kwa ushawishi na ukapata ‘likes’ nyingi pamoja na kuwavutia watu kuchukua hatua, au ukaandika kawaida na watu wakaupuuza na kuendelea na mambo yao. Je wewe ungependa upande upi hapo?

Unapoandika tangazo la kuwakaribisha wateja kwenye biashara yako, unajihusisha na uandishi. Tangazo lako linaweza kuwa na ushawishi wa kuwafanya watu wachukue hatua mara moja au likawa la kawaida na watu wakalipuuza. Tena, ungependa kuwa upande upi hapo?

Naamini hakuna mtu anayekaa chini kuandika ujumbe wa simu, ujumbe mtandaoni au tangazo la biashara yake huku akijiambia wacha nimalize kuandika kitu hichi haraka kwa sababu najua watu watakipuuza na hawatachukua hatua, lakini inabidi tu niandike. Hayupo mtu wa aina hii.

Sasa kama hakuna mtu wa aina hii, ambaye anaandika kwa kusudi la kupuuzwa, kwa nini maandishi mengi yanapuuzwa sana? Jibu ni moja, kwa sababu watu hawajajikubali kama waandishi na kujifunza kuandika kwa namna ambayo italeta ushawishi kwa wale wanaowalenga.

Hivyo rafiki yangu, nianze kwa kukuambia kubali kwamba wewe ni mwandishi. Halafu ukishakubali, chukua hatua ya kujifunza kuwa mwandishi bora, ili uweze kuandika nakala ambazo zinawasukuma watu kuchukua hatua.

Kwa kukubali kwamba wewe ni mwandishi na kujifunza njia bora za uandishi wenye ushawishi kutakuwezesha wewe kufanikiwa sana kwenye kazi au biashara unayofanya. Kwenye kitabu chetu cha juma tunakwenda kujifunza mbinu bora za uandishi wenye ushawishi. Karibu sana ujifunze.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUANDIKA NAKALA INAYOUZA SANA.

Aliyekuwa mwandishi na mhamasishaji Zig Zigler aliwahi kunukuliwa akisema kuuza ni kuhamisha hamasa, kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuaji. Akiwa na maana kwamba unaweza kuuza chochote kama una hamasa kubwa juu ya kitu hicho, na kuweza kuihamisha hamasa hiyo kutoka kwake na kuipeleka kwa mteja.

Zipo njia mbili za kuhamisha hamasa yao kama muuzaji kwenda kwa mnunuaji. Njia hizo ni kuongea na kuandika. Uongeaji wako unaweza kuwa wa ushawishi au usio na ushawishi, kuna mtu akiongea watu wanasikiliza kwa shauku, wakati mwingine akiongea watu wanapiga miayo na kusinzia.

Kadhalika kwenye uandishi, kuna watu ambao wakiandika watu wanasoma na kuhamasika na wapo wengine ambao wakiandika watu hata hawajisumbui kusoma, kwa sababu kichwa cha habari tu kinakosa mvuko.

Leo tunakwenda kujifunza kuhusu uandishi wenye ushawishi ambao unakuwezesha kuuza zaidi kile unachouza.

Kwenye kitabu cha HOW TO WRITE COPY THAT SELLS; The Step-By-Step System For More Sales, to More Customers, More Often cha RAY EDWARDS. Tunakwenda kujifunza mambo yote muhimu unayopaswa kuyajua ili kuweza kuandika nakala ambayo inauza sana.

Karibu tujifunze ili tuweze kuwa waandishi bora na chochote tunachoandika kiwe na ushawishi na kuweza kuuza zaidi.

MOJA; ANZA NA WAZO KUBWA.

Hatua ya kwanza kwenye uandishi wa mauzo ni kuwa na wazo kubwa, wazo ambalo linakubeba wewe na kile unachouza, wazo ambalo linagusa matatizo, mahitaji na maumivu ya wateja wako. Wazo hilo kubwa unapaswa kuweza kulielezea kwenye sentensi moja na mteja akakuelewa.

Hivyo kaa chini na tengeneza wazo kubwa la bidhaa au huduma unayouza, ambalo ndiyo litakuwa msingi wa nakala zako zote za mauzo unazoandika.

