“The person who has practiced philosophy as a cure for the self becomes great of soul, filled with confidence, invincible—and greater as you draw near.”
SENECA, MORAL LETTERS, 111.2
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FALSAFA NI TIBA YA NAFSI…
Angalia wakati wowote ambao umewahi kujikuta kwenye matatizo na changamoto kubwa kwenye maisha yako, ni wakati ambao hukuwa na msingi unaouishi au ulipuuza misingi yako.
Angalia watu wote wanaopitia magumu na changamoto kubwa kwenye maisha yao na utaona hakuna misingi wanayoishi kwenye maisha yao, au kama wanayo basi hawaifuati.
Unapokuwa huna msingi unaosimamia kwenye maisha yako, au ukawa na msingi lakini ukaupuuza, basi unakaribisha matatizo na changamoto za kila aina.
Na wengi wanapojikuta kwenye matatizo na changamoto hizo, wanakimbilia kuchukua hatua ambazo zinafanya mambo kuzidi kuwa magumu zaidi.
Jawabu la yote, tiba ya matatizo na chamgamoto zote ni falsafa.
Unapokuwa na falsafa unayoisimamia na kuiishi, siyo kwamba hutakutaha na matatizo au changamoto, bali matatizo na changamoto utakazokutana nazo hazitakuyumbisha.
Kwanza hazitakutokea kwa mshangao, kwa sababu ulitegemea zitokee na pili utachukua hatua sahihi kukabiliana nazo, bila ya kujali ni kubwa au ngumu kiasi gani.
Kwa falsafa yetu tunayoiishi kwenye KISIMA CHA MAARIFA, falsafa ya Ustoa, kila wakati unakuwa kwenye maandalizi, kwa kujua lolote usilotegemea litokee linaweza kutokea.
Na pale unapokutana na matatizo au changamoto huruhusu zikuvuruge,
Badala yake unajiuliza kama ipo njia ya kutatua changamoto hiyo,
Kama jibu ni ndiyo basi unachukua hatua ya kutatua.
Kama jibu ni hapana basi unaachana nayo na kuendelea na mambo mengine.
Unaona jinsi maisha yanavyokuwa rahisi ukiishi kwa misingi ya falsafa?
Huhitaji kujiumiza wala kujipa msongo, ni kuchukua hatua kama kuna unachoweza kufanya au kuachana nayo kama hakuna cha kufanya.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi kwa misingi ya falsafa ili kuweza kupata tiba sahihi ya nafsi yako.
Na mara zote unapojikuta kwenye matatizo au changamoto, kabla hujakimbilia kufanya chochote, rudi kwanza kwenye misingi ya falsafa.
#FalsafaTibaYaNafsi #IshiKwaMisingi #UsihangaikeNaYaliyoNjeYaUwezoWako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1