“Silence is a lesson learned from the many sufferings of life.”
—SENECA, THYESTES, 309
Shukrani ndiyo kitu pekee tunachoweza kutoa kwa nafasi hii nzuri tuliyoiona leo.
Siyo kwa akili zetu, wala nguvu zetu, bali ni kwa bahati tu.
Kuhakikisha tunaitumia vizuri nafasi hii ya leo, nafasi ambayo wapo wengine wangekuwa tayari kukipa mabilioni waione, lakini haijawezekana, ni kwenda kufanya yale muhimu na kuepuka kupoteza muda kwenye mambo yasiyo muhimu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UKIMYA UNA NGUVU KUBWA…
Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anapiga kelele na hakuna aliye tayari kusikiliza.
Hili limefanya watu wakose fursa nzuri za kujifunza,
Lakini pia limesababisha wengi kuharibu fursa mbalimbali ambazo wamezipata.
Ukimya una nguvu kubwa sana ambayo ukiweza kuitumia basi utaweza kupiga hatua kubwa.
Ukimya unakupa nafasi ya kusikiliza na unaposikiliza kwa kina basi unajifunza mengi, kwa sababu kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mtu.
Ukimya unawafanya watu waone wewe ni mtu makini na kukuchukulia kwa uzito wa hali ya juu. Unapokuwa kimya, watu hawawezi kujua uko upande upi au una mtazamo gani juu ya jambo fulani, hivyo wanakuchukulia kwa umakini. Lakini unapokuwa mwongeaji sana, unaweka kila kitu wazi na watu wanakuwa hawapati tabu ya kujua upo upande upi au una mtazamo gani.
Mtu mmoja amewahi kusema, mtu mpumbavu akikaa kimya, anadhaniwa ni mtu mwenye hekima. Kumbe basi kuwa mtu mwenye hekima haihitaji hata uwe na uwezo mkubwa sana kiakili, inahitaji uweze tu kukaa kimya.
Mtu mwingine akasema, kadiri unavyoongea sana, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kusema kitu cha kipumbavu. Na ukiangalia iko wazi, mtu anaanza kuongea vitu vya maana, lakini hanyamazi, anaendelea kuongea na mwishoni anaongea vitu ambavyo vinavuruga kabisa aliyoongea mwanzo.
Ukimya una nguvu kubwa sana, kama utaweza kuutumia vizuri. Siyo ukimya wa kuamua tu kukaa kimya, bali ukimya wa kusikiliza, ukimya wa kujifunza na ukimya wa kusema yale muhimu na kisha kukaa kimya.
Usitake kuongea kwa sababu kila mtu anaongea au kwa sababu ni zamu yako kuongea,
Bali ongea kwa sababu una kitu muhimu cha kusema, na ukishakisema ishia hapo na kaa kimya.
Unafikiri kwa nini tumepewa mdomo mmoja na masikio mawili?
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia nguvu ya ukimya katika kujifunza na hata kujenga sifa yako mbele ya wengine.
#UkimyaUnaNguvu #OngeaKidogoSikilizaZaidi #SiyoLazimaKuwaNaMaoniKwaKilaJambo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1