Mfano wa kuandika wazo lako kubwa ni kwa kutumia mfumo huu; HADHIRA YAKO, TATIZO WALILONALO, BIDHAA/HUDUMA YAKO na JINSI INAVYOFANYA KAZI.

Tutumie mfano wa kitabu kinachotoa maarifa ya kifedha, wazo kuu linakuwa hivi; mtu yeyote anaweza kuondoka kwenye umasikini na madeni kwa kusoma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambacho kitampa maarifa sahihi ya kuongeza kipato, kuweka akiba na kuwekeza.

MBILI; VIPENGELE 15 VYA BARUA YA MAUZO.

Unapoandika nakala yoyote inayoelezea bidhaa au huduma unayouza kwa lengo la kuwashawishi wateja kununua, hiyo inaitwa barua ya mauzo. Iwe unaandika kwa barua ya kawaida, barua pepe au makala kwenye mtandao au tovuti, kuna vipengele 15 ambavyo unapaswa kuhakikisha vinakuwepo kwenye nakala ya mauzo unayoandoka.

 1. Kabla ya kichwa cha habari, haya ni maelezo mafupi yanayoshika umakini wa walengwa.
 2. Kichwa cha habari, hapa ndipo mtu anapovutiwa kusoma nakala nzima.
 3. Utangulizi, hapa unaweka msisitizo wa umuhimu wa kile kilichoelezwa kwenye kichwa cha habari.
 4. Mwongozo, hapa unaweka vigezo vya nani nakala hiyo inamlenga na atanufaikaje kwa kuisoma.
 5. Nakala yenyewe, hapa sasa ndipo maelezo mengi yanapoingia, ambayo yanajumuisha vipengele vingine vinavyoelezewa hapo chini.
 6. Vichwa vidogo vya habari, hivi vinagawa nakala yako kwenye vipengele mbalimbali. Unapoweka vipengele inakuwa rahisi kwa mtu kusoma na kufuatilia.
 7. Kujenga mahusiano na msomaji, kuonesha kwamba unamjua vizuri kwa matatizo na maumivu yake.
 8. Orodha ya pointi muhimu, hapa unaorodhesha zile pointi muhimu ambazo unataka mteja aelewe kuhusu kile unachomshawishi.
 9. Sifa yako; hapa unahitaji kutoa maelezo ya kwa nini watu wakusikilize na kukuamini.
 10. Shuhuda; hapa unahitaji kuwa na shuhuda za watu wengine ambao wanathibitisha kile unachoeleza.
 11. Uhalali wa thamani; hapa unaeleza thamani unayoitoa huku ukilinganisha na gharama ambayo mtu analipa, kisha kuonesha kwa nini mtu anapata zaidi ya anacholipia.
 12. Kugeuza hatari; hapa unaiondoa hatari kwa mteja na kuiweka kwako, unatoa uhakika kwamba mtu atapata kitu kinachomfaa na kama hatapata basi atarejeshewa fedha yake.
 13. Zawadi; unapaswa kujumuisha zawadi ambazo mteja atazipata kwa kuchukua hatua, hiyo inampa hamasa zaidi.
 14. Hatua ya kuchukua; nakala yako ya mauzo lazima impe mteja hatua ya kuchukua ili kupata ile ofa unayompa.
 15. S (MUHIMU/NYONGEZA); Mwisho wa nakala yako ya mauzo unapaswa kuweka maelezo ya nyongeza au muhimu ambayo yanajumuisha ile ofa unayotoa faida zake na hatua za kuchukua.

Wasomaji wengi husoma kichwa cha habari, kuangalia vichwa vidogo vya ndani na kisha kwenda kusoma mwisho. Hivyo maeneo hayo yakiwa vizuri, utaweza kuwashawishi wengi kununua.

TATU; JINSI YA KUANDIKA KICHWA CHA HABARI KINACHOVUTIA.

Kichwa cha habari cha nakala yako ya mauzo huwa kinaitwa ‘tangazo la tangazo’. Yaani unaandika tangazo, lakini pia inabidi ulitangaze tangazo hilo. Kichwa cha habari ndiyo chenye nguvu ya kumvuta mtu kusoma zaidi au kumpoteza. Hivyo unapaswa kuandika vichwa vya habari vyenye mvuto wa kumfanya msomaji asome zaidi ili kunufaika.

