“Indeed, how could exile be an obstacle to a person’s own cultivation, or to attaining virtue when no one has ever been cut off from learning or practicing what is needed by exile?”
—MUSONIUS RUFUS, LECTURES, 9.37.30–31, 9.39.1
Kuiona siku nyingine mpya na nzuri kama ya leo ni jambo la kushukuru sana.
Tunapaswa kushukuru kwa sababu kuiona siku hii ni bahati kwetu, siyo nguvu wala akili zetu.
Na njia pekee ya kulipa bahati hii ni kuitumia vyema siku hii ya leo, kwa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi na kuacha kupoteza muda kwa mambo yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIKWAMISHWE NA CHOCHOTE.
Usikubali kitu chochote kinachotokea kwenye maisha yako kiwe kikwazo kwako kujifunza zaidi, kuwa mtu mwema na kufanya kazi zako.
Unaweza kupanga vizuri mambo yako, lakini kinachokuja kutokea ni tofauti kabisa na ulivyopanga.
Usiruhusu matokeo ya tofauti unayopata yawe kikwazo kwako kuwa wewe.
Kwa kila kinachitokea, hakikisha unapata fursa ya kujifunza, unapata fursa ya kuwa mtu mwema na unapata fursa ya kuifanya kazi yako.
Hata kama umefungwa au kuwekwa kizuizini, bado unao uhuru wa fikra zako, wa kuchagua ufikiri nini katika hali kama hiyo. Chagua ni nini unajifunza, nini unafikiri na hatua zipi unapiga bila ya kujali upo katika hali gani.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukazana kujifunza, kuwa bora na kuifanya kazi yako bila ya kujali ni matokeo gani unayokutana nayo leo.
#UsikwamishweNaChochote #KazanaKuwaBoraKilaSiku #IfanyeKaziYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1