Kichwa cha habari kinapaswa kukamilisha majukumu matatu muhimu;

 1. Kushika umakini wa mteja, kumfanya aache kile anachofanya sasa na kutaka kusoma nakala hiyo.
 2. Kutoa ahadi ambayo inamvutia mteja kuendelea kusoma ili kujua zaidi.
 3. Kuibua udadisi ndani ya mteja wa kutaka kusoma.

Hakikisha kichwa cha habari unachoandika kinakidhi vigezo hivyo vitatu.

NNE; AINA TANO ZA VICHWA VYA HABARI VINAVYOUZA ZAIDI.

Kuna aina tano za vichwa vya habari ambavyo vina ushawishi mkubwa kwa wateja na kuwasukuma kuchukua hatua. Aina hizo ni kama ifuatavyo;

 1. Jinsi ya; hiki ni kichwa cha habari kinachomweleza mteja jinsi ya kufanya kitu fulani. Mfano; jinsi ya kutengeneza fedha kwenye mtandao kwa kutumia blogu.
 2. Nipe nikupe; hiki ni kichwa cha habari ambacho kimekaa kimuamala, kinamwahidi mteja kitu fulani kwa kutoa kitu kingine. Mfano; nipe dakika 30 upate wateja zaidi.
 3. Kwa nini; hiki ni kichwa cha habari ambacho kinatoa sababu ya kwa nini mtu afanye kitu. Mfano; sababu 10 kwa nini mpaka sasa wewe siyo tajiri.
 4. Swali la uchunguzi; hiki ni kichwa cha habari ambacho kinauliza swali ambalo linamvutia mtu kusoma ili kupata majibu. Mfano; je ungependa watu wengi zaidi wanunue vitabu vyako?
 5. Kama; hiki ni kichwa cha habari kinacholinganisha kitu kinachoonekana kuwa kigumu na kingine ambacho ni rahisi. Mfano; kama unaweza kupokea na kutuma email basi unaweza kuendesha blogu.

Kwa kila aina ya kichwa cha habari unaweza kutengeneza vichwa vya habari vingi ambavyo vinamvutia mteja kuchukua hatua.

TANO; JINSI YA KUANDIKA BARUA PEPE ZINAZOLETA FEDHA ZAIDI.

Barua pepe ni moja ya njia zenye nguvu sana kwenye mauzo. Japo mitandao ya kijamii inaonekana kuwa na nguvu na watumiaji wengi, bado kwenye mauzo barua pepe zina nguvu kubwa kuliko mitandao ya kijamii. Barua pepe ina nguvu kwa sababu inamlenga mtu mmoja tofauti na mitandao ya kijamii ambayo humlengi mtu mmoja.

Ili kuweza kuuza zaidi kupitia barua pepe, zingatia mambo haya 21 muhimu;

 1. Tengeneza orodha ya mawasiliano ya email ya wateja wako kwa kupata ruhusa yao. Hapa unawaomba watu wajiunge kwenye mfumo wako ili wawe wanapokea ujumbe kutoka kwako.
 2. Tumia mfumo wa kutuma email wenye sifa nzuri. Mfano MailChimp, Aweber, InfusionSoft na kadhalika.
 3. Wape watu sababu ya kujiunga kwenye mfumo wako wa email, unaweza kuwapa zawadi pale wanapojiunga au kuwaahidi mambo mazuri kama wakijiunga.
 4. Epuka malalamiko ya wasomaji kwa kutuma ujumbe mara kwa mara. Kama unatuma ujumbe mara moja na kukaa muda mrefu bila kutuma, unapokuja kutuma tena ni rahisi wapokeaji kulalamika kwamba hawataki jumbe zako.
 5. Tengeneza mfumo wa kutuma email wenyewe (autoresponders) kwa wasomaji tangu wanapojiunga mpaka unapowatumia ujumbe unaowataka wanunue kitu.
 6. Fanya kazi kubwa ya kutengeneza ushawishi wa kuwafanya watu waingie kwenye mfumo wako wa email. Toa kitu ambacho wengine hawatoi kama zawadi ya watu kujiunga na mfumo wako wa email.
 7. Wape watu sababu ya kuendelea kukaa kwenye mfumo wako wa email na kujifunza. Kwa sababu watu wamejiunga haimaanishi wataendelea kuwepo au kusoma. Wengi hujiunga lakini hawasomi, na wengine wanajiunga lakini baada ya muda wanajitoa. Wape wasomaji wako maarifa yanayowafanya waendelee kubaki kwenye orodha yako.
 8. Weka hatua ya kuchukua kwenye kila barua pepe unayotuma, hata kama hakuna unachouza, wape wateja hatua ya kuchukua, hata kama ni ya kufungua na kujifunza zaidi kitu kingine. Unapowajengea wasomaji wako utamaduni huu wa kuwa na hatua ya kuchukua inakuwa rahisi kwao kununua pale unapowataka wafanye hivyo.
 9. Tengeneza maelezo mazuri kuhusu wewe binafsi au biashara yako ambao yatakaa mwisho wa kila barua pepe unayotuma. Inawapa wateja kukujua zaidi.
 10. Unapokuwa na bidhaa unayotangaza au kuuza tengeneza mfumo wa email unaoeleza kuhusu bidhaa hiyo na kuwashawishi wateja kununua. Kila barua pepe imfanye mteja kutaka kusoma inayofuata na kuibua tamaa. Mwisho mteja anapewa ofa na hatua za kuchukua.
 11. Jua ni kitu gani hasa unachotaka kwa msomaji wako kwa kila barua pepe unayotuma, na hakikisha barua pepe hiyo inatimiza hitaji hilo.
 12. Hakikisha kila barua pepe unayotuma inakuwa na ujumbe mmoja muhimu na hatua moja ambayo msomaji anapaswa kuchukua. Barua pepe ikiwa na hatua nyingi inamchanganya mteja.
 13. Andika kichwa cha habari cha baura pepe chenye mvuto na ushawishi kwa msomaji kufungua ili kusoma zaidi.
 14. Anza kila barua pepe na taarifa ambayo ni ya kweli na mteja hawezi kupingana nayo. Mfano unaweza kuanza na tarehe ya siku husika, hii inamfanya msomaji aanze kwa kukubaliana na wewe.
 15. Epuka barua pepe yako kuonekana kama tangazo, badala yake ifanye ionekane kama ujumbe ambao mtu anamtumia rafiki yake.
 16. Weka faida kubwa ya kile unachomshawishi mteja kwenye aya ya kwanza ya barua pepe. Watu wengi huwa hawasomi barua pepe yako, hivyo una sekunde 30 tu za kumshawishi mtu, manufaa makubwa yawe mwanzoni kabisa.
 17. Tumia maelezo ya mwisho ya nyongeza kutoa muhtasari wa barua pepe nzima na pia kutoa kiungo ambacho mtu anapaswa kubonyeza ili kuendelea na hatua nyingine.
 18. Weka angalau viungo (link) vitatu ambapo mteja anapaswa kubonyeza kwenye email yako. Yaani hata kama link ni ile ile, iweke sehemu tatu muhimu, mwanzo, katikati na mwisho. Ile ya mwanzo huwa inafunguliwa mara nyingi zaidi.
 19. Tuma barua pepe fupi ambazo zinamfanya msomaji kutaka kujifunza zaidi.
 20. Barua pepe zako zionekane na kusomeka kama zimetoka kwa rafiki na siyo kama tangazo.
 21. Mtu akitaka kujitoa kwenye mfumo wako wa email, mpe nafasi ya kufanya hivyo. Usilazimishe kutuma ujumbe kwa mtu ambaye hataki kupokea, atachukua nafasi kubwa na hakuna anachochangia kwako.

MUHIMU; Katika kutumia mfumo wa email kuuza, kuna watu watakujibu mambo hasi na ya kukatisha tamaa. Usisome wala kujibu majibu ya aina hiyo. mpe mtu mwingine kazi hiyo na wewe kazana kuandika barua pepe chanya kwa wale wanaonufaika.

SITA; VITU VITATU VITAKAVYOKUWEZESHA KUUZA ZAIDI.

Ili kuuza zaidi unapaswa kuzingatia vitu vitatu muhimu sana katika uandishi wa nakala zako za mauzo.

Kitu cha kwanza ni kutoa ofa ambayo mteja hawezi kuikataa. Hii ni ofa ambayo inajibu matatizo na maumivu ya mteja, pamoja na kumpa hatua ya kuchukua ambayo akiichukua ananufaika na asipoichukua anapoteza.

Kitu cha pili ni kuondoa hatari kwa mteja na kuileta kwako. Hapa mpe mteja uhakika wa kutokupoteza kwa kumwambia kama atakachonunua hakitamfaa siyo tu atakirudisha na kupata fedha yake, bali pia atalipwa kwa usumbufu aliopata.

Kitu cha tatu ufungaji wa nguvu. Hapa ni jinsi unavyofunga nakala yako ya mauzo. Unapaswa kuifunga kwa hatua ambazo mteja anapaswa kuzichukua na kwa namna anavyopaswa kuzichukua. Usimwache mteja hewani baada ya kuwa umeshamweleza kila kitu, badala yake mweleze kila anachopaswa kufanya na matokeo ambayo ayatarajie.

Kwenye kila nakala yako ya mauzo, hakikisha vitu hivyo vitatu vipo na vinaeleweka kwa urahisi na wateja wako na hilo litafanya uuze zaidi.

Rafiki, zingatia mambo haya sita tuliyojifunza hapa ili uweze kuwa na uandishi wenye ushawishi na unaowasukuma watu kuchukua hatua.

Kwenye #MAKINIKIA YA JUMA tutajifunza AINA 9 ZA OFA UNAZOPASWA KUMPA MTEJA KWENYE UANDISHI WAKO na VIPENGELE 11 VYA NAKALA YA UZINDUZI WA BIDHAA AU HUDUMA WENYE MAFANIKIO. Kupata makinikia haya jiunge na channel ya TANO ZA JUMA, maelezo ya kujiunga yapo mwisho wa makala hii.

#3 MAKALA YA JUMA; HATUA SITA ZA KUANDIKA NAKALA INAYOUZA.

Kuna hatua sita za uandishi wa nakala za mauzo zenye ushawishi mkubwa kwa wale unaowalenga.

Hatua hizi sita zinagusa maeneo yote muhimu ambayo yanamsukuma yule unayemlenga kuchukua hatua, lakini pia zinampa mtu huyo hatua ambayo anapaswa kuichukua.

Kwa kujua hatua hizi sita na kuzitumia kila wakati unapoandika na hata kuongea, utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Hatua hizi sita unaweza pia kuzitumia kwenye uandishi wa ujumbe mfupi wa simu, uandishi wa barua za kawaida au barua pepe, uandishi wa makala na hata uandishi wa kitabu.

Zijue hatua hizi sita kwa kusoma makala ya juma ambayo ipo hapa; Uza Zaidi; Hatua Sita (06) Za Kuandika Nakala Ya Mauzo Inayowavutia Watu Kusoma Na Kushawishika Kununua Unachouza.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku kwa makala mpya na nzuri zaidi.

#4 TUONGEE PESA; TENGENEZA KIPATO KUPITIA UANDISHI.

Watu wengi wamekuwa wanasema kwamba uandishi haulipi. Watu hao wanakuwa wamehangaika sana katika uandishi lakini hawajapiga hatua kwenye maisha yao. Na watu hao wanakuwa sahihi kwa sababu moja, wanaandika kawaida, hawana mfumo bora wa uandishi ambao utawawezesha kutengeneza kipato kikubwa kwao.

Ukweli ni kwamba kuna fursa nyingi sana za kutengeneza kipato kupitia uandishi. Ni fursa nyingi mno, kiasi kwamba kama mtu akiamua kujifunza na kuchukua hatua, basi anaweza kutengeneza kipato kikubwa sana kwenye maisha yake.

Zifuatazo ni njia unazoweza kutumia kutengeneza kipato kupitia uandishi.

Moja; kuandika kuhusu kazi au biashara yako. Hapa unaandika nakala za mauzo, zinazowavutia watu kwenye kazi au biashara unayofanya na kuwashawishi kuja kununua kile unachotoa. Kadiri unavyoweza kandika vizuri, ndivyo unavyoweza kuwavutia wengi na kuuza zaidi.

Mbili; kuwaandikia wengine. Popote pale ulipo, kuna watu wana bidhaa au huduma nzuri sana, zinazoweza kuwasaidia wengine kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao, lakini hawajaweza kuwafikia watu wengi. Hapo kuna fursa ya wewe kuijua vizuri bidhaa au huduma hiyo, kisha kuandika nakala za mauzo na kila anayenunua bidhaa au huduma kupitia nakala zako, basi mtu huyo anakupa wewe kamisheni. Angalia ni bidhaa au huduma zipi unaweza kuzifanyia hivyo, ingia makubaliano na wahusika na anza kuandika nakala za mauzo.

Tatu; kuwa mwandishi na kuuza kazi zako za uandishi. Unaweza kuwa mwandishi kwenye eneo lolote unalochagua, na kwa kujifunza njia bora za uandishi wenye ushawishi, ukaweza kuwavutia watu kusoma kazi zako na hata kuzinunua pia. Hapa unaweza kuwa na vitabu, kozi au huduma nyingine kama za ushauri ambapo utawavutia watu kuzipata kupitia uandishi wenye ushawishi.

Rafiki, hapo ulipo sasa, unaweza kutumia uandishi wa nakala za mauzo kama sehemu ya kuingiza kipato cha pembeni. Jifunze na kuwa mwandishi bora, andika sana na kuwa na mpango bora wa kutengeneza kipato kupitia uandishi wako.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UJUZI ULIOZALISHA MAMILIONEA WENGI DUNIANI.

“There is virtually no other skill that can make you as much money as copywriting. Nearly all internet millionaires know this secret: more than their product, more than their traffic generation techniques, more than their email campaigns, more than who their joint-venture partners might be, it’s their copywriting that has made them rich.” – Ray Edwards.

Upo ujuzi mmoja ambao umezalisha mamilionea wengi dunia kuliko ujuzi mwingine wowote ule. Ujuzi huo ni uandishi wa nakala za mauzo (copywriting). Kama umewahi kuona tangazo la bidhaa kwenye tv, redio au gazeti na likaingia kwenye fikra zako kiasi cha kuwa unafikiria tangazo hilo muda mwingi basi jua kuna watu walikaa chini na kuandika tangazo hilo, ili kukulenga wewe.

Kama umewahi kusoma maelezo ya kitu fulani na ukatoka ukiwa na hamasa na kuchukua hatua mara moja, basi jua hapo kuna watu wamekaa chini kaundika kitu kinachokulenga wewe, wakiwa wana hatua ambayo wanataka wewe uchukue.

Uandishi wa nakala za mauzo, ni moja ya ujuzi ambao unalipa zaidi duniani, hasa pale mtu anapoweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu. Jifunze uandishi wenye ushawishi kama tulivyojifunza kwenye kitabu cha juma hili na utaweza kuongeza kipato chako maradufu.

Rafiki, hizi ndizo tano za juma hili la 31 la mwaka 2019, tumejifunza kwa kina kuhusu uandishi wa nakala za mauzo, moja ya njia ambazo kila mmoja wetu anaweza kutumia kukuza zaidi kipato chake. Nenda kayaweke kwenye matendo haya uliyojifunza na hutabaki hapo ulipo sasa.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili tunakwenda kujifunza AINA 9 ZA OFA UNAZOPASWA KUMPA MTEJA KWENYE UANDISHI WAKO na VIPENGELE 11 VYA NAKALA YA UZINDUZI WA BIDHAA AU HUDUMA WENYE MAFANIKIO. Pia kwenye channel ya TANO ZA JUMA nitashirikisha kitabu cha Brian Tracy kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF SELLING, ambacho kitakusaidia sana kubobea kwenye mauzo. Jiunge na channel ya TANO ZA JUMA leo uendelee kujifunza na kunufaika zaidi. Maelezo ya kujiunga yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu